Wapendanao, Jokate Mwegelo ‘Kidoti’ na Ali Kiba ‘King Kiba’ wakiwa katika pozi.
Na mwandishi wetu, Risasi Jumamosi
DAR ES SALAAM: Wapendanao, Jokate Mwegelo ‘Kidoti’ na Ali Kiba ‘King Kiba’, wamedaiwa kuzichapa kavukavu ndani ya gari kisa kikiwa ni ujumbe mfupi wa maneno (SMS), Risasi Jumamosi lina ubuyu kamili.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, ishu hiyo ilitokea katikati ya wiki iliyopita maeneo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam bila kujulikana walikuwa wakitokea wapi kwenda wapi.
Jokate Mwegelo ‘Kidoti’.
Jokate na Kiba awali walimwagana lakini hivi karibuni wakarudiana baada ya familia ya Kiba, akiwemo mama yake, kuwakutanisha Februari 5, mwaka huu kwenye Hoteli ya Slipway, Masaki jijini Dar na kumaliza tofauti zao.
Siku hiyo ya kupatanishwa kulikuwa na hafla ya uzinduzi wa video ya Kiba iitwayo Lupela ambayo inafanya vizuri katika soko la muziki wa Bongo Fleva nchini.
TUJIUNGE NA CHANZO
Kwa mujibu wa chanzo makini, Jokate na Kiba walipishana kauli baada ya mrembo huyo anayefanya vyema katika tasnia ya muziki, filamu na mitindo Bongo kulazimisha kusoma ujumbe mfupi wa maneno ulioingia kwenye simu ya mpenzi wake huyo.
Ali Kiba ‘King Kiba’.
SIKU YA TUKIO
Chanzo hicho kiliweka bayana kuwa wawili hao wakiwa katika mizunguko yao hivi karibuni, walisimamisha gari lao maeneo ya Kinondoni-Biafra na ndipo walipoanza kuzozana kwa muda kabla ya kuanza kushikana maungoni.
“Walitaitiana kwenye gari. Wakapaki, Kiba alionekana kushuka kama anataka kumuacha Jokate peke yake ndani ya gari, Jokate hakukubali, akashuka na yeye kumlazimisha arudi. Mazungumzo yalisikika Jokate akihoji ni kwa nini jamaa anamkatalia kusoma meseji iliyoingia kwenye simu yake! Ndipo timbwili liliponoga.
“Ilikuwa mtiti wa aina yake lakini Kiba alipoona ‘nzi’ (mashuhuda) wanaanza kujaa, akaona isiwe tabu, akarudi ndani ya gari na Jokate naye akaingia wakaondoka zao,” kilisema chanzo hicho kilichoshuhudia timbwili zima.
MENEJA AFUNGUKA
Kabla ya kuwatafuta wawili hao, mwanahabari wetu alimtafuta mmoja kati ya mameneja wa Kiba aliyeomba hifadhi ya jina ambaye aliweka wazi kuwa, wawili hao walipishana ‘Kiswahili’ kutokana na SMS ambayo haikuwa mbaya isipokuwa walishindwa kudhibiti hasira zao.
Msikie: “Walipishana lugha baada ya Jokate kulazimisha kusoma au kuona ujumbe ulioingia kwenye simu ya Kiba. Halafu kwani unafikiri basi ulikuwa ujumbe mbaya, ilikuwa ni meseji yangu niliyomtumia kumpa maelekezo ya kazi lakini Jokate akamaindi.
“Alichokosea Kiba ni kukataa kumpa simu sasa sijui naye ana vimeo vyake au vipi lakini hapo ndipo utata ulipoanzia. Wakavutana kwa muda lakini bahati nzuri Kiba akawa mstaarabu, akarudi ndani ya gari kama Jokate alivyomtaka, wakamalizana na kuendelea na safari yao,” alisema meneja huyo.
PENZI LIPO PALEPALE
Akaongeza: “Kwa sasa wapo freshi. Si unajua mambo kama hayo kwenye mapenzi yanatokea. Wamewekana sawa na kila kitu kipo kwenye mstari. Wamewekeana mikakati mizuri kuhusu matumizi ya simu.”
KIBA ANASEMAJE?
Baada ya kuzungumza na meneja huyo, mwanahabari wetu alimtafuta King Kiba kupitia kilongalonga chake cha mkononi ambapo alipopatikana alitoa majibu tata ambayo gazeti lilishindwa kubaini kama amekubali au amekataa.
Msikilize: “Kwa nini kila siku mnaniuliza habari za skendo tu? Mbona hamniulizi kuhusu muziki wangu unavyofanya vizuri kitaa au hujasikia ngoma yangu ya Lupela inavyokamata chati? Acha mambo yako bwana.”
Akaongeza: “Halafu, hata kama ni kweli wewe tatizo lako ni nini? Mengine ni mambo binafsi. Haipendezi kila ninachofanya au kinachonitokea nikitangaze kwenye vyombo vya habari. Mimi nafikiri uwe unaniuliza zaidi kuhusu kazi yangu ambayo mashabiki ndiyo wanataka kuijua.” (akakata simu).
JOKATE HAPOKEI SIMU
Jitahada za kumpata Jokate ili aweze kuzungumzia sakata hilo ziligonga mwamba baada ya mrembo huyo kutopokea simu na hata alipotumiwa ujumbe mfupi, hakujibu chochote.
Jokate na Kiba kwa sasa ni ‘kapo hot’ ambayo mashabiki wengi wanawaombea wafikie hatua ya kuoana licha ya kuwa na mvutano kutoka kwa wazazi wa Jokate ambao waliwahi kuripotiwa kutoafiki uhusiano huo.
No comments:
Post a Comment