Mrisho Ngassa.
KAMA umebahatika kwenda kwenye mazoezi ya Yanga, utagundua kuna mambo kadhaa muhimu yatakayosababisha mabadiliko katika mechi ya kesho ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika mazoezi hayo kwenye Uwanja wa Shule ya Sekondari ya Loyola, Mabibo, inaonyesha wazi kuwa Brandts atampanga Ngassa kama kiungo wa kushoto, nafasi aliyokuwa akicheza Haruna Niyonzima.
Ngassa ataanza kuichezea Yanga kwa mara ya kwanza kesho na Brandts anaonekana atamrudisha Niyonzima katika namba yake ya dimba la juu, yaani namba nane.
Kutokana na mfumo ambao amekuwa anautumia, inaonekana wazi kikosi cha Yanga kesho kitakuwa hivi, kipa ni Barthez, mbili na tatu Mbuyu Twite na David Luhende wakati katikati ni nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani.
Kiungo wa ukabaji atakwenda Frank Domayo ‘Chumvi’ na inaonekana mkongwe Athumani Idd ‘Chuji’ ataanzia benchi kwa kuwa alipewa ruhusa ya kwenda mjini Mpwapwa kwa ajili ya mazishi ya shangazi yake.
Pamoja na kuwa wengi waliamini kinda Simon Msuva atakaa benchi baada ya kurejea kwa Ngassa, kinachoonekana Mholanzi huyo atamchezesha kulia, yaani namba saba na Ngassa atakaa 11.
Niyonzima ni nane na kwa namna mechi iliyopita dhidi ya Azam FC ilivyokuwa, hakuna ubishi Brandts ataanza na wageni tupu kule mbele, Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza ambaye alionekana tishio baada ya kuingia. Hii ina maana, Jerry Tegete atakuwa ‘ubaoni’.
Brandts amekuwa akizigawa timu kwa mfumo fulani mazoezini ambao unaonyesha ataanza na kikosi hiki ambacho kama kweli wachezaji watatulia, basi si rahisi kukizuia.
No comments:
Post a Comment