Monday, February 23, 2015

COUTINHO AZUA BALAA MBEYA, VIONGOZI WAHAHA KUMTULIZA


Mshambuliaji wa Yanga, Mbrazili, Andrey Coutinho.

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Mbrazili, Andrey Coutinho, juzi Jumamosi alizua balaa jijini hapa na kuwaacha midomo wazi baadhi ya viongozi wake huku wasijue la kufanya wakati kikosi cha timu hiyo kilipotinga kwenye Uwanja wa Sokoine kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya kujiandaa na mechi ya jana dhidi ya Mbeya City.

Balaa hilo lilitokana na mchezaji huyo kugoma kufuata maagizo ya viongozi hao ambao walimzuia asiende kukaa katika viti vilivyokuwa uwanjani hapo kwa ajili ya kuvaa viatu kabla ya kuanza mazoezi mpaka watakapokuwa wamevizindika kwa dawa maalumu ya kienyeji kutokana na kile kilichodaiwa kuwa Mbeya City tayari walikuwa wameshamwaga uchawi wao.

Coutinho aligoma kuwasikiliza viongozi hao kila walipokuwa wakimwambia asiende kukaa katika viti hivyo, badala yake yeye ndiyo kwanza alizidi kutembea akielekea sehemu hiyo.Kitendo hicho kilionekana kuwasononesha sana viongozi hao lakini kabla ya kukaa, kiongozi mmoja wa benchi la ufundi la timu hiyo, alikimbia na kwenda kumzuia asikae katika viti hivyo na anachotakiwa kufanya ni kwenda kusimama uwanjani.
Hali hiyo ilionekana kumshangaza sana Coutinho na kujikuta akinyanyua mikono yake juu, akimwomba Mungu kisha akaenda kusimama karibu kabisa na alipokuwa amesimama kocha mkuu wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm huku akishangaa kuona kilichokuwa kikifanywa na viongozi hao katika viti hivyo.
Baada ya mazoezi ya timu hiyo kumalizika, Coutinho aliliambia gazeti hili: “Nilijua walikuwa wananitania, ndiyo maana nilikuwa naenda kukaa katika viti hivyo, naomba wanisamehe kwa usumbufu walioupata.”

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...