Gladness Mallya/ijumaawikienda
Inasikitisha
sana! Huku akitundikiwa dripu nyumbani kwao, Sinza ya Vatican jijini
Dar, daktari ameanika ugonjwa unaomtesa staa wa muziki wa Dansi Bongo,
Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’ kuwa vipimo vinaonesha anashambuliwa na
fangasi kichwani (ubongo) na shingoni.
YU HOI TENA
Habari zinaeleza kuwa tatizo hilo
limesababisha Banza kuwa hoi kwa mara nyingine akiumwa na kichwa kupita
kiasi hivyo kushindwa kufanya lolote.Kufuatia maumivu anayoyapata, Banza
amewaomba Watanzani wamuombee kwani anaamini katika maombi yao.
MAOMBI MUHIMU
Akizungumza kwa tabu na Ijumaa
Wikienda, Banza ambaye kwa sasa hawezi kunyanyuka kwenye kochi alisema
anatamani angepona ili arudi jukwaani hivyo maombi yao ni muhimu kuliko
kitu chochote na ni msaada tosha kwake.
“Kikubwa nawaomba Watanzania waniombee kwani hali niliyonayo siyo ya
kawaida, nasikia maumivu makali sana ya kichwa na shingo hadi nashindwa
kula.“Hata kuongea ndiyo hivi kwa shida na muda mwingi naweka kitambaa
cha maji ya baridi kwenye paji la uso ili kupunguza makali ya maumivu,”
alisema Banza kwa masikitiko makubwa.
Banza kwa sasa anatibiwa nyumbani kwao baada ya kupata matibabu
kwenye Hospitali ya Sinza-Palestina ambapo anaongezewa maji (dripu) na
kuendelea kumeza dawa za ugonjwa huo.
DAKTARI ATHIBITISHA
Banza alisema ugonjwa huo amethibitishiwa na daktari wake kwenye hospitali hiyo baada ya kuchukuliwa vipimo.
FANGASI KICHWANI AU KWENYE UBONGO IKOJE?
Kwa mujibu wa mtaalam wa magonjwa ya kichwa, kitaalam ugonjwa huo huitwa Mucormycosis.
Ni ugonjwa ambao katika siku za hivi karibuni umekuwa maarufu huku
ukisababisha vifo vya watu wengi. Kitaalam, ugonjwa huu husababishwa na
fangasi waitwao Murcorales ambao huingia ndani ya mwili wa binadamu kwa
njia ya hewa.
Ukivuta hewa yenye fangasi hao, huingia na kwenda moja kwa moja
kwenye mfumo wa damu kisha kuanza kuzunguka ndani ya mwili kufuata damu.
Baada ya kukaa kwa wiki kadhaa kwenye mfumo wa damu, huhamia kwenye uti
wa mgongo (spinal) ambapo huzaliana kwa wingi na kuanza kusambaa
kuelekea kwenye ubongo.
Fangasi hawa wanapofika kwenye ubongo, huushambulia na kusambaa kwa
kasi ambapo uwezekano wa mgonjwa kupona huwa mdogo. Kati ya kila watu
100 wenye ugonjwa huo, karibu 30 hupoteza maisha.
DALILI ZA UGONJWA
Dalili za awali za ugonjwa huo ni kuwa na uvimbe mwekundu unaotokea
kuzunguka macho ambao huongezeka kadiri fangasi wanavyozidi kushambulia
ubongo.
Dalili nyingine ni pamoja na kuumwa kichwa upande mmoja, uso kuuma,
homa kali, kupumua kwa shida na kutokwa kamasi za rangi nyeusi.Pia ngozi
ya mwili wa mgonjwa huanza kubadilika rangi na kuwa nyekundu. Hali hiyo
huendelea hadi ngozi inapobadilika zaidi na kuwa nyeusi.
TIBA
Vipimo vya ugonjwa huo hufanywa kwa mashine
ya MRI ambapo mtu akibainika ameambukizwa fangasi hao, hutibiwa kwa
upasuaji wa ubongo na kuondoa sehemu zilizoathirika pamoja na kutumia
dawa kali za Amphotericin B au Posaconazole, wakati mwingine dawa hizi
huchanganywa pamoja.
WATU WALIOPO KWENYE HATARI
Watu wanaoweza
kuupata ugonjwa huu kwa urahisi ni wagonjwa wa kisukari, HIV,
waliofanyiwa upasuaji wa kupandikiza viungo ndani ya miili yao kama figo
au ini, na matumizi ya dawa za ‘corticosteroids’ kwa kipindi kirefu.
No comments:
Post a Comment