Diamond Platnumz akiwa kwenye pozi la huzuni. |
MAJANGA! Wiki iliyopita mambo hayakuwaendea poa mafahari wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ baada ya kila mmoja kupatwa na masaibu yake, Ijumaa Wikienda linakupa moja baada ya jingine.
TUKIO LA DIAMOND
Chanzo makini kilichoshuhudia sakata zima kilieleza kuwa, Jumanne iliyopita Diamond aliingia kwenye ‘tifu’ zito na kijana aliyefamika kwa jina la Salehe Hafidhi ‘Ans Ken’ baada ya kumharibia kamera yake aliyompa kwa lengo la kumfanyia kazi zake.
“Palichimbika, Diamond alimkabidhi Ans Ken kamera yenye thamani ya shilingi Mil. 12 kama kitendea kazi maana anafanya naye kazi. Sasa jamaa akaiharibu, Diamond alipohoji jamaa akajibu mbovu ndipo mtiti ulipoibuka.
“Ilikuwa ni mvutano mzito Diamond akimtaka kijana huyo amlipe kamera yake jamaa akawa analeta ubishi ndipo Dangote (Diamond) akaona isiwe shida bora akimbilie polisi Mabatini (Kijitonyama) kushtaki na jamaa akakamatwa na kuwekwa ndani,” kilisema chanzo hicho.
MTUHUMIWA AKANUSHA TUKIO
Baada ya mwanahabari wetu kunasa tukio zima, alimvutia waya mtuhumiwa (Ans Ken) ambaye aliachiwa kwa dhamana siku moja baada ya kuswekwa lupango ambapo alikanusha kuwa tukio la yeye kugombana na Diamond halikutokea.
“Kwanza mimi siitwi hayo majina uliyonitajia, sina tatizo na Diamond na wala sitaki kugombana naye siku si nyingi nimetoka naye South kufanya kazi,” alisema.
AZIDI KUJIKANYAGA
Alipohakikishiwa na mwanahabari wetu kuwa ana RB inayomuonesha kuwa yeye ni mtuhumiwa wa Diamond, Ans Ken kwa kujikanyaga alibadili kauli yake ya awali na kusema mtafaruku ni kitu cha kawaida katika kazi huku pia akiendelea kukanusha.
“RB si karatasi la kawaida tu, siyo kweli bwana. Hiyo siyo stori achana nayo, kwanza kwenye kazi kugombana mbona ni kitu cha kawaida si kila jambo litatangazwa, hajawahi kunifikisha polisi,” alisema kwa kujikanyaga maneno.
DIAMOND SASA
Kwa upande wake Diamond alipotafutwa simu yake iliita bila kupokelewa lakini Ijumaa Wikienda limenasa jalada la kesi hiyo aliyoifungua Diamond katika Kituo cha Poisi Kijitonyama iliyosomeka KJN/RB/2020/2016 KUHARIBU MALI.
Nay wa Mitego na gari lake lililovunjwa kioo.
TUKIO LA NAY SASA
Katika tukio jingine, Nay wa Mitego, alinusurika kifo baada ya kuvamiwa mara mbili kwa nyakati tofauti na watu wasiojulikana huku wakimuacha na maumivu ya kumvunjia vioo na taa za gari zake mbili.
TUKIO LA KWANZA
Akiwa katika Mitaa ya Kinondoni Manyanya, Februari 24, mwaka huu Nay alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuegesha gari lake aina ya Toyota Prado kandokando ya barabara ambapo alipoingia dukani na kurejea, alikuta limevunjwa taa ya upande wa kushoto na watu wasiojulikana.
MAJANGA ZAIDI
Kama hiyo haitoshi, usiku wa kuamkia Februari 27, mwaka huu akiwa mitaa ya Sinza-Kamanyola, Nay alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana ambao walimvunjia kioo cha nyuma cha gari yake Toyota Port aliyokuwa ametoka nayo usiku huo na kuigesha maeneo hayo.
Prado ya Nay wa Mitego kabla ya kuvunjwa taa ya nyuma. |
MSIKIE NAY
Akizungumzia matukio hayo, Nay alisema hajawahi kukutana na mwaka wa misukosuko kama mwaka huu baada ya kuachia wimbo wake wa Shika Adabu Yako ambao ndani yake ‘amewa-diss’ mastaa kibao wa Bongo.
“Dah! Naweza kujikuta hata nikimfanyia mtu maamuzi magumu, juzi tu nimetoka kuvunjiwa taa ya gari yangu ile Prado, nikiwa niko kwenye hali ya kutafuta fedha ya kununua taa, leo tena nimevamiwa na watu nisiowajua na wamenivunjia kioo cha gari yangu hii Toyota Port.
“Najua wanaonifanyia haya ni wajinga wachache ambao wanataka kupambana na mimi baada ya kuachia wimbo wangu wa Shika Adabu Yako, sasa kuanzia sasa itabidi niongeze zaidi umakini maana maadui wameongezeka japo nina RB ya kujihami,” alisema Nay.
TUMEFIKAJE HAPA?
Siku chache baada ya kuuachia Wimbo wa Shika Adabu Yako ambao ‘uliwachana’ mastaa wenzake kisha baadaye wimbo huo kufungiwa na Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Nay amekuwa akipokea vitisho mbalimbali kutoka kwa watu asiowajua licha ya kutoa taarifa katika Kituo cha Polisi Kimara-Mwisho, jijini Dar.