Kopa, Msaga Sumu
kupagawisha ‘Amsha Mama’ kesho
MKONGWE wa miondoko ya
mipasho nchini, Khadija Kopa, na mkali wa Singeli, Msaga Sumu, hatimaye
wamejitokeza na kujigamba kuwa kesho wataonyesha maajabu ya nguvu katika
tamasha la Amsha Mama Festival litakalofanyika katika Viwanja vya Mwembe-Yanga
Temeke jijini Dar es Salaam.
Wakizungumza mbele ya
waandishi wa habari ndani ya ukumbi wa Travertine, Magomeni jijini Dar, Khadija
Kopa na Msaga Sumu walisema kwamba kwa makamuzi waliyojipanga nayo kesho kwenye
tamasha hilo kuna hatari ya ‘kufia jukwaani’ kwani wamejipanga kutoa burudani
kwa wakazi wa Temeke kiasi ambacho hawajawahi kukifanya kwenye maisha yao.
“Kusema kweli sisi kwa
pamoja tumejipanga kuwaburudisha mashabiki zetu wote kwani tuna uhakika kama
tutapewa muda mrefu wa kufanya shoo basi kuna hatari ya kufia jukwaani kwani
muziki wetu ni wa watu wa Temeke hivyo hatuna budi kesho kufanya kila
linalowezekana ili tu tuweke historia mpya kupitia tamasha hili la Amsha Mama
Festival”, alisema Kopa.
Kwa upande wa Mratibu
Mkuu wa Tamasha hilo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa lebo ya Candy na Candy Records,
Joe Kariuki, tamasha hilo linalotarajiwa kufanyika mapema kesho ni mahususi kwa
kuwaamsha wanawake wote wa Afrika Mashariki na Kati ili waweze kupata nafasi ya
kujituma bila uoga katika biashara na kazi zao mbalimbali.
“Ukiachilia mbali hilo
la kuwaamsha kinamama pia kesho kutakuwa na wasanii kibao wa hapa nchini
wakitumbuiza, miongoni mwa wasanii hapo ni Juma Nature, Khadija Kopa, Mr Blue,
Snura, Msaga Sumu, Ali Chocky, Roma, Young Killer na Tunda Man,” alisema Joe
huku akiwataka watu wote wajitokeze kwa wingi kwani tamasha hilo ni la bure.
Mratibu Mkuu wa Tamasha hilo, Joe Kariuki, akisisitiza jambo juu ya tamasha hilo.
|
Mkali wa miondoko ya
Singeli, Msaga Sumu, akielezea namna atakavyowapagawisha wakazi wa Temeke hiyo
kesho.
|
No comments:
Post a Comment