Tuesday, December 31, 2013

FRANCIS MIYEYUSHO,JOSHUA AMUKULU KUZICHAPA LEO MSASANI CLUB


Bondia Joshua Amukulu(kushotO) wa Kenya akitunishiana misuli na Fransis Miyeyusho wakati wa upimaji uzito kwa ajili ya pambano lao litakalofanyika kesho Dec 31 katika ukumbi wa Msasani Club.

Bondia Kalama Nyilawila(kushoto) na Ibrahimu Maokola baada ya kupima uzito kwa ajili ya mpambano wao wa utangulizi katika pambano la Miyeyusho na Joshua.

Bondia Fransic Miyeyusho akipima uzito .

Miyayusho akihojiwa.

Bondia Ibrahimu Class 'king Class Mawe' kushoto akitunishiana misuli na Mustafa Dotto.
NJEMBA ALIYEKUWA AKITAKA KUONANA NA RAIS KWA NJIA YA KUNG'ANG'ANIA JUU YA MNARA WA SIMU UBUNGO HATIMAYE ASHUSHWA


 
Jamaa mmoja ambaye jina lake halijaweza kupatikana leo majira ya saa 5 na nusu asubuhi alipanda juu ya mnara wa kampuni ya simu Vodacom mkabala na ofisi ya Tbs,alipokuwa juu ya mnara alikua na picha pamoja na document mbalimbali ambazo alisema hashuki mpaka Rais Jakaya Kikwete afike eneo hilo.

Baadhi ya mashuhuda wanasema kuwa jamaa ni mpiga debe maeneo ya ubungo na madai yake alifungwa jela miaka 6 bila hatia hivyo moja ya sababu zilizofanya apande juu na kuhitaji kuonana na rais kwa ajili ya kuzungumza nae.
 
Kikosi cha Zimamoto na uokoaji walifanikiwa kumshusha majira ya mchana huu na kumpeleka moja kwa moja kituo cha polisi.

NAPE:CCM TUNAIPONGEZA TUME YA KATIBA MPYAYasema itatafakari na kuamua ipasavyo hoja za Tume
Yasisitiza mchakato utumike kuwaunganisha WatanzaniaChama Cha Mapinduzi kimeipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini kwa kazi iliyofanya kuufikisha mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya hapa ulipofika. Akizungumza katika mahojiano maalumu na baadhi ya waandishi wa habari mara baada ya Tume kuwasilisha rasimu ya pili ya katiba Nape alisema;


“CCM inaipongeza Tume kwa kazi waliofanya, tunatambua kazi kubwa waliyofanya, wamekamilisha kazi waliyotumwa salama na kwa wakati. Sasa tuwaachie wanaondelea na mchakato yaani bunge la katiba na hatimaye wananchi. Tunautakia kila lakheri mchakato huu, utumike kutuunganisha watanzania badala ya kutugawa” amesema Nape.

Kuhusu pendekezo la Tume la muundo wa Muungano wa serikali tatu Nape anasema; “Tumesikiliza hoja za tume juu ya sababu za kuendelea kupendekeza muundo wa serikali tatu, tumezisikia, tutazichukua,kuzipeleka kwenye vikao vya Chama baada ya tafakuri ya kutosha tutaamua ipasavyo” alisisitiza Nape.Aidha Nape alitumia nafasi hiyo kuwatakia watanzania kila lakheri kwenye mwaka mpya wa 2014

AGNES MASOGANGE KUUZA NYAGO KWA MARA YA KWANZA KWENYE VIDEO YA TUNDAMANMsanii wa muziki wa kizazi kipya nchini Khalid Ramadhani Tundamani anatarajia kumwonyesha kwa mara ya kwanza 'Video queen' Agnes Gerad maarufu Masogange katika video ya wimbo wake wa Msambinungwa. Akiongea Tundaman alisema ataondoka nchini Januari 5, 2014 kwenda Nairobi kwa ajili ya utengenezaji wa Video hiyo na kwamba ameamua kufanya video hiyo akiwa na Masogange kwani ni msichana anayefanya vizuri katika video nyingi za wasanii pia ana kipaji cha kazi hiyo.

RASIMU INAYOONYESHA UWEPO WA SERIKALI TATU YATUA KWA JK


Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba akimkabidhi Rais Jakaya Kikwete (kulia) Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya siku ya jana.
Jaji Warioba akimkabidhi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kushoto) Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya siku ya jana.

Rais Jakaya Kikwete (kulia) akiteta jambo na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba.
Jaji Warioba akisoma ripoti ya Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya siku ya jana.

MUUNDO wa serikali tatu umeendelea kuwa ndani ya Rasimu ya Katiba iliyokabidhiwa jana kwa Rais Jakaya Kikwete kutokana na ambacho Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema ndiyo itakuwa suluhu ya malalamiko juu ya kero za Muungano.

Akikabidhi Rasimu hiyo jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Tume, Jaji Joseph Warioba, alisema baada ya kukaa na kupitia malalamiko juu ya muundo wa sasa wa Muungano na takwimu za waliotoa maoni, imeona serikali tatu zinakidhi matakwa ya Watanzania wengi.
Uamuzi wa Tume umefanyika baada ya kupokea maoni kutoka kwa makundi ya watu zikiwamo taasisi za serikali, ambao asilimia kubwa ikiwemo Ofisi ya Waziri Mkuu, walionesha kuhitaji muundo huo wa Muungano.

Akiwasilisha taarifa ya Tume kwa Rais Jakaya Kikwete na Rais Ali Mohamed Shein, Jaji Warioba alisema katika maoni yaliyotolewa, takwimu zinaonesha upande wa Tanzania Bara, asilimia 61 walipendekeza serikali tatu; asilimia 24 mbili na asilimia 13 moja.

Kwa upande wa Zanzibar, asilimia 60 walipendekeza Muungano wa Mkataba, asilimia 34 serikali mbili na asilimia 0.1 serikali moja. Aidha, taasisi nyingi kama vile vyama vya siasa, asasi za kiraia na jumuiya za kidini zilipendekeza muundo wa serikali tatu.

Miongoni mwa taasisi za serikali zilizopendekeza mfumo wa serikali tatu, ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambazo katika maoni yao, zilisema muundo huo utaondoa kero za Muungano.
Kwa upande wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, lilipendekeza kuwapo kwa Mamlaka huru ya Zanzibar, Mamlaka huru ya Tanganyika na Mamlaka ya Muungano kila moja ikiwa na mipaka yake.

Jaji Warioba akieleza namna Muungano ulivyoteka mjadala wa Rasimu ya Awali ya Katiba, alisema kwa Tanzania Bara, wananchi zaidi ya 39,000 walitoa maoni kuhusu eneo hilo.

“Wananchi karibu wote waliotoa maoni, walijikita kwenye suala la Muungano. Kati ya wananchi karibu 38,000 waliotoa maoni, 19,000 walitoa maoni kuhusu Muungano,” alisema.
Malalamiko Bara, Zanzibar

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, baada ya kuona takwimu za waliotoa maoni na kuzichanganua, Tume iliamua kufanya utafiti kuhusu muundo wa Muungano na kubaini malalamiko mengi kuhusu Muungano.
Akitaja malalamiko waliyobaini, Jaji Warioba alisema kwa upande wa Zanzibar, yapo malalamiko makubwa matatu ambayo ni Serikali ya Tanganyika kuvaa koti la Serikali ya Muungano linalosaidia Tanganyika zaidi kuliko Zanzibar.

“Koti hilo limeifanya Tanganyika kuwa ndiyo Tanzania,” alisema. Mengine ni kuongezeka kwa mambo ya Muungano na hivyo kuathiri madaraka ya Zanzibar na kufifisha hadhi yake hivyo kuendelea kumezwa. Wazanzibari wanalalamikia pia kumwondoa Rais wa Zanzibar kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Kwa upande wa Bara, malalamiko makubwa yaliyobainishwa na Tume ni wananchi wa Bara kutokuwa na haki ya kumiliki ardhi Zanzibar wakati wenzao wa Zanzibar wana haki hiyo Bara.
Malalamiko mengine ni Zanzibar kuwa nchi huru, yenye bendera, wimbo wake, serikali na imebadili Katiba yake ili ijitambue kama nchi, wakati Tanzania Bara imepoteza utambulisho wake.
Vile vile wanalalamikia Zanzibar kwamba imebadili Katiba na kuchukua madaraka ya Jamhuri ya Muungano kama vile kuelekeza sheria za Muungano zilizopitishwa na Bunge zipelekwe kwenye Baraza la Wawakilishi kujadiliwa.

Tume baada ya kufanya uchambuzi wa malalamiko hayo, ikaona ni vigumu kuyafanyia ukarabati hivyo ikaona ipendekeze muundo wa serikali tatu ili pande zote mbili ziwe na hadhi sawa.
“Kila upande utashughulikia mambo yasiyo ya Muungano na Serikali ya Muungano itabaki na mambo machache ya msingi na ambayo yanaunganisha Taifa,” alisema.
Uraia

Hata hivyo, Jaji Warioba alisema Tume imetambua kuwa muundo huo una changamoto zake, hivyo ili kujikinga nazo, imependekeza mambo matatu likiwamo la uraia kubaki kuwa mmoja.
Imependekeza raia wote wa Jamhuri wawe huru na wawe na haki zote za kisiasa, kiuchumi na kijamii katika nchi nzima isipokuwa katika mazingira maalumu.
“Haki zao zikiingiliwa na upande wowote bila sababu maalumu, itasababisha kuibuka kwa utaifa, utanganyika au uzanzibari na uzalendo utayumba. Uzalendo ukiyumba, Muungano pia utayumba,” alisema.

Licha ya uraia, lingine ni Serikali ya Muungano kuwa na uhakika wa mapato kwa ajili ya kulipia gharama za Muungano ambapo Tume imependekeza ushuru wa bidhaa uwe ni kodi ya Muungano.
Kodi hiyo itakidhi sehemu kubwa ya matumizi ya Muungano na sehemu iliyobaki itapatikana kutokana na mapato yasiyo ya kodi yanayotokana na mambo ya Muungano, michango ya nchi washirika na mikopo.

Tatu ni kuundwa kwa Tume ya Uhusiano na Uratibu wa Serikali chini ya uenyekiti wa Makamu wa Rais wa Muungano na ijumuishe viongozi wakuu wa nchi washirika.
Majukumu ya Tume ni kusimamia mashauriano na ushirikiano kati ya Serikali ya Muungano na za nchi washirika ili kuhakikisha sera zinawiana na pia kusimamia na kuimarisha masuala yenye maslahi kwa Taifa na pia kutatua migogoro.
Kazi ngumu

Jaji Warioba ambaye alikiri suala la Muungano kuwa moja ya mambo yaliyojadiliwa kwa hisia kali tangu Rasimu ya awali ilipotolewa, alisema kazi ya kukusanya maoni na kuibuka na mapendekezo hayo katika Rasimu hii, haikuwa rahisi ikizingatiwa wajumbe wa Tume wametoka katika makundi tofauti.
Alisema, “kila mmoja wetu alikuwa na imani yake, maoni yake, itikadi yake, msimamo wake. Lakini tulikubaliana mapema kabisa, kwamba wajibu wetu ni kwa Taifa. Kwa hiyo tuliacha imani na misimamo yetu binafsi na kuamua kusikiliza wananchi kwa makini sana.”

Aliendelea: “Majadiliano yetu yalilenga kupata mwafaka wa kitaifa. Baadhi ya mapendekezo yetu kwa hakika yatapokewa kwa hamasa kubwa. Lakini la muhimu ni kupata mwafaka wa kitaifa badala ya kufikia uamuzi kwa kujipima katika makundi.”

Kulingana na taarifa ya Mwenyekiti huyo, kama ilivyokuwa katika Rasimu ya Awali, suala la muundo wa Muungano ndilo lililochukua muda mwingi wa Tume.
CCM yapongeza

Akizungumzia Rasimu hiyo kwa niaba ya CCM, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho Tawala, Nape Nnauye, alisema wanaipongeza Tume kwa kazi kubwa iliyoifanya kwa utulivu na umakini mkubwa na sasa sehemu iliyobaki ni ya Bunge Maalumu la Katiba na kura za wananchi.
“CCM inaitakia kila la heri sehemu muhimu iliyobaki katika mchakato ifanyiwe kazi kwa busara na umakini mkubwa kama ilivyotangulia kufanywa,” alisema Nape.
CCM ambayo inaamini katika Serikali mbili, ilisema imesikiliza kwa makini taarifa ya Tume hasa katika suala la Serikali tatu na sababu zilizotolewa na kwamba inazichukua na itaziingiza katika vikao vyake, itatafakari na kutoa uamuzi unaopasa.
Uteuzi, uongozi

Katika Rasimu hii ambayo ni ndefu kuliko ya awali, madaraka ya Rais hasa ya uteuzi yamepunguzwa kwa kuweka vyombo vya kupendekeza majina ya watu wa kuteuliwa na kwa baadhi ya vyeo kuhitaji kuthibitishwa na Bunge.

Rasimu hiyo yenye ibara 271 ikilinganishwa na ya awali yenye ibara 240, hata hivyo imesisitiza Rais ndiye mwenye hadhi na heshima ya Mkuu wa Nchi, Amiri Jeshi Mkuu na Kiongozi wa Serikali.
Vile vile imependekezwa wabunge wasiwe mawaziri, kuwe na ukomo wa uwakilishi katika Bunge na wapiga kura wawe na madaraka ya kumwajibisha mbunge hata kabla ya kumalizika kwa muhula wake.

Mengine ni Spika na Naibu Spika wasitokane na wabunge au kiongozi wa juu wa chama cha siasa. Uraia ni mmoja wa Jamhuri ya Muungano ni mmoja.
Rasimu inapendekeza kutambuliwa kwa uraia wa kuzaliwa na kujiandikisha ambao ni wa nchi moja. Aidha, inapendekeza kuwapa hadhi maalumu watu wenye asili au nasaba ya Tanzania ambao wameacha kuwa raia wa Tanzania kwa kuchukua uraia wa nchi nyingine.

Marufuku kiongozi wa umma kutumia wadhifa, nafasi au madaraka kwa manufaa yake binafsi, familia yake, ndugu, jamaa, marafiki au mtu aliye na uhusiano naye wa karibu.
Vile vile Tume kwa kuzingatia maoni ya wananchi, tofauti na ilivyokuwa katika Rasimu ya Awali, sasa inapendekeza Msajili wa Vyama vya Siasa iwe ni taasisi inayojitegemea na si kuwa sehemu ya Tume Huru ya Uchaguzi.

Imependekeza pia kuwepo Jeshi la Polisi moja na Idara ya Usalama wa Taifa moja katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kipindi cha mpito

Rasimu inapendekeza muda wa mpito wa miaka minne, kuanzia tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba Mpya hadi Desemba 31, 2018; na kwamba sheria zilizopo sasa zitaendelea kutumika hadi zitakapobadilishwa.

Masuala yaliyopendekezwa yafanyiwe kazi katika kipindi cha mpito ni pamoja na kutungwa Katiba ya Tanganyika, mgawanyo wa rasilimali baina ya Serikali ya Muungano na serikali za nchi washirika.
Mengine ni kufanya maandalizi ya kuendesha uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 2014.

Kuundwa kwa tume na taasisi za kikatiba zilizoainishwa kwenye Katiba. Rasimu ya wananchi Akielezea mchakato wa maandalizi ya Rasimu hiyo, Jaji Warioba alisema tofauti na wasiwasi uliokuwapo kwa ushiriki wa wananchi wa kawaida, ungekuwa dhaifu, sura tano za mwanzo za Rasimu zinatokana na mchango mkubwa kutoka kwa wananchi.
“Tume ilipoanza kulikuwa na wasiwasi, kwamba ushiriki wa wananchi wa kawaida ungekuwa dhaifu kwa sababu iliaminika kwamba wananchi kwa ujumla wao hawana ujuzi wa Katiba,” alisema Jaji Warioba.
Aliendelea kusema: “Lakini Tume iligundua mapema kwamba wananchi wanajua mambo mengi ambayo ni msingi wa Katiba yoyote. Sura tano za mwanzo wa Rasimu ya Katiba zinatokana na mchango mkubwa kutoka kwa wananchi.”

Kwa mujibu wa Jaji Warioba, maoni ya wananchi yalihusu misingi ya Taifa, tunu za Taifa, maadili na miiko ya viongozi, dira ya Taifa na haki za binadamu.
Wananchi pia walitoa maoni mazito kuhusu uongozi na utawala wa nchi, ikiwa ni pamoja na nafasi ya wawakilishi wao bungeni.

Ilikotoka Tume Aprili 6 mwaka jana, Rais Kikwete aliteua wajumbe 34 wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Warioba na kuwaapisha Aprili 13 mwaka huo kabla ya kuanza kazi yao, Mei 2.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ilitoa miezi 18 kwa Tume kukamilisha kazi yake. Sheria pia ilitoa nafasi ya Tume kuongezwa muda usiozidi miezi miwili na iliomba muda huo ikakubaliwa kabla ya kukamilisha kazi yake jana na kuikabidhi kwa Rais

RAIS JK AMTEUA ERNEST MANGU KUWA MKUU WA JESHI LA POLISI TANZANIA


 
Kamishna wa Polisi Ernest Mangu aliyeteuliwa na Rais Kikwete kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Desemba 30, 2013, amemteua Kamishna wa Polisi Ernest Mangu kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini.

Taarifa iliyotolewa usiku wa leo na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa Kamishna Mangu anachukua nafasi ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini anayestaafu, Saidi Mwema.

Kabla ya uteuzi wake unaoanza keshokutwa, Januari Mosi, 2014, Kamishna Mangu alikuwa Mkurugenzi wa Inteligensia ya Jinai (Director of Criminal Intelligence)katika Jeshi hilo la Polisi.

Aidha, taarifa hiyo inasema kuwa Rais Kikwete amemteua Kamishna Abdulrahman Kaniki kuwa Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi, ambayo ni nafasi mpya katika muundo wa sasa wa Jeshi la Polisi.

Kabla ya uteuzi wake, Kamishna Kaniki alikuwa Kamishna wa Uchunguzi wa Kijinai (Commissioner for Forensic Investigations).

Mkuu wa Jeshi la Polisi mpya ataapishwa kesho, Jumanne, Desemba 31, 2013 katika Viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam. Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.

Saturday, December 28, 2013

SOMA WARAKA WA ABSALOM KIBANDA KWENDA KWA RAIS DK.KIKWETE
Absalom Kibanda.
Rais Jakaya Kikwete alipofika Kumjulia Hali Absalom Kibanda nchini Afrika ya kusini Mwezi tarehe 8-2013.
MHESHIMIWA Rais wangu, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete. Nakusalimu kwa salamu ya utii inayotambua na kuheshimu kwa dhati mamlaka makubwa na ya juu uliyonayo kama mkuu wa taifa letu ambalo mazingira yake ya leo yanapaswa yawe wenye mwelekeo wa kushangilia kama si kujivunia uhuru ambao tuliupata mwaka 1961 na 1964 kwa kutegemea upande tulipo katika muungano wetu.

Mheshimiwa Rais, najisikia faraja iliyojaa majonzi moyoni kupata fursa hii adhimu kukuandikia waraka ambao msukumo wake unasukwasukwa na dhamira njema kabisa ambayo aghalabu kiini chake si kingine bali mapenzi mema kwa nchi na viongozi wetu wote.

Ni faraja kwa kuwa nimepata fursa ghali na adimu ya kuteta na kiongozi wetu mkuu kwa upendo, uhuru na kwa kujiamini, huku nikiwa na uchungu pia kwa sababu ujumbe ambao unabebwa na waraka huu ni wa kuumiza sana nafsi, roho, akili na mwili.

Mheshimiwa Rais, wewe ni kiongozi wa Watanzania wote tukiwamo sisi ambao baadhi ya wateule wako wameamua kwa sababu wanazozijua wao na wakati mwingine wakidai kwa maelekezo ya wakuu wao kutujengea taswira zinazotufanya tuonekane tu watu wa ovyo na kada ya wanajamii waliokosa utu na eti tunaopaswa kufundishwa hekima na somo la uzalendo ambalo limekuwa sehemu ya makuzi yetu nyumbani, shuleni, jeshini na ndani ya jamii.

Kabla sijafikisha ujumbe ambao nimeubeba kwa mfano wa mzigo mzito moyoni, napenda kwanza kupitia fursa hii kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na neema kwa kuniwezesha kuuona mwanga wa siku hii njema ya leo ambayo kama si kwa kudra na mapenzi yake, yumkini ingeongeza hesabu za siku ambazo kiwiliwili changu kingekuwa katika kaburi la sahau ambalo kila kukicha linameza roho za makumi kama si mamia ya Watanzania wasio na hatia wanaopoteza maisha kutokana na kazi za mikono ya majahili, miungu watu waliojitwalia haki ya kuchagua aina ya maisha na vifo vya watu wengine.

Baada ya hilo, kwa niaba ya mamilioni ya Watanzania wenzangu ambao hawana fursa ya kuwasiliana nawe kwa njia kama hii ya waraka niliyoitumia, napenda kutumia pia wasaa huu kukushukuru wewe binafsi kwa namna ulivyojitoa usiku na mchana pasipo kuchoka kuliongoza taifa hili katika mazingira magumu yaliyojaa changamoto za kila namna ambazo wakati mwingine sina shaka hata kidogo kwamba zimekuwa zikikunyima raha na kukosa usingizi.

Wakati nikikuandikia ujumbe huu, picha na taswira yako inayonijia ni ile ya Machi 8, mwaka huu siku uliponitembelea kando ya kitanda nilichokuwa nimelazwa katika Hospitali ya Milpark, Johanesburg kule Afrika Kusini ikiwa ni siku mbili tangu nilipovamiwa, nikajeruhiwa na kupewa ulemavu na majahili ambao hadi leo hii wameweza kuukwepa mkono mrefu wa vyombo vya dola unavyoviongoza.

Mheshimiwa Rais, japo nilikuwa nina maumivu makali na machungu ya kupoteza jicho, kidole na kupasuliwa kwa mifupa ipatayo minane katika paji langu la uso, ukiacha taya lililoachanishwa kikatili na watesi wangu wale, bado ninaweza kukumbuka kwa ufasaha namna ulivyozungumza nami ukionyesha jinsi ulivyokuwa ukiguswa na kuumizwa sana na tukio lile.

Ni jambo la bahati mbaya sana kwamba, tangu niliporejea nchini miezi sita iliyopita sijapata kukutana nawe ana kwa ana ingawa nilipata fursa ya kukutumia salamu zangu za shukrani kupitia kwa marafiki zako kadhaa akiwamo msaidizi na mshauri wako nambari moja, Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal ambaye siku zote wakati nikiwa katika matibabu nchini Afrika Kusini na hata baada ya kurejea nchini, alionekana kuwa mtu wa kukosa amani kabisa pasipo kunijulia hali kwa njia ama ya simu, wasaidizi wake na mwisho kwa kuonana nami ana kwa ana.

Nayarejea haya yote huku nikitambua kwamba, wakati ninapoandika waraka huu ndiyo kwanza umerejea kutoka nchini Marekani ambako ulikwenda kuchunguzwa afya yako ambayo nina matumaini makubwa ni njema hasa kwa kuzingatia ukweli kuwa, ulikwenda huko siku chache tu baada ya kuiwakilisha vyema nchi yetu katika msiba mzito wa shujaa wa mapambano ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini, mzee wetu, Nelson Mandela.

Ninapoyatafakari matibabu ghali niliyopata nchini Afrika Kusini kwa msaada wa mwajiri wangu na safari yako nchini Marekani, vinanikumbusha swali la mmoja wa wasaidizi wangu hapa ofisini aliyetaka kujua ni sababu gani hasa ambazo zimekuwa zikisababisha wasomi na viongozi wetu kuchunguzwa na kutibiwa katika hospitali za nje, tofauti na ilivyokuwa kwa Madiba ambaye kwa nyakati zote tangu afya yake ianze kumtatiza alikuwa akipata matibabu huko huko kwao Afrika Kusini?

Niseme kweli, japo nilikuwa na jibu au majibu ya swali lake, sikuwa na maelezo ya kutosheleza yaliyokuwa na mwelekeo wa kukata kiu ya swali lake, ingawa kwa kupapasa nilifanya kila juhudi kuutetea utaifa wangu na viongozi wake ilhali miye mwenyewe nikiendelea kukosa raha kwa namna nilivyokuwa nikitoa majibu ambayo yalikuwa yakionyesha hali ya kuukubali unyonge, kukiri ufukara, kuficha udhaifu wetu kama taifa na kutetea makosa ambayo aghalab ninyi viongozi wetu na wale wa kabla yenu mngeweza kuwa watu mliostahili kuwa na majibu halisi.

Rais wangu, swali na majibu vilisababisha kimoyomoyo, nijiulize maswali mengi mengine na moja ya maswali hayo yakiwa ni wapi tulipopotea njia hata tukafikia hatua ya kusababisha kuwa na kundi kubwa la watu waliokata tamaa, wanaoteswa na ufukara, ukosefu wa ajira na kila aina ya kero na karaha zinazozonga maisha yao ya kila siku.

Mheshimiwa Rais, hali hiyo ilinipeleka moja kwa moja nchini Afrika Kusini na hususan katika Hospitali ya Milpark ambako huko ndiko miye mwenyewe na Watanzania wenzangu wengine tulikonusuru maisha yetu, huku baadhi kama ilivyo kwa Dk. Sengondo Mvungi wakipoteza maisha yao baada ya kukimbizwa huko.

Mheshimiwa Rais, naomba unisamehe kwa kulisema hili nitakaloliandika hapa kwamba, jibu nililolipata haraka haraka kuwa moja ya chagizo la matukio ya namna hii kutokea, halikuwa jingine bali ni kushindwa kuwajibika ipasavyo kwa viongozi wetu hususan wale tuliowapa dhamana ya kuongoza sekta kadhaa nyeti kama ya afya na ustawi wa jamii.

Ushahidi wa kupwaya huko kwa viongozi hususan wale walio chini yako, ndiko huko huko ambako kumedhihirika pia wiki iliyopita bungeni Dodoma, ambako tulishuhudia zahama nyingine iliyowang’oa madarakani mawaziri wako muhimu wanne kwa sababu kama hizo hizo za mkwamo wao au watendaji wa chini yao katika kusimamia ipasavyo na kuchukua hatua kwa wakati, kila yatokeapo matatizo yanayogusa maeneo wanayoyaongoza.

Nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu, mheshimiwa Rais iwapo nitaficha shauku ya moyo wangu ambayo ilikwenda sambamba na tukio lile la Dodoma lililowagusa baadhi ya mawaziri ambao anguko lao linaweza likaelezwa kuwa ni ‘ajali ya kisiasa’ nikitumia msamiati ulioutumia wewe mwenyewe kwa mara ya kwanza ulipozungumzia tukio la kujiuzulu kwa waziri wako mkuu wa kwanza, Edward Lowassa.

Haja ya moyo wangu, nikiwa mhariri, mwanahabari, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na mdadisi wa kawaida tu wa mambo, ilikuwa kuona anguko la namna hiyo hiyo likimfika Waziri wa Habari ambaye amethibitisha pasipo na shaka kuwa pamoja na kuwa msomi wa Shahada ya Falsafa (Phd), ni kiongozi asiyejua anachofanya kwa kiwango cha kuwa mtu ambaye vichwa vya watu wengine ndivyo vinavyofikiri kwa niaba yake.

Nilitamani afikwe na zahama hiyo si kwa sababu ya kuwa na hasira au kumchuria mabaya, bali kwa kuzingatia ukweli kwamba yeye ni mtu ambaye bado anasongwa na matongotongo ya mfumo wa kibabe wa zama za magazeti ya Serikali na yale ya chama tawala, ambayo yanalazimika kuandika yale tu yanayofurahisha nyoyo na akili za watawala.

Mheshimiwa Rais, ingawa natambua na kuheshimu ukweli mchungu kwamba, suala la nani awe waziri na nani asiwe ni jambo la wewe mwenyewe kupenda na kuchagua na kwamba ulishasema mapema kabisa mbele yetu kwamba urais wako hauna ubia, bado naamini pia kwamba, wewe ni mtu msikivu na mkweli uliye tayari kusikia na kustahimili mambo mengi machungu unayokabiliana nayo kila siku.

Kwa sababu hiyo, basi napenda kukueleza kwa kuweka kumbukumbu sahihi ili mbele ya safari kabla na baada ya kumaliza urais wako uje kuyatafakari na kuukumbuka ushauri huu kwako kwamba, waziri uliyempa dhamana ya kulea na kuendeleza vyombo vya habari, ni mtu wa kuhofiwa, jeuri, mwenye kiburi, asiyeshaurika na dikteta asiyekutakia mema wewe binafsi, vyombo vya habari, serikali yako na taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa rais sijui kama unajua kwamba tangu umteue amefanya kazi na vyombo vya habari vya umma na hata baada ya sisi kufanya juhudi kubwa ya kuwa karibu naye kikazi kwa makusudi na kwa ujeuri mkubwa, amekataa wito na kupuuza maoni na ushauri wetu na kwa namna ya kusikitisha amesikika akitamba waziwazi kwamba anao uwezo wa kulifungia au kulifutia usajili gazeti lolote ambalo ataliona linakwenda kinyume cha maadili ya uandishi wa habari.

Waziri huyu ambaye alitarajiwa kuwa na silika za kuwa mlezi bora kutokana na jinsia yake na historia yake ya kupata kuwa mwanaharakati kabla ya kuingia serikalini, ndiye ambaye mamlaka makubwa uliyomtwisha, ameyageuza na kuwa mwavuli wa kuvisulubisha vyombo vya habari vyenye uthubutu wa kukosoa serikali na kuandika ukweli mchungu ambao asingependa kuona ukiripotiwa.

Mheshimiwa Rais, pengine baya zaidi kwa tasnia hii ni kwamba waziri huyo ana bahati mbaya ya kuwa na mmoja wa wasaidizi na washauri wake katika sekta yetu ya habari ambaye naye, hulka zake tangu aingie katika tasnia ya habari amekuwa ni mtu wa kujipendekeza, kupenda makuu, kuzusha na kutokuwa na mawazo huru. Huyu si mwingine bali Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO).

Ni jambo la bahati mbaya kwamba waziri huyu msomi pengine kwa sababu ya kutojua vyema rekodi na historia ya msaidizi wake huyo, ambaye japokuwa naye pia ni mteule wako, amejikuta akiwa mhanga wa fikra pandikizi zinazopenyezwa wizarani chini ya uratibu mahususi unaofanywa na baadhi ya wateule wako ambao wameshaanza kujipanga kusaka urais baada ya wewe kustaafu.

Mheshimiwa Rais, nimelazimika kuyasema yote haya baada ya kula kiapo cha moyoni huku nikirejea mafunzo tuliyokuwa tukikaririshwa utotoni chini ya imani ya wana TANU, ambayo hata sisi ambao hatukuwa wanachama wa chama hicho tulilazimika kuikariri kwa kuitamka kila kukicha; ‘Nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko.’

Rais wangu, gazeti la MTANZANIA limerejea tena mitaani. Japokuwa ni rahisi kuhesabu miezi, napenda kukueleza kwamba, ilikuwa ni miezi mitatu michungu sana kwetu kihisia na katika hali halisi.

Nitakuwa mzushi sawa sawa na hao ninaowashangaa leo, iwapo nitasema kulikuwa hakuna hitilafu au makosa ya kiuandishi ambayo yaliwapa kisingizio cha mikakati waliyoipanga mapema kabisa, wasaidizi wako hao kwa kulifungia gazeti letu hili.

Mheshimiwa Rais, nasema haya kwa sababu ni ukweli ulio bayana kabisa kwamba, habari zilizoandikwa na kutoa mwanya kwa serikali yako kutuadhibu gazeti hili, hazikulenga kuchochea na wala hazikuchochea kabisa chuki yoyote dhidi ya yeyote na mamlaka unazoziongoza kwa namna na kwa njia yoyote ile.

Siyo siri hata kidogo, mkurugenzi aliyetangaza uamuzi huo alifanya hivyo akijua watu wengi hawajui mapito na dhamira yake. Tunajua yeye alimshauri vibaya waziri na serikali huku akijua vyema kwamba, yuko hapo alipo kwa maelekezo mahususi ya kundi la watu wenye malengo binafsi ambao mheshimiwa rais, niko tayari wakati wowote na mahali popote kukueleza kwa kina na kwa undani ili wakati utakapotaka kuchukua maamuzi ya haki na kweli ujue undani halisi wa mambo haya.

Leo hii wakati tukirejea tena sokoni, tayari tumeshasikia kuendelea kuwapo kwa mikakati ile ile ya kuhakikisha gazeti hili na jingine ambalo halipendwi na watu hao hao kwa sababu binafsi yakiinaingizwa tena mtegoni na kufungiwa kifungo kingine kama hiki tulichomaliza au kinachofanana na kile kilichoifika MwanaHalisi.

Mheshimiwa Rais, naandika waraka huu nikikumbuka semi zako mbili unazotumia; ‘tunajenga nyumba moja kwanini tugombee fito?’ na ile ya ‘akili za kuambiwa changanya na zako’ ambazo kwa muktadha wa waraka wangu huu kwako zinaweza zikawa za msaada sana kwako na pengine kwetu sisi wa MTANZANIA ambao tunashangilia kurejea mtaani kwa gazeti letu lililodhulumiwa fursa ya kuchapwa kwa muda wa siku 90.

Nimelazimika kukutumia wewe Rais si kwa lengo la kuchosha akili zako au kukupotezea muda, isipokuwa kwa kutambua hadhi, heshima na mamlaka makubwa uliyonayo juu ya wateule wako hao ambao wameamua kwa sababu ya jeuri za kimamlaka walizonazo kuumiza watu na kutupa sifa na majina mabaya tusiyostahili. Hakika wazungu walikuwa sahihi waliposema ‘power currupts’.

Mheshimiwa Rais, lingekuwa ni jambo la kheri kwa Serikali na kwa taifa letu zima iwapo kusudi la kufungia magazeti linalopangwa na wateule wako kuwa utamaduni wa kudumu, lingekuwa ni kujenga mustakabali mwema kwako wewe binafsi, chama chako, Serikali unayoiongoza na nchi yetu kuliko hili la sasa lenye dhamira ya kufunga watu midomo, kutesa, kuzusha na kuharibu taswira yetu kama watu binafsi, taasisi na taifa.

Ni kwa sababu hizo, mheshimiwa Rais ndiyo maana baada ya kusukwasukwa na moyo na kuumizwa mno kifikra nikaona nitakuwa sijaitendea haki nafsi yangu na haki za maelfu ya Watanzania ambao tunaamini wanahitaji huduma ya magazeti haya katika kukidhi mahitaji yao muhimu ya kimaisha, kielimu na kiufahamu kila kukicha na kuacha dhamira hizi za kishetani zikiendelea kuongoza sekta yetu.

Mheshimiwa Rais, siyo siri hata kidogo kwamba, ingawa mawazo hasi dhidi ya uhuru wa kikazi na kiwajibikaji wa vyombo vya habari na wanahabari yanaonekana kutawala kauli na maamuzi ya baadhi ya viongozi na washauri wako kwa kiwango cha kukushawishi hata wewe binafsi kukubaliana nayo, ukweli ni kwamba, nyuma ya maneno matamu wanayotumia kutupaka matope, kutujeruhi na kutupa kila aina ya sifa mbaya kuna ajenda za kutuharibia sisi, kukuharibia wewe, kukomoa, kuumiza na zaidi kulikwamisha taifa.

Nitakuwa mhariri nisiyewajibika, iwapo nitakaa kimya ilhali nikijua fika kwamba, leo hii ndani ya wizara iliyopewa dhamana ya kulea vyombo vya habari, baadhi ya wateule wako na watendaji wake wamekalia viti walivyonavyo si kwa sababu ya kuwa kwao na uwezo kustahimili ukosoaji, au upeo wao wa kuchochea maendeleo ya kitaaluma, bali kwa kuendeleza na kuyatumikia matakwa ya utarishi wa kifikra na kimatendo.

Kwa waraka huu mheshimiwa Rais, wakati tukikuahidi kwa dhati kabisa wewe binafsi na Watanzania wenzetu kwamba, tutaendelea na kazi kwa kuzingatia miiko na maadili ya uandishi wa habari, sambamba na kuheshimu sheria zilizopo, tunapenda kuliweka hili bayana kwamba, tutakuwa wa mwisho kuwatii viongozi dhalimu, madikteta, waliokosa utu na ambao kwao hila ndiyo msingi mama wa kupotosha na kupindisha mambo kwa sababu tu ya kulinda maslahi na malengo yao binafsi au yale ya makundi yenye hila.

Rais wangu, nimeona nitakuwa mtu nisiyekutakia mema wewe binafsi na taifa kwa ujumla, iwapo nitakaa kimya na kuruhusu fikra za kikaburu zikijijenga vichwani mwa viongozi wetu.

Mheshimiwa Rais, tutakuwa tumeshindwa kutimiza wajibu wetu kama wanahabari, wahariri na viongozi iwapo tutahalalisha kwa sababu ya ukimya wetu majina mabaya tunayoitwa leo na wateule wako kama wasaliti, wachochezi na wazushi.

Miye binafsi naamini kwa dhati kabisa kwamba iwapo wewe utaamua kwa moyo na nia njema kulinusuru taifa letu na majahili hao walio ndani ya Serikali yako, basi siku moja historia itakuja kuandika kwa usahihi na ufasaha jina lako na letu..

Mungu ibariki Tanzania.

SNURA AWASHUKURU MASHOSTI WAKE FACEBOOK


 
Snura Mushi.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao mmoja wa kijamii mwanadada Snura mushi alimua kufunguka yafuatao kwa mdada Wema Sepetu, Tundaman, Chekibudi na Marehemu Sharo Milionea kwa jinsi walivumsaidia kufika hapo alipo leo. Snura alisema yafuatayo…

Kwa Wema Sepetu
Msema kweli mpenzi wa mungu wakati narecod wimbo wangu wa kwanza wema alihusika sana...hela yake ilihusika studio, sauti yake ilihusika kwenye wimbo huo ambao ni shogaake mama ...vazi langu la show kwa mara ya kwanza wema ndio alinibunia namm nimeliandeleza vazi hilo mpaka leo kwenye show zangu sina chakukulipa wema ila nakushukuru sana nakuombea kwa mungu akubariki zaidi na zaidi wema sepetu...

Kwa Tundaman
Sijui nianzie wapi lakini huyu ndio mtu alie tumia nguvu kuniingiza kwenye muziki baada ya kuona kama siwaelewi hivi kila waliponiambia ....wakati anazindua album yake ya starehe gharama pale maisha aliamua kutengeneza tangazo ambalo lilisema snura atatambulisha wimbo wake mpya kwa mara ya kwanza kiukweli alinivuruga kwasababu mm sikua na wimbo wowote sasa kwa kuhofia aibu nishatangazwa ndio nikalazimika kwenda kurecod shogaake mama haraka sana na nikafanya hiyo show watu wakanielewa sana huo ndio ulikua mwanzo ....leo hii nimeona faida yake asante sana kakaangu tunda man mungu akubariki sana umekua mtu muhim sana kwenye maisha yangu tuendelee kushikana hivihivi kwa shida na raha nakupenda sana kakaangu tunda man captain ...msambinungwa..

Kwa Chekibudi
Ningependa kuanza na movie kabla ya muziki...japokua mwaka huu nimefanya vizuri sana katika muziki...basi kama kuna mtayarishaji wa movie anae tambua na kuthamini kipaji changu ni huyu ....nakushukuru sana kakaangu chekbud kwa kutambua umuhim wangu asante sana kaka ....nadhani kama ww nimshabiki wangu kwenye movie utakubaliana na hilo hakuna movie ya chekibudi mimi sipo...nakutakia kila lakheri brother. ....shukrani zinaendelea fuatilia ujue nani anafuata wako wengu kuna vitu vingi sana mtavijua ambavyo naamini hamjawahi kuvisikia mtavijua kupitia mtiririko huu wa shukrani.....

Kwa marehemu Sharo Milionea
Alinipigia kelele sana nifanye muziki yalikua yanaingilia huku na kutokea kule.....najua utakua una jiuliaza kwann nimemuweka wakati alishafariki toka mwaka jana na shukrani nnazozitoa ni za mwaka huu...nimefanya hivi kwasababu ktk miaka yote mwaka huu ndio umekua wa mafanikio sana kwangu na sababu ni mziki ambao huyu ndio mtu aliekua akinipigia kelele sana nifanye sijui kwann sikumsikilizaga natamani angekuepo aone kile alichokua anakitamani aone watanzania na nje ya tanzania walivyonipokea vizuri...R.i.p brother

MISS TANZANIA 2013 AWAFARIJI WATOTO YATIMA

 

Redds Miss Tanzania 2013 Happiness Watimanywa ( kushoto) akipinga hodi ikiwa ni ishara ya kukaribishwa katika Kituo cha kuleta watoto yatima Mgolole cha Masista wa Moyo Safi wa Maria wa Morogoro , ambapo alifuatana na warembo wengine wawili, Miss Tanzania mshindi wa tano, Elizabeth Perrty, na Sabra Islam Miss Morogoro 2013, wazazi wake na Viongozi wa juu wa Kamati ya Miss Tanzania na kupokelewa na Mama Mkuu wa Kituo hicho, Sista Flora Maria Chuma ( mwenye kutabasamu ) Desemba 25, mwaka huu walipotembelea kwa ajili ya kutoa zawadi ya vyakula vya aina mbalimbali ikiwa ni mpango wake wa kusaidia makundi ya aina hiyo.

Redds Miss Tanzania 2013 Happiness Watimanywa ( kulia) akimkabidhi kopo la maziwa Mama Mkuu wa Kituo cha kuleta watoto yatima Mgolole cha Masista wa Moyo Safi wa Maria wa Morogoro ,Sista Flora Maria Chuma ( kushoto) Desemba 25, mwaka huu walipotembelea kutoa zawadi ya vyakula vya aina mbalimbali kwa Kituo hicho ikiwa ni mpango wa kusaidia makundi ya aina hiyo akiambatana na warembo wengine wawili, Miss Tanzania mshindi wa tano, Elizabeth Perty, na Sabra Islam Miss Morogoro 2013, wazazi wake na Viongozi wa juu wa Kamati ya Miss Tanzania.

Redds Miss Tanzania 2013 Happiness Watimanywa ( kushoto) akiwa amempataka mikononi mtoto yatima Happiness, akiwa na warembo wengine wawili, Miss Tanzania mshindi wa tano, Elizabeth Perrty, ( kulia) na mwezake Sabra Islam Miss Morogoro 2013, na Viongozi wa juu wa Kamati ya Miss Tanzania, akiwemo Mkurugenzi Hashim Lundega, wakisikiliza maelezo ya Mama Mkuu wa wa Kituo cha kuleta watoto yatima Mgolole cha Masista wa Moyo Safi wa Maria wa Morogoro ,Sista Flora Maria Chuma ( hayupo pichani ) ,Desemba 25, mwaka huu walipotembelea na kutoa zawadi ya vyakula vya aina mbalimbali kwa Kituo hicho siku ya sikukuu ya Christimas ikiwa ni mpango wake wa kusaidia makundi ya aina hiyo.

Redds Miss Tanzania 2013 Happiness Watimanywa ( kushoto) akiwa amempataka mikononi mtoto yatima Happiness, alipoteembelea Kituo cha kuleta watoto yatima Mgolole cha Masista wa Moyo Safi wa Maria wa Morogoro , Desemba 25, mwaka huu walipotembelea na kutoa zawadi ya vyakula vya aina mbalimbali kwa Kituo hicho siku ya sikukuu ya Christimas ikiwa ni mpango wake wa kusaidia makundi ya aina hiyo, pia alifuatana na warembo wengine wawili, Miss Tanzania mshindi wa tano, Elizabeth Perrty, na Sabra Islam Miss Morogoro 2013, wazazi wake na Viongozi wa juu wa Kamati ya Miss Tanzania .

Redds Miss Tanzania 2013 Happiness Watimanywa ( kushoto) akiwa na warembo wengine wawili, Miss Tanzania mshindi wa tano, Elizabeth Perty, na Sabra Islam Miss Morogoro 2013, wazazi wake na Viongozi wa juu wa Kamati ya Miss Tanzania, wakisikiliza maelezo kutoka kwa Mama Mkuu wa wa Kituo cha kuleta watoto yatima Mgolole cha Masista wa Moyo Safi wa Maria wa Morogoro ,Sista Flora Maria Chuma ( kulia) Desemba 25, mwaka huu , walipotembelea na kutoa zawadi ya vyakula vya aina mbalimbali kwa Kituo hicho ikiwa ni mpango wake wa kusaidia makundi ya aina hiyo.

Redds Miss Tanzania 2013 Happiness Watimanywa akisaini kitabu cha wageni.
Redds Miss Tanzania 2013 Happiness Watimanywa akigawa zawadi za vyakula vya aina mbalimbali kwa baadhi ya watoto yatima wanaolelewa na Kituo cha Mgolole cha Masista wa Moyo Safi wa Maria wa Morogoro , Desemba 25, mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kusaidia watoto wa aina hiyo , akiwa ameambatana na warembo wengine wawili, Miss Tanzania mshindi wa tano, Elizabeth Perty, na Sabra Islam Miss Morogoro 2013, wazazi wake pamoja na Kamati ya Miss Tanzania.Picha na John Nditi

NDOA YA WEMA,DIAMOND HII HAPA,PENNY APIGWA CHINI JUKWAANI KWEUPEHUKU mchumba’ke, Penniel Mungilwa ‘Penny’ akifungasha virago kurejea kwao, mzee mzima Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ametangaza kumuoa Miss Tanzania 2006, Wema Isaac Sepetu ‘Madam’.
 
Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’(kushoto) na Penniel Mungilwa ‘Penny’ wakiongea jambo enzi za mapenzi yao.

Ishu hiyo ilijiri ndani ya Viwanja vya Leaders Club, Kinondoni jijini Dar ambapo mkali huyo wa Bongo Fleva alikuwa akikamua kwenye sherehe ya Krismasi aliyoiandaa mwenyewe.
Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ na Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ baada ya kupanda jukwaani katika viwanja vya leaders.

TANGAZO LA AWALI
Awali kabla ya kufikia eneo la kutangaza kuoana, Diamond aliweka wazi jukwaani kwamba yeye na Wema wamerudiana.
Diamond Platnumz akiongea jambo baada ya Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ kupanda jukwaani.

MTIRIRIKO ULIVYOKUWA
Diamond, akiwa ameshika kipaza sauti alikatisha kuimba na kuwauliza mashabiki wake, hasa watoto waliohudhuria kwa wingi tamasha hilo, je, wanataka kumuona shemeji yao?
“Itakuwa si vizuri mkaondoka bila kumuona shemeji yenu, nikuleteeni mumuone?” aliuliza Diamond. Swali hilohilo akalirudia tena ambapo lilipokelewa kwa shangwe huku mashabiki wakilitaja jina la Wema.
Diamond Platnumz na Wema Isaac Sepetu wakijiachia.

WEMA APANDISHWA JUKWAANI

Kufuatia kelele za mashabiki, Diamond alimuomba Disco Joker (DJ) wake amuwekee Wimbo wa Ukimwona ambao ulisindikiza ujio wa Wema jukwaani akifuatana na wapambe wa Diamond.
“DJ acha huo, nipigie Wimbo wa Ukimwona watu wangu wa nguvu wamwone shemeji yao kwani tangu nilivyokwenda naye China walikuwa wakisumbuliwa na maneno tofautitofauti kutoka kwenye mitandao ya kijamii,” alisikika Diamond.
 
Diamond, akiwa ameshika kipaza sauti akiima Wimbo wa Ukimwona na Wema akiwa amemkumatia.

JUKWAA SASA
Hali haikuwa ya kawaida jukwaani kwani kilichofuata hapo ni Wema kuonesha kwa vitendo mambo yaliyoashiria kuwa, wawili hao sasa ni mwendo mdundo.
Wema alishuhudiwa akimzungushia mikono Diamond kwenye kiuno jambo ambalo liliwafanya baadhi ya mashabiki wa mastaa hao kutoa machozi ya furaha kuona penzi la wawili hao limerudi upya, wengine walimwambia Diamond amuoe Wema.
“Diamond muoe Wema, mnapendezana sana,” walisikika mashabiki.

Wema Isaac Sepetu ‘Madam’akimuaga Diamond Platnumz kwa kumkumatia.
MAWIFI WADAI KUHARIBIWA SIKU NA KAKA YAO
Hata hivyo, kitendo cha Diamond kumwita Wema jukwaani kilionekana kuharibu furaha ya sikukuu kwa ndugu zake kwani bila ya kuuma midomo dada zake staa huyo wakiongozwa na Esma Khan walinuna na kuanza kuondoka.
“Yaani siku yangu imeshaharibika, nilikuja nina furaha sasa imepotea, tuondokeni ndugu zanguni,” alisema Esma akiwaambia Mwanaisha Abdul ‘Queen Darleen’ na Halima Haroun ‘Kimwana’.

Diamond Platnumz na Penny wakiwa pamoja enzi za mapenzi yao.
MAMA DIAMOND ASHANGAA
Kitendo cha ndugu hao kukasirika hakikupokelewa vizuri na bi mkubwa wao yaani mama Diamond, Sanura Kassim ‘Sandra’ ambaye aliwajia juu akiwashangaa.
“Wajinga nini? Sasa walitaka Diamond… (tusi) wao, mtu ameshaamua kupenda wamwache, mi’ mwenyewe nimeshajifunza, sitaki kuingilia penzi lake,” alisema mwanamke huyo ambaye mjini anazungukia usafiri aina ya Altezza.


Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Penniel Mungilwa ‘Penny’.

Baada ya shoo hiyo iliyomalizika saa moja usiku, paparazi wetu alimfuata Diamond akiwa amesimama na Wema na kuwauliza kama kweli wana nia ya kufunga ndoa.
“Hilo mwana mbona lipo wazi, nataka kumuoa staa na nataka kuzaa na staa,” alisema Diamond huku Wema akiwa hapingi.MAMA WEMA ATANGAZA VITA NA DIAMOND
Wakati Dimaond akitambia ndoa na Wema, siku hiyohiyo ya Krismasi, mama wa Wema, Mariam Sepetu alidaiwa kutangaza vita na mwanamuziki huyo baada ya kusikia tetesi kuwa amerudiana na mwanaye.
Kwa mujibu wa rafiki wa karibu wa mama Wema (jina tunalo) mama wa staa huyo alichukizwa na kitendo cha Diamond kurudiana na mwanaye kwani anaamini anamchezea tu.

Mama wa Wema, Mariam Sepetu.

Rafiki huyo alizidi kudai kuwa, taarifa hizo zimemuweka mama huyo kwenye wakati mgumu na kudai kuwa popote atakapokutana na mwanamziki huyo atampopoa mawe au machungwa hata ikiwa siku ya ndoa yao.
“Mama Wema amesema hampendi Diamond, popote atakapomuona itakuwa vita ya wawili, kama kuna jiwe atamrushia, hata machungwa kama yapo yatakuwa halali yake,” alisema rafiki huyo.

WOSIA WA MZEE SEPETU
Mpashaji huyo wetu alizidi kufunguka kuwa, mama Wema ana wosia mkononi ambao aliuacha marehemu mumewe, mzee Isaac Abraham Sepetu.
Alisema katika wosia huo, mzee huyo alisema hataki Diamond amuoe Wema na kama mrembo huyo atakiuka wosia huo atapatwa na laana mbaya katika maisha yake.
“Kinachomuumiza zaidi mama Wema ni huo wosia, mzee Sepetu alisema hataki mtoto wake aolewe na Diamond, kama atakataa kuna kitu kibaya kitamkuta katika maisha yake,” alisema rafiki huyo.

MAMA WEMA ASAKWA
Baada ya kupata habari hizo, gazeti hili lilimvutia waya mama Wema ili kuweza kuthibitisha madai hayo ambapo alisema kuwa, hayuko tayari kuzungumzia jambo hilo kwa wakati huo mpaka atapoamua akisisitiza muda si mrefu.
“Jamani nina mambo mengi sana ya kufanya na sijatulia kabisa siko tayari kuzungumza chochote kwa sasa nikiwa tayari nitawaambia kila kitu,” alisema mama Wema.Friday, December 27, 2013

TAMASHA LA KRISMAS LILIVYOBAMBA MJINI MOROGORO LEOMmoja ya Waimbaji machachari katika anga ya muziki kiroho a.k.a Injili,Bone Mwaitege akionesha umahiri wake wa kucheza,na madansa wake kwenye uwanja wa Jamuhuri,mkoani Morogoro mapema leo ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa tamasha la Krismasi,ambapo hapo jana limezinduliwa rasmi jijini Dar katika uwanja wa Taifa na kuhudhuriwa na watu kibao.

Mwimbaji wa nyimbo za kusifu na kuabudu,Upendo Kilahiro akiwaimbisha sehemu ya wakazi wa mji wa Morogoro waliojitokeza kwenye muendelezo wa tamasha la krisimasi lililofanyika jioni ya leo ndani ya uwanja
wa jamuhuri mkoani Morogoro.

Madansa wa mwimbaji nyota wa muziki wa Injili hapa nchini,Rose Muhando wakiwajibika vilivyo.
Malikia wa nyimbo za Injili,Rose Muhando akiimba kwa hisia wimbo wake mpya uitwao FACEBOOK,ndani ya uwanja wa jamuhuri,mkoani Morogoro mapema leo jioni.

Sehemu ya mashabiki wakishangilia.
Mwimbaji wa injili kutoka nchini Zambia,Eprahim Sekereti akiimba sambamba na kundi la Victoria singers,ndani ya uwanja wa Jamuhuri mkoani Morogoro jioni ya leo ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa tamasha la Krisimasi.

Mwimbaji wa nyimbo za injili,Upendo Nkone akiwaimbisha mashabiki wake (hawapo pichani) waliofika kulishuhudia tamasha hilo la mwendelezo wa krisimasi mpaka mwaka mpya.

Mmoja wa waimbaji wa nyimbo za kiroho kutoka mkoani Morogoro,Tumaini Njole akiimba huku akiwa katika staili ya kipekee kabisa,huku mayowe na shangwe zikisikika kutoka kwa mashabiki


Sehemu ya mashabiki

Vijana wa kundi la The Voice wakiwaimbisha mashabiki na watazamaji waliofika kwenye tamasha hilo ndani ya uwanja Jamuhuri mkoani Morogoro.

JACK PATRICK ADAIWA KUNASWA NA DAWA ZA KULEVYA CHINAJackie akiwa kwenye picha na rafiki yake Cheif Rocka aliye thibithisha habari za kukamtwa kwake huko China. Amesema huyu ni Jackie na hakuna ubishi ubalozi pia umethibithisha habari hizo. Sikiliza kwa makini Sauti hiyo hapo chini.

WANASOKA WALIVYOJITOKEZA KUUAGA MWILI WA KOCHA WA MAKIPA SIMBA SC

 
Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Kocha wa makipa wa Simba, marehemu James Kisaka likiingizwa kwenye basi la klabu hiyo, baada ya kutolewa heshima za mwisho katika misa iliyofanyika katika Kanisa la Muhimbili, Dar es Salaam. Marehemu Kisaka atasafirishwa kwenda kwao wilayani Muheza, Tanga kwa mazishi yatakayofanyika leo.
Aliyekuwa Kocha Msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelo 'Julio', (kushoto) akijadiliana jambo na baadhi ya wachezaji wa soka waliokwenda kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu James Kisaka.
 
Mjane wa marehemu James Kisaka, Teddy Kisaka akifarijiana na mtoto wa pili wa marehemu Kisaka, Boniface baada ya kutoa heshima za mwisho.
Ndugu wa karibu wa marehemu Kisaka akilia alipokuwa akitoa heshima za mwisho

Wednesday, December 25, 2013

AIRTEL YAWATAKIA WATANZANIA HERI SIKUKUU YA KRISMASI


-Airtel yawatakia Watanzania heri ya sikukuu
-Yazidi kutanua kifua kwamba ni Baba lao
Kampuni ya mitandao ya simu za mkononi ya Airtel imewaasa Watanzania wote kote nchini kulinda amani na utulivu wa nchi katika kipindi hiki cha sikukuu ikiwa ni baada ya kuwatakia heri ya Christmas na mwaka mpya.

Akizungumza kwenye ofisi za makao makuu ya Airtel, Meneja Uhusiano wa Airtel Tanzania, Jackson Mmbando alisema sikukuu za Christmas na mwaka mpya ni sikukuu muhimu sana kwa wananchi wa taifa hili hivyo zinapaswa kusherehekewa kwa amani na utulivu.

“Ninawaomba wateja wa Airtel na watanzania wote kwa ujumla kutambua umuhimu wa sikukuu hizi na kuepuka kufanya matukio ambayo yanaweza kuhatarisha amani na utulivu wa taifa,” alisema Mmbando.

Aidha alisema katika msimu huu wa sikukuu bado Airtel inazidi kudhihirisha kuwa ni baba lao kwa wateja wake kwa kutoa huduma zilizo za gharama nafuu zinazowawezesha kutuma na kupokea pesa bure pia kutumia huduma mbalimbali za inataneti na kupiga kwenda mitandao yote.

“Airtel bado ni baba lao kupitia huduma zetu mbalimbali, Wateja wetu bado wanaweza kunufaika na huduma zetu ambapo kwa sasa wateja wanaweza kupata vifurushi vya inataneti kwa gharama nafuu, kupiga simu kwenda mitandao yote na pia kutuma na kupokea pesa bure,” alisema Mmbando.

Ikumbukwe kuwa vifurishi vyote vya siku vya Yatosha vinadumu kwa masaa 25 tangu mteja anapojiunga ikiwa na lengo maalumu la kumfanya mteja aweze kufurahia huduma hiyo na kuwafaidisha watanzania waendelee kuokoa pesa nyingti walizokuwa wakizitumia kwenye mawasiliano na kuanza kuzitumia katika shughuli nyingine za uchumi wa taifa na jamii kwa ujumla.

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...