Friday, February 26, 2016

ISHU YA KUNYWA MAJI ILI UWE MWEUPE NI FUNZO JIPYA KWA RAY!

Msanii wa Filamu Bongo Vicent Kigos 'Ray', akiangalia kitu kwenye Laptop yake huku maji yakiwa pembeni yake.
NCHI za wenzetu hususani Marekani ambako biashara ya burudani imeendelea, mastaa wamekuwa wakitengeneza ‘kiki’ mbalimbali ili kuifanya jamii iwafuatilie kwa wakati huo.

Tumeshuhudia watu kama kina Jay Z na Beyonce wakitangazwa kuwa wanaachana, baada ya muda mfupi unasikia mmoja wao ameachia albamu au wimbo mpya.

Unaibuka uhusiano wa staa fulani na staa fulani ambao awali haukuwepo, ukifuatilia kwa makini, utagundua hakuna uhusiano. Zilikuwa ni mbwembwe tu za kiki ya muvi kama si wimbo mpya ambao walipanga kuuachia.

Si kwamba hawana uwezo katika kazi zao, wanafanya hivyo ili kukifanya kile kitu wanachokwenda kukizindua, kiwe gumzo kwa wakati huo na kusababisha kila mtu kuzungumzia ujio huo mpya wa kazi ya msanii husika.

Wanapofanya hivyo, kwenye mitandao ya kijamii, redio na televisheni vyote vinakuwa vikijadili kituko kilichofanywa na staa husika hivyo kwa wakati huo ni rahisi sana mashabiki kuzidi kuweka mhemko wa kazi ya staa huyo.

Hilo limekuwa likifanyika pia Bongo. Wapo baadhi ya wasanii wamekuwa wakifanya jambo pale wanapotaka kutoa kazi mpya. Mifano ipo mingi, nikukumbushe mdogo wa hivi karibuni. Linex aliibuka na picha za harusi, kila mtu akajua ameoa kumbe hamna lolote, ilikuwa kiki ya wimbo mpya.

Takriban wiki moja sasa, staa wa sinema za Kibongo, Vincent Kigosi ‘Ray’ amefanikiwa kuipata kiki ya kwenye mitandao na vyombo vya habari.

Hiyo yote ilitokana na kuulizwa swali lililomtaka aeleze nini sababu ya yeye kubadilika muonekano na kuwa mweupe tofauti na zamani ndipo alipoibua taharuki kwa kusema maji ndiyo yamefanya awe mweupe.

Ndani ya dakika chache tangu atoe jibu hilo, nchi nzima ‘ililipuka kwa maji’. Watu kutoka Mbeya, Songea, Mtwara, Kigoma na kwingineko waliiga tabia ya kunywa maji. Wakatupia picha zilizowaonesha wakinywa maji.

Hata ambaye hakusikia jibu la Ray, alichukuwa muda wake kuchimba undani wa sakata hilo. Alimfuatilia Ray katika mitandao yake ya kijamii na kusababisha jamaa apate wafuasi wengi katika mtandao wake wa Instagram.

Wakati jambo hilo linaibuka, tayari Ray alikuwa ameachia muvi yake ya Tajiri Mfupi sokoni. Bahati mbaya muvi hiyo haikuweza kufahamika kabla sababu watu wengi walikuwa hawamtembelei mtandaoni kwake na hawamsikii kwenye vyombo vya habari.

Alikuwa hafanyi mahojiano kivile. Umaarufu ulianza kupungua. Ray yule aliyekuwa akichuana vikali na Steven Kanumba (Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi) kwa kununua magari ya kifahari, sijui ana bifu na fulani si huyu wa sasa.

Ray wa sasa amekuwa kimya. Wateja wake wanaofuatilia kazi zake katika vyombo vya habari hawamsikii. Hawajui kama ana mpango wa kwenda kufanya muvi nje ya nchi wala kujua anatarajia kuoa lini? Yupo na nani?

Baada ya kiki ya maji kushika hatamu, jina lake limerudi kwenye mstari. Ray amekuwa ‘keki’, anajadiliwa kila kona. Siku mbili hazikutosha kumjadili kwenye mitandao, wiki nzima na zaidi sasa bado anaendelea kuzungumzwa.

Uzuri ni kwamba mwenyewe ameonesha ushirikiano katika suala la maji, hakuweka hasira, basi si vibaya kama atalichukuwa jambo hilo kama somo kwa manufaa ya sanaa yake.

Ukimya usiwe wa muda mrefu. Fanya jambo watu wazidi kukufuatilia na kukujadili. Huo ndiyo ustaa. Naamini kutokea hapo alipo na kuendelea, tutamshuhudia Ray katika anga nyingine kama ataamua ‘ku-maintain’ maana uwezo anao, jina lake ni kubwa kwenye sanaa na lina historia yake!

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...