Wednesday, February 3, 2016

YANGA YAMEWAFIKA HAPAAA ....NI BAADA YA KAMUSOKO NAYE KUA NJE YA TIMU HIYO!


Kiungo  tegemezi wa klabu ya Yanga Mzimbabwe, Thabani Kamusoko (kushoto), akipiga stori na kiungo mwenzake Haruna Niyonzima.
WAKATI Yanga ikiingia dimbani leo ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kuchafuliwa rekodi yao kwa kufungwa katika mechi iliyopita, ghafla inakumbana na balaa lingine la kumkosa kiungo wao wa kimataifa, Mzimbabwe, Thabani Kamusoko.
Kamusoko anatarajia kukaa jukwaani leo wakati Yanga ikitaka kurekebisha makosa mbele ya Tanzania Prisons katika mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya kutokana na majeraha aliyonayo ya enka ya mguu wa kulia.
Thabani Kamusoko.
Yanga ilichafuliwa rekodi yao ya kutofungwa tangu kuanza kwa msimu huu baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Coastal Union, wiki iliyopita ambapo kichapo hicho kiliwafanya kutofautiana kwa pointi tatu pekee na wapinzani wao, Simba SC, badala ya sita kama ilivyokuwa awali.
Kukosekana kwa Kamusoko katika mchezo huo ni pigo kubwa kwa Yanga kutokana na mchango mkubwa wa Mzimbabwe huyo kwa sasa ambaye tayari ameshafunga mabao matano na kuisaidia Yanga kukwea kileleni kwa pointi 39. Kamusoko anayesifika kwa kutawanya mipira pande zote za uwanja huku akimudu vyema majukumu ya kupiga pasi za mwisho kwa ustadi mkubwa, ameliambia Championi Jumatano kuwa hatakuwepo kwenye mchezo huo kutokana na maumivu makali anayoyasikia kwa sasa.
“Hapana, sitaweza kucheza kwenye mchezo wa kesho (leo), dhidi ya Prisons kwa sababu nina maumivu ya enka ya mguu wangu wa kulia. Inaniuma kuikosa hiyo mechi lakini nitajitahidi nipone haraka ili nirejee mapema uwanjani,” alisema Kamusoko.
Hata hivyo, gazeti hili lilipowasiliana na kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi, Hans van Der Pluijm, alifafanua zaidi kuhusiana na hilo na kwamba mchezaji huyo kwa sasa amepumzishwa na anatarajia kuanza mazoezi Alhamisi ya kesho kuangalia maendeleo ya hali yake.
“Kuna tatizo kidogo hapa, Kamusoko yupo nje ya kikosi, ana majeraha ya enka na anatakiwa kupumzika kwa saa 48 kabla ya kurudi tena mazoezini Alhamisi kuangalia anaendeleaje, siwezi kusema kwamba anaweza kukaa nje kwa muda gani mpaka hapo nitakapopata majibu ya daktari baada ya kumcheki tena.
“Kuhusu nani ataziba nafasi yake, naendelea kuangalia kwa kuwa nina wachezaji wengi wazuri wapo fiti, hakitaharibika kitu nafikiri kesho (leo) mapema kila kitu kitajulikana,” alisema Pluijm.
Ingawa kocha huyo hakuwa tayari kufafanua kuhusiana na atakayeziba pengo la Kamusoko ambaye kwa mara ya kwanza anakosa mechi ya ligi tangu atue Yanga, lakini kulingana na hali ya kikosi hicho ilivyo kwa sasa ni wazi Mnyarwanda, Haruna Niyonzima anarejea kikosini kuchukua nafasi hiyo.
Hiyo sasa imekuwa tofauti na ilivyokuwa ikidhaniwa kuwa Mbuyu Twite, anaweza kuchukua mikoba ya beki wa kati baada ya Kelvin Yondani, kuwa nje kwa kadi nyekundu na badala yake ataendelea kubaki kama kiungo mkabaji akiwasaidia ulinzi mabeki wa kati Pato Ngonyani atakayechukua nafasi ya Yondani akishirikiana na Mtogo, Vincent Bossou.
Kamusoko anaungana na nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Haji Mwinyi wanaosumbuliwa na majeraha kwa kipindi kirefu sasa.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...