Saturday, February 6, 2016

SOMA HAPA SIMLIZI ZA MAISHA YA CHRISTIAN BELLA!


Christian Bella
CHRISTIAN Bella anaendelea kusimulia kuwa kitendo cha kumpa msichana huyo ujauzito hakikuzua kizaazaa kikubwa kwa sababu tu wakati huo kidogo alikuwa ana uwezo wa kuingiza shilingi mbili tatu ambazo ziliweza kumsaidia kumtunza mwanadada huyo na mtoto ambaye angezaliwa.

Anaendelea kusema kuwa jambo la muhimu aliloamua ilikuwa ni kujadiliana na msichana huyo namna ya kufanya ikiwemo yeye kwenda kujitambulisha nyumbani kwa mama mtoto wake huyo mtarajiwa.

“Mambo yalikwenda vizuri. Baada ya kufika kwao, wazazi wake hawakuwa na noma, zaidi walinipongeza kwa kitendo changu cha kwenda kujitambulisha na wakatutakia uhusiano mwema huku wakitusisitiza kufikiria pia juu ya suala la kufunga ndoa na kuishi pamoja,” anasema Bella na kuendelea kuwa;

Siku zikazidi kusonga mbele hatimaye miezi tisa ikatimia, mpenzi wake huyo akashikwa uchungu wa kuzaa, baada ya kukimbizwa hospitali akafanikiwa kujifungua mtoto wa kiume mwenye afya njema.

Bella anasema kwamba kuitwa baba ilikuwa ni furaha mpya maishani mwake. Anaongeza kuwa sababu ya kufurahi kwake ilikuwa ni kupata mtoto aliyempa jina la Jordan katika umri mdogo jambo ambalo vijana wengi wa umri wake hawakuwa wanalifurahia kutokana na mazingira ya kipato wakati mwingine kuwa magumu. Anasema walikuwa wanaogopa kuwa na mujukumu makubwa zaidi ya umri wao.

“Oke, vipi lakini, baada ya mtoto kupatikana ulimpeleka nyumbani kwa wazazi?” Nilimuuliza swali hilo lengo langu lilikuwa kumpa upepo kidogo ili apumzike baada ya ‘kufloo’ sana.

“Kwa nini nisimpeleke?” Aliniuliza swali, lakini kabla sijajibu akaendelea.

“Nilimpeleka kwa baba na mama na hadi sasa Jordan anaishi Kinshasa kwa wazazi wangu, mama yake yuko Uingereza kwa ndugu zake.”

“Alihamia huko lini?”

“Kipindi cha nyuma sana bado mimi mwenyewe nikiwa Kongo sijaja Tanzania. Wakati anaondoka alisema anakwenda Uingereza kwa ajili ya masomo lakini ndiyo akawa amehamia hivyo na kumuacha mtoto, mimi baadaye nilianzisha uhusiano na mwanamke mwingine,” anasema Bella.

“Sawa, ehee hebu turudi kwenye gemu la muziki, nini kiliendelea baada ya wewe na bendi yako kuachia albamu mpya ya Yako Wapi Mapenzi ambayo ilifanya vyema?”

Bella anasema baada ya albamu hiyo ambayo asilimia kubwa ya nyimbo zake alizitunga yeye lakini katika kuimba akashirikiana na wenzake wa bendi hiyo ya Chateau du Soleil kuzidi kufanya vizuri, mawazo yake yalibadilika na kutamani sana kuondoka kwenye bendi hiyo ndoto zake zikiwa kujiunga na Bendi ya Koffi Olomide.

Anaendelea kusema kuwa, haikuwa kazi rahisi kupata nafasi kwenye bendi ya Koffi iitwayo Quartier iliyokuwa inaonekana kukamilika huku ikiwa na wasanii wakali baadhi yake wakiwa Fally Ipupa na Ferre Gola.

Bella anazidi kuongeza kwa kusema kuwa baada ya kwenda kuomba nafasi kwenye bendi hiyo ya Koffi huku akiambatanisha na baadhi ya kazi zake alizokuwa amekwisha zifanya, Koffi alimkubalia baada ya kumzungukia kwa muda mrefu akimsisitizia juu ya ombi lake lakini hakupewa nafasi ya kufanya mazoezi na wasanii wakubwa wa bendi hiyo.

“Jambo hilo liliniumiza mno moyoni, lakini sikuwa na cha kufanya, niliamua kukaza katika mazoezi huku nikiamini ipo siku uwezo wangu utaeleweka, nitaingia kwenye orodha ya wasanii wakali ambao wangepewa nafasi ya mbele katika bendi,” Bella anasema na kuongeza kuwa;

“Katika mazoezi nikiwa na wasanii wenzangu chipukizi nilikuwa najitahidi sana kukopi uimbaji wa Ferre Gola maana ndiye alikuwa msanii ambaye nilimpenda na kutamani kuwa kama yeye.

Kutokana na juhudi nilizozionesha kwenye mazoezi ulifika wakati Koffi akaniambia nilikuwa nimeanza kuiva na akaniahidi baada ya muda mchache ningepewa nafasi ya kufanya mazoezi na wasanii wenye majina makubwa,” anasema Bella.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...