Wednesday, April 11, 2012

........BABA WA KANUMBA ASHINDWA KUHUDHURIA MAZISHI YA MWANAE.......SHIBUDA AMWAKILISHA.......
MBUNGE wa Maswa Magharibi, John Shibuda jana alimwakilisha baba wa msanii maarufu wa filamu nchini marehemu Steven Kanumba katika mazishi ya msanii huyo akidai kuwa baba huyo Charles Kusekwa Kanumba ameshindwa kuhudhuria mazishi hayo kutokana na kusumbuliwa na maradhi ya malaria na shinikizo la damu na si matatizo yake na merehemu huyo. Kupitia uwakilishi huo, Shibuda pia alisoma barua aliyoeleza kutoka kwa mzazi huyo wa Steven Kanumba akieleza kushindwa kwake kufika kwenye mazishi hayo na kwamba ametuma watoto wake na wakwe zake kumwakilisha. "Baba yake Kanumba siku ya Jumamosi alikuwa anajisikia vibaya na alipokwenda hospitali alipimwa na kukutwa ana malaria 15 na shinikizo la damu likiwa 180 - 140. Lakini pia ana matatizo ya miguu kwa muda mrefu, anatembea kwa msaada wa baiskel,"alisema Shibuda. Akisoma barua hiyo Shibuda alinukuu barua ya baba wa Kanumba akisema:"Salam, nashukuru wana kamati ya mazishi ya mwanangu kwa kunitumia nauli ili niweze kuja kumzika mtoto wangu. Lakini kutokana na maradhi yanayonikabili sitaweza kuja, ila nawatuma wanangu Michael na Mjanael, pia mkwe wangu Chrisant Msipi waniwakilishe. Matatizo yangu na mwanangu yalishakwisha." "Msianze kuleta maneno yenu ya umbea umbea na uzushi eti hajafika kwenye msiba wa mwanawe kwa kuwa hawaelewani huo ni uzushi, walishaelewana na alikuwa na mawasiliano mazuri na mke wake mama Kanumba na ndiyo maana akatuma wawakilishi wake,"alisema Shibuda.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...