Tuesday, February 17, 2015

ANGALIA HAPA JINSI YA KUGAWANA MALI MUME NA MKE NDOA INAPOVUNJIKA


Na Bashir Yakub

NDOA inapovunjika kuna kuna mambo makuu matatu ambayo hutokea kutokana na ndoa hiyo kuvunjika. Kwanza ni kugawana mali walizochuma wanandoa, pili hifadhi ya watoto na tatu matunzo ya watoto. Haya ni matokeo ya kuvunjika kwa ndoa, mengine zaidi kuhusu kuvunjika kwa ndoa tutayaona hapa wakati nikieleza mgawanyo wa
mali za wanandoa.

1.MALI ZIPI HUTAKIWA HUGAWANYWA NDOA INAPOVUNJIKA?

Ndoa inapotangazwa kuvunjika, mali ambazo hupaswa kugawanywa ni mali za wanandoa wenyewe. Swali mbele yetu ni kuwa ni zipi mali za wanandoa? Mali za wanandoa ni zile zote zilizochumwa na wanandoa hao kwa jitihada au juhudi za pamoja wakati wa ndoa yao.

Mali hizo zaweza kuwa zinahamishika au hazihamishiki. Mali zisizohamishika ni kama nyumba, viwanja, mashamba n.k. Mali zinazohamishika ni kama magari, baiskeli, pikipiki,vifaa vya ndani kama fenicha, fedha benki, na mali nyingine ambazo hazionekani kwa macho au hazigusiki kama hisa n.k.

Zingatia sana usije kudhulumiwa kwa kuwa hata hisa pamoja na akiba ya fedha benki nayo ni mali inayostahili kugawanywa.

2. JE MALI ILIYOPATIKANA KABLA YA NDOA HUGAWANYWA?

Mali zilizopatikana kabla ya ndoa haziwezi kugawanywa ndoa inapovunjika isipokuwa tu kama zilibadilishwa kuwa za wanandoa wakati wa ndoa. Swali ni zinawezaje kubadilishwa kuwa za wanandoa? Zinabadilshwa kuwa za wanandoa iwapo wanandoa walikubaliana kwa makubaliano maalum kuwa mali kadha wa kadha zitakuwa zao wote.

Na hii inaweza kuwa kwa maandishi au kwa kubadili majina ya nyaraka za umiliki na kuzifanya kuwa na majina yote mawili ya wanandoa kutoka la mmoja la awali. Lakini pia zaweza kuwa za kwao wote kimatendo, kwa mfano kabla ya ndoa mmoja wa wanandoa alikuwa na nyumba lakini haijamaliziwa.

Wakati wa ndoa nyumba hiyo ilimaliziwa kwa nguvu zao za pamoja na sasa imekamiliki. Nyumba ile inageuka kuwa ya wote. Kwa ufupi maendelezo yoyote yanayofanywa na wanandoa katika mali ambayo hapo awali kabla ya ndoa ilimilikiwa na mmoja peke yake, yanaibadilisha mali ile kuwa ya ndoa. Hata kupaka rangi ni tendo la kuifanya mali kumilikiwa kwa pamoja na hivyo kustahili mgao ndoa inapovunjika.

3. MAMA WA NYUMBANI LAZIMA APATE MGAO NDOA INAPOVUNJIKA?

Hapo juu wakati naeleza maana ya neno mali za wanandoa ambazo hustahili mgao ndoa inapovunjika, nilieleza kuwa mali hizo inabidi ziwe zimepatikana kwa nguvu, juhudi au jitihada au mchango wa pamoja kipindi cha ndoa. Swali ni nini maana nguvu, jitihada, au mchango wa pamoja?

Watu wengi hujua kuwa juhudi au mchango wa pamoja unaopelekea mali kuwa za wote na hivyo kustashili mgao ndoa inapovunjika ni ile ya ‘leta nilete’. Yaani kama ni nyumba inajengwa mume akitoa saruji mwanamke atoe nondo au mume akitoa hela na mwanamke atoe hela na kama ni gari mwanaume akitoa milioni kadhaa na mwanamke naye achangie za kwake kadhaa na hapo ndipo itakuwa mali yao wote na eti hapo ndipo mgao unapostahili. Hiyo ina maana lakini finyu sana!

Maana ya kisheria ya mchango au juhudi za pamoja hujumuisha kazi anazofanya mama nyumbani wakati baba akiwa nje ya nyumba kwa uzalishaji mali. Kuosha vyombo, kupika, usafi wa nyumbani, kutunza na kuandaa watoto, kufua, na kila kazi ya nyumbani ni mchango na juhudi ya pamoja kwa maana niliyosema na lazima ilipwe kwa kugawana mali ndoa inapovunjika.

Kwa maana hii mama wa nyumbani hustahili mgao wa mali ndoa inapovunjika. Hii ni sheria na kufanya hivyo ni lazima, si hiari wala hisani ya mtu.

4. KWA NINI SHERIA IMEAMURU MGAO WA MALI KWA MAMA WA NYUMBANI?

Sheria inamini kuwa wakati wa ndoa mwanamke huwa ametoa sadaka maisha yake na utu wake katika kuwatunza watoto (kama wapo) na kuitumikia familia kwa ujumla kwa kufanya kazi zote za nyumbani kitu ambacho humwekea ugumu wa kuzalisha pesa na baadhi ya mali zitokanazo na pesa.

Sheria inaamini kuwa hilo hutokana na nafasi yake hiyo ya kuwa mwangalizi wa nyumba wa muda wote. Hivyo basi haiwezi kuwa busara, hauwezi kuwa ubinadamu, hauwezi kuwa utu, hauwezi kuwa ustaarabu, haiwezi kuingia katika akili ya yeyote na haiwezi kamwe kuwa sawa kwa mwanamke kama huyo, baada ya talaka, asipate chochote na aondoke bila chochote baada ya kuwa amepoteza miaka mingi katika kuitumikia familia hiyo.

Hii ndiyo sababu kuu ya kumpa mgao wa mali mama ambaye hushinda nyumbani.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...