Saturday, February 21, 2015

TAARIFA KAMILI JUU YA MAZISHI YA MEZ B INGIA HAPA...


ALIYEKUWA memba wa kundi la Chamber Squad, Moses Bushagama ‘Mez B’ ambaye amefariki jana mjini Dodoma anatarajiwa kuzikwa Jumatatu katika makaburi ya Wahanga yaliopo Maili Mbili mjini Hapo. Mtandao huu uliongea na mama wa marehemu, Marry Mkandawile ambaye alisema kuwa kwa sasa msiba upo maeneo ya Kisasa mjini hapo. KWA HISTORIA ZAIDI YA MAREHEMU MEZ B INGIA HAPA.....

MSANII wa muziki wa Bongo Fleva aliyekuwa akiwika na kundi la Chamber Squad, Moses Bushagama ‘Mez B’ amefariki dunia asubuhi ya leo majira ya saa 4:30 mjini Dodoma.
Mez B akiwa katika moja ya mahojiano yake na kituo cha TV.

Hii imekuwa ni pigo la pili kwa kundi la Chamber Squad kupoteza memba wake baada ya awali kumpoteza Albert Mangweha ‘Ngwear’.Katika makala haya yanauelezea undani wa Mez B mpaka kufikia umauti.

MEZ B NI NANI?
Mez B amekulia mjini Dodoma maeneo ya Area C. Akiwa anasoma katika Shule ya Sekondari ya Mazengo, Dodoma ndipo alipokutana na wenzake Noorah, Ngwear pamoja na Dark Master.
Kwa mara ya kwanza walipokutana shuleni hapo, walianzisha kundi la CFG yaani Chemba Fleva Guys lililokuwa likiundwa na Ngwear, Mez B pamoja na Nzeku.

Walipomaliza shule, wakaamua waendeleze kundi na kubadilisha jina na kujiita Chamber Squad.
Awali Chamber Squad ilianzishwa na Tino Mkale, Mgulu George na wengine kibao ambao hawakuwa na majina kabla ya kuliacha kundi hilo likimilikiwa na Ngwear, Noorah, Mez B na Dark Master.
Rehema Chalamila (picha ya chini) ambaye ni mmoja ya mastaa waliowahi kushirikisha na Mez B katika Wimbo wa Basi Kama Vipi.
AANZA KUNG’ARA
Mez B alianza kutambulika kama mwanamuziki wa R&B ambapo alitoka na Wimbo wa Fikiria na baadaye akawika na nyimbo kama Furaha Tele, Mama na Mwana, Nichukue pamoja na Mpenzi njoo aliyokuwa amemshirikisha Afande Sele.

Nyimbo nyingine zilizompa umaarufu ni pamoja na Kidela, Nimekubali, Shemeji, Basi Kama Vipi akiwa ameshirikiana na Ray C na Noorah.
Miongoni mwa wimbo uliopandisha kundi la Chamber Squad ni pamoja na Home Sweet Home ambao Mez B aliutendea haki kwa upande wa kiitikio.
NGWEAR AFARIKI, MMOJA APUNGUA
Mei 28, 2013 Kundi la Chamber Squad lilipata pigo kwa kuondokea na memba wao, Albert Mangweha ‘Ngwear’ ambaye alifariki akiwa nchini Afrika Kusini alikokwenda kufanya shoo kwenye miji mbalimbali nchini humo ikiwemo Johannesburg na Cape Town.Alizikwa mkoani Morogoro, Juni 6, 2013 katika makaburi ya Kihonda.
Baada ya hapo kundi la Chamber Squad lilibakiwa na vichwa vitatu ambavyo ni Noorah, Mez B pamoja na Dark Master.
Memba mwenzao, Dark Master alishawahi kusema kuwa kundi hilo bado lipo na walikuwa njiani kuja na nyimbo mfululizo. Mez B akiwa na majeraha baada ya kujerehuliwa na mtu asiyejulikana.
ASHAMBULIWA, ATAKA KUULIWA
Zikiwa zimepita wiki chache tangu Mez B ampoteze memba mwenzake, Ngwear alipata balaa la kushambuliwa na mtu asiyemfahamu akiwa sehemu ya burudani maeneo ya Sinza, jijini Dar.
Usiku huo Mez B alikuwa ameenda kutafuta chakula (Chips) na kushuhudia mtu mmoja akiamuliwa na mabaunsa achomwe visu.
Tukio hilo lilianzia pale Mez B alipofika eneo hilo ambalo alishangaa mtu mmoja akiitusi serikali pamoja na Mez B mwenyewe hali iliyozua tafrani.Kitendo cha Mez B kuondoka, baunsa mmoja alimfuata mtu aliyekuwa akitukana na kumuamuru amchome visu Mez B. Ujasiri ulimsaidia Mez B kwani alikuwa achomwe shindoni lakini alikwepa na kuchoma baadhi ya maeneo ya usoni.
Suala hilo alilipeleka mbele ya vyombo vya sheria ambapo bado kesi ilikuwa ikiendelea.
Picha aliyopiga Mez B na wasichana wawili katika Fukwe za Mikadi, jijini Dar.
AFUMWA AKIJIACHIA NA WASICHANA UFUKWENI
Septemba mwaka jana, Mez B alilingia katika msala wa kukutwa katika Fukwe za Mikadi, jijini Dar akiwa na wasichana ambao walionekana wakiwa watupu.
Moja ya magazeti pendwa, yalichapisha habari hiyo ambayo picha zilimuonyesha Mez B akiwakumbatia huku wasichana hao wakionekana watupu kama walivyozaliwa.
Wasichana hao waliotambulika kama Vicky na Rebecca walikuja kubainika kuwa siyo raia wa Tanzania na kudaiwa kuwa Mez B alikuwa akitengeneza video ya wimbo mpya na wasichana hao waliomba kupiga picha naye tu baada ya kumuona.
AANZA KUUGUA
Februari mwaka huu, Mez B alianza kuugua na kulazwa katika hospitali moja mkoani Dodoma akiwa anasumbuliwa na maumivu ya kichwa na shingo hali iliyomfanya awe chini ya uangalizi wa madaktari.
Kauli yake ya mwisho baada ya kuugua ilikuwa ni kuomba msamaha kwa mashabiki kwa kuchelewa kuanza ‘projekti’ mpya kutokana na hali iliyokuwa ikimkabili.
“Bado nasumbuliwa na Pneunomia tangu mwezi wa 12 mwaka jana lakini kwa sasa naendelea vizuri na matibabu na nategemea kuruhusiwa muda wowote. Nikitoka nitaendelea na projekti yangu,” alisema Mez B. AFARIKI DUNIA
Mez B amefariki dunia saa 4:30 asubuhi katika Hospitali ya Mwananchi mjini Dodoma ambapo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa Homa ya Mapafu ambao kitaalamu unajulikana kama Pneunomia.
Taratibu juu ya mazishi bado hazijafanyika na tutaendelea kukujuza zaidi.
Uongozi na wafanyakazi wa Global Publishers unatoa pole kwa ndugu na wana familia wa Mez B kwa msiba uliotokea.Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...