Monday, January 20, 2014

SHOMARI KAPOMBE KUTUA YANGA SC

Baada ya chenga za hapa na pale, kila kitu sasa kimewekwa hadharani kwamba beki wa zamani wa Simba, Shomari Kapombe, ametaka mkataba wake na AS Cannes ya Ufaransa uvunjwe na imeelezwa anataka kubaki nchini na kujiunga na Yanga.
Habari za uhakika kutoka ndani ya AS Cannes nchini Ufaransa na kuthibitishwa na wakala wake anayeishi nchini Uholanzi, zimeeleza Kapombe amefanya mazungumzo na Yanga ambao wamemshawishi kubaki nchini.
Mmoja wa viongozi wa AS Cannes ameliambia Championi Jumatatu kwamba: “Shomari amesusa kuja na anataka mkataba wake uvunjwe, lakini bado hatujaelewa hasa tatizo ni nini, ila tunajua amefanya mazungumzo na timu ambayo ni mabingwa wa Tanzania (Yanga), kitu ambacho si sahihi.
“Amesema anataka kubaki Tanzania, kidogo inatushangaza kwa kuwa kesi yake moja kuhusiana na kutaka kulipwa fedha imefika Fifa, lakini ajabu kabisa hatukuwahi kukataa kumlipa, badala yake tulisimamisha malipo kutokana na kuchelewa kwake. Huo ndiyo ukweli, ila sipendi jina langu liandikwe gazetini.”
Blogu hii ilikuwa ya kwanza kuandika kuwa Kapombe amekwama nchini na yuko mkoani Morogoro licha ya kuripotiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwamba alishaondoka kwenda Ufaransa.
Juhudi za kumpata wakala wake, Dennis Kadito akiwa nchini Uholanzi anakoishi zilizaa matunda jana na akasema ana taarifa za Yanga pamoja na Azam FC kufanya naye mazungumzo.
“Kweli kuna hizo taarifa, si nzuri kwa kuwa ni kukiuka utaratibu. Tayari Kapombe amesema anataka mkataba uvunjwe, kama umesikia hivyo ni sahihi. Nawashauri Yanga au Azam kama wanamtaka waje nizungumze nao tukae na AS Cannes, basi tumalizane.
“Mkataba wake ni wa miaka miwili, hivyo wasitumie njia ya mkato kwa kuwa mambo yako wazi na mimi au AS Cannes hakuna mwenye shida,” alisema.
Kapombe alitokea Simba na kujiunga AS Cannes bure, Simba ikitegemea kupata fedha kama atauzwa katika timu nyingine za Ulaya, lakini mgogoro ulianza baada ya kutolipwa mshahara wake kutokana na kutokuwa na akaunti ya benki za kule Ufaransa lakini baadaye alilipwa baada ya kumaliza utata huo.
“Kweli kuna fedha anadai, utaona katika miezi minne aliyokuwa Ufaransa hajalipwa mwezi mmoja. Hii inatokana na ile ishu ya kuchelewa alipokuwa katika timu ya taifa. Halafu, awali alichelewa kulipwa kutokana na suala kutokuwa na kibali cha kazi kilichochelewesha ashindwe kufungua akaunti ya benki.
“Ila AS Cannes ambao walikasirishwa na Kapombe kuchelewa Tanzania walitaka TFF ndiyo wamlipe mshahara kwa kuwa ndiyo walimchelewesha, sasa kesi yake iko Fifa. Ninaamini atashinda na mimi niko upande wake maana ndiyo wakala wake.
“Lakini bado nasisitiza kuwa lazima Yanga wafuate utaratibu maana taarifa za kuzungumza naye ninazo na ni za uhakika,” alisema wakala wake huyo.
Kiongozi wa AS Cannes alisema wametumia mamilioni ya fedha kumtibu Kapombe, lakini wanashangazwa na mambo yanavyokwenda.
“Suala lake tutalishughulikia baadaye, tulikuwa na mechi muhimu na ngumu za FA. Tumeitoa St Etienne inayoshiriki ligi kuu, sasa tutarudi kushughulikia suala lake ingawa tunaweza kulifanyia kazi zaidi baada ya Fifa kutoa hukumu.”
Yanga wamekuwa wakikataa katakata kulizungumia suala la Kapombe kwa hofu ya kuingia kwenye adhabu ya kuzungumza na mchezaji mwenye mkataba.
“Najua sasa Yanga hawawezi kukubali, ila wanawasiliana naye na walishakaa wakamalizana kwa mazungumzo ya awali na sasa kuna mambo kadhaa wanamsaidia,” alisema rafiki yake aliyetoa siri kwa mara ya kwanza kuwa yuko Morogoro.
Taarifa zinaeleza Yanga wamelenga kumjumlisha kwenye dirisha la Caf kama watasonga mbele au mwanzoni mwa msimu mpya, mara tu baada ya dirisha kufunguliwa.
Kabla ya kuondoka nchini na kujiunga na AS Cannes inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Ufaransa, Kapombe alikuwa nahodha msaidizi wa Simba.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...