Friday, February 13, 2015

PRE-VIEW LIGI KUU BARA LEO


Hatariii..... Leo Wagosi wa Ndiba, Coastal Union watakipiga na Wabishi wa Jiji, Mbeya City kwenye Uwanja wa Mkwakwani

Achana na mechi za kimataifa, zinazowahusu, Yanga na Azam wikiendi hii, nayo Ligi Kuu Bara, itaendelea kutimua vumbi katika viwanja mbalimbali leo na kesho, nyingi zake zikiwa ni za visasi kutokana na kumbukumbu mbovu kwenye mechi za mzunguko wa kwanza.
Ndanda vs Mtibwa
Ni mechi yenye tafakuri nyingi. Kwanza, Mtibwa ambao ni vinara wa zamani wa ligi wataingia uwanjani na hasira za kupoteza mechi mbili mfululizo-dhidi ya Yanga na Azam ndani ya kipindi cha wiki moja. Ilikuwa wiki nzito wa Wakata Miwa hao wa Manungu, Turiani ambapo wameweka rekodi ya kuruhusu mabao saba ndani ya wiki moja.
Yote kwa yote, benchi la ufundi la kikosi hicho chini ya Mecky Maxime amekiri na kuomba mzigo wa mabao hayo aubebe yeye na si mchezaji mmojammoja, huku akiahidi kufanyia marekebisho udhaifu wa kiunfundi alioubaini katika vichapo hiyo.
Yamkini, udhaifu huo utakuwa umerekebika ndani ya siku mbili tangu juzi baada ya kichapo cha mabao 5-2 kutoka kwa mabingwa na vinara, Azam.
Lakini kwa upande wa pili, kuna asilimia fulani mchezo wa leo ukawa mgumu kwa Mtibwa, kutokana na kasi  ya Ndanda ambayo ikiwa kwenye uwanja wa nyumbani, Nangwanda Sijaona, imekuwa mwiba
mkali kwa timu vigogo, ambapo alichachafya Azam huku pia ‘ikiidindia’ Yanga. Hata hivyo bado wana kumbukumbu ya kuchapwa na Mtibwa mabao 3-1 katika mchezo wa awali, hivyo watataka kulipa kisasi.
Coastal Union vs Mbeya City
Hii ndio ‘match day’ ya leo kwenye ligi. Mtanange utakaopigwa kwenye Uwanja Mkwakwani Tanga, moja ya viwanja visivyoishiwa vituko.
Coastal wanaingia uwanjani wakiwa na furaha ya suluhu waliopata mbele ya Simba katika mchezo wao wa mwisho, lakini wakumbuke kuwa wanakutana na timu inayoibuka kama moto wa kifuu, ambayo imeanza kufanya vema baada ya kujitutumua kutoka mkiani na kupanda hadi nafasi ya 10, ikiwa na pointi 16, moja nyuma ya Simba.
Stand vs Mgambo Shooting
Benchi la ufundi la Stand United linajivunia mbinu walipewa na nguli wa zamani wa Barcelona Patrick Kluivert kwa kuwafundhisha mabeki jinsi ya kuokoa hatari na washambuliaji jinsi ya kuwatoka mabeki.
Mkurugenzi wa ufundi, Kanu Muhibu, alisema kutokana na ziara ya nyota huyo kwenye kikosi chao, anamini ni fursa pekee ya kuizamisha Mgambo leo.
Hata hivyo wanakutana na chui aliyejeruhiwa, baada ya kupoteza mchezo wa mwisho mbele ya Kagera kwenye uwanja huohuo wa Kambarage CCM, Shinyanga hivyo haitakuwa ngima rahisi kutokana na ukweli kwamba  timu zote zinapigana kutoka mkiani. Stand ipo nafasi moja kutoka mkiani, huku Mgambo wakiwa nafasi moja juu yao.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...