Friday, January 17, 2014

SOMA YA DIAMOND UPATE KUMSHAURI



 
 JINA lake lipo juu mno, pengine kuliko msanii mwingine yeyote kati ya vijana wanaotingisha anga ya muziki wa kizazi kipya kwa sasa. Siyo jambo la busara hata kidogo, kubeza uwezo wake katika kumiliki jukwaa, jinsi anavyojituma na zaidi, tungo zake zinazoendelea ‘kubamba’ kila kukicha, ingawa zina ujumbe unaofanana, kuhusu mapenzi!
Hapa ninamzungumzia Nasibu Abdul maarufu kwa mashabiki kama Diamond, yule kijana aliyeibuka akitokea mitaa ya Tandale, jijini Dar es Salaam, ambaye sasa anakula kuku kwa mrija katika maeneo ambayo miaka mitano nyuma ilikuwa ni sawa na kumdhihaki mtu aguse mbingu!
Wakati flani nilipata kuandika habari zake, muda ambao rafiki yangu Said Mdoe alikuwa akimtumia katika baadhi ya maonyesho yake, akimchanganya na Mzee Yusuf wa Jahazi Modern Taarab. Kutokana na ugeni wake katika fani, nilipata taabu sana kulijua jina lake, kila siku nilikuwa nikiuliza, anaitwa nani vile?!!
Hivi sasa habari imegeuka, dogo anatisha na sidhani kama Mdoe anaweza tena kumpandisha katika jukwaa, sijui! Binafsi sijawahi kukutana na supastaa huyu, si kikazi wala bahati mbaya. Ninamsikia kama wengi wanavyomsikia, ingawa tofauti yetu ni kwamba mimi sina mzuka naye!
Nimekuwa nikipata simu na sms nyingi katika safu hii, zikimlalamikia, kwamba anaringa na kujisikia. Kama nilivyosema awali, sijawahi kukutana naye, sijawahi kuzungumza naye na sitaki dhambi ya kumjaribu mtu. Kwamba nijaribu kulazimisha nafasi ya kukutana naye ili nithibitishe madai dhidi yake, naona nitakuwa sitendi haki.
Lakini nimejikuta nikilazimika kusema naye baada ya baadhi ya waandishi wenzangu, nao kujiunga na mashabiki juu ya lawama za nyodo za Diamond. Eti sasa hapokei simu zao, hajibu sms zao, hata kama zitakuwa ni kwa ajili ya kuzungumzia kazi zake mwenyewe.
Wanapojaribu kuniambia kuhusu jinsi alivyokuwa anahangaika kuwatafuta wakati ule akipanda mlima, sishangai kwa sababu ninayo orodha ndefu ya wasanii wa aina hiyo. Baadhi yao walikaa kwenye maboksi nje ya ofisi, wakisubiri tumalize kazi ili tufanye nao mahojiano, na walipiga simu kila mara kuulizia kuhusu kutoka kwa habari zao.
Lakini hata walipofanikiwa, heshima iliendelea kuwepo. Ingawa sasa hawawezi kukaa tena kusubiri kwenye maboksi, lakini angalau walipiga simu kusalimia na mara zote walikuwa wepesi kupokea tulipowapigia na kama walikuwa bize, hawakusita kueleza.
Tunao wasanii wa aina hiyo, hadi leo tuko nao pamoja wakiendeleza harakati, bila kujali wana mafanikio kiasi gani. Diamond ni kijana mdogo, aliyepata mafanikio ghafla. Ingawa mwenyewe amekuwa akielezea jinsi alivyosota, akitaka tuamini kwamba amehangaika sana, lakini kwa umri wake, nadhani haelewi nini hasa maana ya msoto.
Kama leo anawadharau waandishi, kwa maana labda sisi tunaoandika magazetini, ambao tulitumia muda mwingi kumpamba ili atoke, huenda pia hivi sasa anaweza kuwa anamdharau mama ntilie, aliyekuwa akimkopesha ukoko wakati ule. Na ni jambo la kutegemea pia kwamba, huenda anawadharau washkaji aliokuwa akishinda nao ghetto!
Nimshauri tu kuwa kelele dhidi yake zimekuwa nyingi, na bahati mbaya zingine zinatoka kwa baadhi ya mashabiki wake. Maringo, kujisikia na kujisifu ni hulka ya mtu, haizuiliki, lakini unapojaribu kutaka kuwa mtu wa watu, ni vyema kuepuka baadhi ya tabia kwa manufaa yako na wadau wako.
Nimkumbushe tu kuwa wapo wasanii ambao walianza kuwika tokea kuanza kwa game na bado hadi leo wako levo za juu, lakini ushirikiano wao kwa wanahabari, mashabiki na wadau ni wa hali ya juu!

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...