Thursday, February 26, 2015

NISAMEHE: HAKYANANI, NENO HILI LITAMWINGIZA LOWASSA IKULU

KIPYENGA! Mpambano wa kuteuliwa na hatimaye kupeperusha bendera ya Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka huu kuwania urais unazidi kushamiri huku jina la waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ‘EL’ likiongoza kutajwa midomoni mwa Watanzania.
Imebainika kuwa pamoja na  kelele nyingi zinazosikika mitaani za “Lowassa! Lowassa!” bado hazitoshi kumwingiza madarakani, kama Rais Kikwete hatamwona anafaa kuwa mrithi wake.
Lowassa alikuwa mmoja wa wanamtandao waliofanikisha kuingia ikulu kwa Rais Jakaya Kikwete ‘JK’ katika uchaguzi wa mwaka 2005. Baada ya JK kuingia ikulu,  Lowassa aliteuliwa kuwa waziri mkuu wa serikali ya awamu ya nne hadi alipojiuzulu, Februari 2008 kufuatia tuhuma za kashfa ya mkataba tata wa Kampuni ya Kufua Umeme ya Richmond.

Rais Jakaya Kikwete ‘JK’.
WANAMTANDAO WENGINE
Mbali na Lowassa, wanamtandao wengine waliofanikisha JK kuingia ‘magogoni’ ni Bernard Membe, Emmanuel Nchimbi, Abdulahman Kinana na Rostam Aziz.
Kwa utaratibu usio rasmi wa mitandao ya kisiasa duniani, Rais Kikwete baada ya kumaliza muhula wake wa miaka kumi anatakiwa kumrithisha kiti mmoja kati ya wanamtandao waliopigana kufa na kupona kumwingiza madarakani.
Miongoni mwa wanamtandao hao, Kinana ana kikwazo cha kugombea kwa sababu tayari amezunguka nchi nzima kukisafisha chama chake, wakati wenzake wakiwa wamepigwa kufuli, hivyo kitendo cha kuchukua fomu kitatafsiriwa kama aliwazuia wenzake ili yeye apate nafasi ya kujitangaza.
Mwanamtandao mwingine ni Rostam ambaye kwa sababu ya shughuli zake nyingi za kibiashara, hana ndoto za kuingia ikulu na kuongoza taifa. Hii inafanya wabaki wanamtandao watatu, Lowassa, Nchimbi na Membe.
Edward Ngoyai Lowassa.
Duru za kisiasa zinaonesha kuwa yeyote kati ya watatu atakayeungwa mkono na rais aliyeko madarakani anayo nafasi kubwa ya kuibuka rais kama atawashinda wagombea wa vyama vya upinzani.
Pamoja na kung’ara kwa Lowassa, wachambuzi wa siasa za ndani wa chama tawala na serikali wanampa nafasi ndogo ya kupenya kukiwakilisha chama chake kupambana na wapinzani kutokana na mambo kadhaa, lakini kubwa likionekana ni fununu za kutoungwa mkono ndani ya chama chake, hasa na baadhi ya viongozi wa juu.
Imedaiwa kuwa jambo pekee linaloweza kumfanya Lowassa akafanikiwa kuvunja kuta zilizoko mbele yake ni kuketi mezani na mwenyekiti wa chama chake (Kikwete), kufanya mazungumzo magumu juu ya tofauti zozote zilizopo ndani ya chama chake na ikibidi kuomba msamaha, afanye hivyo.
Kitendo cha Lowassa kuchelewa au kupuuza jambo hilo kinaweza kusababisha Rais Kikwete kumuunga mkono mtu mwingine miongoni mwa wanamtandao watakaochukua fomu kuwania nafasi hiyo jambo litakalofanya uwezekano wa yeye kuingia ikulu kuwa finyu.
NAPE AMETAJWA TOKA ZAMANI
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Nape Nnauye  anatajwa kuwa mpinzani ‘nambari wani’ wa EL huku mwenyewe akijitetea kwamba anachokifanya si kumpinga Lowassa bali ni kusimamia maadili ya chama chake.
Hivi karibuni, Nape alisema kuwa, rais ajaye lazima awe mwadilifu wa kutosha kwa vile licha ya nafasi hiyo serikalini, pia ndiye atakayekuwa mwenyekiti wa chama taifa.
RAIS NI RAIS TU!
Ingawa historia ya nchi ya Tanzania haimpi nafasi rais aliye madarakani kumpendekeza, kumteua au kumpitisha mtu anayemtaka ashike kijiti chake, lakini bado mfumo wa utawala unatoa nafasi kubwa kwa rais kushawishi kwenye ngazi husika ili kumpata mgombea wa kwenda kupambana na vyama vingine.
Vipo vikao rasmi na visivyo rasmi vinavyohusika katika kuwachuja wagombea, achilia mbali taasisi zingine za kiserikali zinazohusika kumpata mtu muafaka, hasa Usalama wa Taifa.Katika chama, majina yote ya wanachama wanaotaka urais yatapaswa kwanza kujadiliwa na Kamati Kuu (CC), ambako mwenyekiti wa kikao hicho ni rais aliye madarakani.
Kabla, baraza la wazee linalowajumuisha marais wastaafu, litahusika kupitia majina hayo ili kutoa baraka kabla ya CC.Ingawa EL anaonekana ana mtaji mkubwa wa watu, hiyo inaweza kuwa sababu isiyo na mashiko kwa sababu mfumo wa uchaguzi hauwapi wananchi nafasi ya kuwateua wagombea katika hatua za awali, badala yake Rais Kikwete anabaki kuwa na nguvu ya uamuzi kutokana na mamlaka aliyonayo kwenye mabaraza ya awali ya uteuzi.
Duru za kisiasa zinaeleza kwamba kabla ya baraza la wazee halijakaa kuwachambua wagombea wote wa nafasi ya urais, rais wa nchi huulizwa chaguo lake. Kwa hiyo kama JK  hatamwona EL anafaa kuwa mrithi wake hatampendekeza.
Kwa upande wa Kamati Kuu ambako rais ni mwenyekiti, ana nafasi kubwa ya kushawishi kuondolewa kwa jina asilolitaka kabla ya kupelekwa katika Mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa ajili ya kupigiwa kura ya mwisho ya kupata wagombea watatu ambao watapelekwa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM ili kumpata mmoja ambaye ndiye atakuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
Lakini hata kama ushawishi wake kwa wajumbe wa kikao hicho utashindwa kuliondoa jina asilolitaka, bado yeye kama mwenyekiti wa chama anayo turufu ya kuliondoa kwenye Mkutano wa NEC.
Nguvu hii ya ushawishi inafanya kitendo cha Lowassa kukaa meza moja na Kikwete kuwa cha lazima ili kufanya safari yake kwenda ikulu kuwa rahisi na laini.
Hata hivyo, ziko taarifa za kuwepo kwa wajumbe wa kamati kuu ‘maslahi’ ambao huangalia zaidi maisha yao ya baadaye kisiasa, ambao hupenda kuwekeza kwa kiongozi atakayeingia baada ya aliyepo kuondoka. Hawa wanaweza kuonesha kumuunga mkono rais lakini wakati wa kupiga kura wakageuka.
WAKATI HUOHUO
Wakati hilo likiendelea, Kamati Kuu ya CCM (CC), itategua kitendawili dhidi ya makada sita waliopewa adhabu ya mwaka mmoja kwa madai ya kuanza kampeni za kuwania urais ndani ya chama hicho kabla ya wakati.
Katika kikao hicho kitakachofanyika kesho Februari 28, jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM, Philip Mangula, atawasilisha ripoti yake ya tathimini dhidi ya makada hao kama walitii adhabu waliyopewa na chama ya kutojihusisha na kampeni mapema au la! Makada hao walipewa adhabu hiyo Februari 18, mwaka jana.
Katibu wa Nec, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ilisema juzi kuwa kikao hicho cha CC kitafanyika chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete.Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya CCM Mtaa wa Lumumba, Dar kiliiambia Uwazi Mizengwe ya Uchaguzi  kuwa, kwa siku kadhaa Kamati ya Mangula imekuwa ikifanya vikao vyake hadi usiku wa manane kuwajadili makada hao.
Makada hao ni Lowassa, waziri mkuu mstaafu awamu ya tatu, Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Steven Wasira, Naibu Waziri wa Mawasiliano Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Sengerema kwa tiketi ya CCM, William Ngeleja.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...