Wednesday, February 27, 2013

RIPOTI KAMILI KUHUSU KUFUNGWA KWA VITUO VIWILI VYA REDIO PAMOJA NA FAINI WALIYOTOZWA CLOUDS FM



Makamu Mwenyekiti wa Kamati Maadili ya Utangazaji nchini, Walter Bgoya (katikati) akizungumza na wanahabari  jijini Dar es Salaam ukumbi wa habari Maelezo

KAMATI ya Maadili ya Utangazaji nchini imevifungia vituo viwili vya radio pamoja na kukipiga faini kituo cha Clouds FM kutokana na kukiuka maadili ya utangazaji.

Vituo hivyo vya redio ambavyo vyote kwa pamoja vimefungiwa kutorusha matangazo yake  kwa miezi sita ni pamoja na Imani FM cha Dar es Salaam na Kwa-Neema FM kilichopo mkoani Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Walter Bgoya alisema Kituo cha Clouds FM kimetakiwa kufuta kipindi
chake cha Jicho la Ng'ombe mara moja pamoja na kulipa faini ya sh. milioni 5.

Akifafanua zaidi Makamu Mwenyekiti huyo alisema vituo vya Imani FM na Kwa-Neema vimefungiwa kwa kosa la kufanya kazi zao kwa uchochezi jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya tasnia ya utangazaji. Kituo cha Clouds FM kimetakiwa kutoanzisha kipindi kingine kinacho fanana na Jicho la Ng'ombe.


Kituo cha Imani FM kinadaiwa kufanya uchochezi kwa wananchi juu ya suala la sensa ya watu na makazi huku kile cha Kwa-Neema kufanya uchochezi juu ya mgogoro wa

uchinjaji wanyama kwa Waislamu na Wakristu mkoani Geita.


Hata hivyo Kamati ya Maadili imeweka mlango wazi kwa vituo hivyo kukata rufaa endapo havikuridhika na adhabu vilivyo pewa kutokana na makosa vinao daiwa kufanya.

Kamati Imevitaka vyombo vyote vya habari kufanya kazi kwa kuzingatia Kanuni Sheria na maadili ya tasnia hiyo ili kuepuka kuzua migogoro kwa wananchi ambao wamekuwa wakiviamini vituo hivyo.

Hata hivyo mara baada ya ujumbe wa kamati hiyo kumaliza kusoma adhabu hizo kwa waandishi wa habari haukuruhusu maswali kwa waandishi wa habari, hivyo waandishi kubaki wameduwaa.

Waandishi wa habari wakiwa katika mkutano huo



No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...