Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi
Kigwangalla, jana alifanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha
COMMUNITY HEALTH EDUCATION SERVICES AND ADVOCACY- (CHESA) kilichopo Upanga,
Wilayani Ilala, jijini Dar es salaam.
Ziara hiyo ya kushtukiza inafuatia
baada ya hatua ya Naibu Waziri huyo wa Afya
Dk.Kigwangalla kuendelea kufanya
ukaguzi wa Asasi mbalimbali zisizo za kiserikali zikiwemo NGO’s na CBO zenye
makosa ya kiutendaji na kimfumo ambayo
ni tofauti na taarifa zao katika usajili wa Serikalini na namna ya uendeshaji
wa wao.
Mbali na hayo kituo hicho cha CHESA
kinashukiwa kuhusika na vitendo vya uhamasishaji wa mahusiano ya mapenzi ya
Jinsia moja (USHOGA), ambayo ni kinyume na mila na Desturi za kitanzania pamoja
na Katiba na sharia za Nchi.
“Mahusiano ya jinsia moja si kinyume
na mila na desturi zetu tu. Bali hata sheria na katiba ya nchi yetu haziruhusu
mfumo huo wa kimahusiano” amesema Dk..Kigwangalla
Aliendelea kubainisha kuwa: “Sisi
kama Serikali hatujawahi kusaini mikataba yoyote ya kimataifa inayoruhusu ushoga hivyo kwa taasisi yoyote hapa Nchini
inayofanya hivyo ni kuvunja sheria za Nchi na inapaswa kuchukuliwa hatua kali
za kisheria na hata kufutiwa usajili wake” aliongeza Dk. Kigwangalla.
Katika ukaguzi wa kituo hicho, Naibu
Waziri wa Afya Dk. Kigwangalla akiwa
ameambatana na Kaimu Msajili wa Asasi zisizo za kiserikali kutoka Wizara
anayoiongoza, Bw. Julius Mbilinyi pamoja na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Ilala, Hassan Selengu pia wamefanya ukaguzi katika kituo hicho ili
kubaini kama kuna uwepo wa vilainishi vinavyotumiwa na watu wenye mahusiano ya
jinsia moja ambavyo hivi karibuni Serikali ilipiga marufuku matumizi yake hapa
nchini.
“Serikali ilikifuta kituo cha ‘SISI
KWA SISI’ kwa sababu kilihusika na tuhuma za ushawishi wa mahusiano ya jinsia
moja ambacho pia wewe ulikuwa Mkurugenzi wake. Sasa tumeamua kuchunguza na
kituo hichi ili tujue kama mnahusika na vitendo hivyo ili tuchukue hatua endapo
itabainika ama la” ameeleza Dk. Kigwangalla.
Aidha, Naibu Waziri wa Afya Dk.
Kigwangalla amemtaka Mkuu wa upepelezi
Bwana Hassan Selengu afanye uchunguzi wa kina katika kituo hicho ili
kubaini pesa za misaada katika kituo hicho zinatokea wapi lakini pia ni kubaini
kama kituo hicho kinajihusisha na ushawishi wa watu kujiunga na mahusiano ya
jinsia moja.
“Tunawasiwasi kuwa mnapokea pesa
nyingi na misaada mingi kutoka katika
Taasisi mbalimbali lakini pesa hizo zinatumika kuhamasisha mapenzi na mahusiano
ya jinsia moja.
Mbali na hayo. taarifa za usajili wa kituo hichi zinakinzana
na malengo na miradi inayofanyika hapa.
Pia ipo miradi mbalimbali ambayo haijasajiliwa wala hujaitaja katika
maelezo yako lakini inafanyika katika
kituo hichi” alihoji Dk. Kigwangalla
huku akimtajia baadhi ya miradi hiyo ambayo Serikali inaitambua.
Na Hashim Ibrahim (UDSM-SJMC).
No comments:
Post a Comment