Tuesday, January 26, 2016

BUNGE LAANZA KURINDIMA DODOMA LEO!

Spika mpya wa Bunge la 11, Job Ndugai.
MKUTANO wa Pili wa Bunge la 11 unaanza leo mjini Dodoma ambapo Bunge litajadili hotuba ya Rais kwa muda wa siku tatu.

Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano wa Bunge, Owen Mwandumbya alisema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari mjini hapa.

Alibainisha kuwa Bunge litamaliza vikao vyake Februari 5, mwaka huu.

Alisema kutakuwa na kujadili hotuba ya Rais aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge jipya la 11 Novemba 20, 2015.

“Mjadala kuhusu hotuba ya Rais unatarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia Januari 26 hadi Januari 28, 2016” alisema.

Alisema kwa kuwa Bunge la 11 mpaka sasa lina idadi ya Wabunge 380, ni wazi kuwa kwa siku tatu zilizotengwa, wabunge wote hawatapata nafasi ya kuchangia.

Pia, alisema katika kikao cha kwanza leo, itawasilishwa hoja ya kutengua Kanuni za Bunge ili badala kila Mbunge kuchangia kwa dakika 15 sasa iwe dakika 10 tu.

Aidha, Kipindi cha Jioni badala ya kuanza saa 11 jioni, kianze saa 10 jioni na hilo litaongeza idadi ya wachangiaji kutoka 63 ambao wangepatikana kwa utaratibu wa kawaida hadi 114 baada ya Kanuni husika kutenguliwa.

Vilevile, utaratibu utaandaliwa ili Spika aweze kuchagua wabunge watakaochangia kwa kuzingatia uwiano wa vyama na vigezo vingine. Pamoja na hayo, Bunge litajadili na kuridhia Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Alisema Bunge litajadili na kuidhinisha Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka 5, unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Mpango huo ni wa Mwaka 2016/17 – 2020/21 na itakumbukwa kuwa kila mara tunapoanza Bunge jipya Serikali huwasilisha Mpango huo bungeni ili uweze kujadiliwa na Bunge”.

Mkutano uliopita wa Novemba 2015 ulikuwa ndio wa kwanza wa Bunge jipya na mahsusi kwa ajili ya ufunguzi wa Bunge tu, hivyo kulazimika kuhamishia katika mkutano huu wa Pili, ambao kimsingi hushughulikia Taarifa za Mwaka za Kamati za Bunge.

Shughuli nyingine itakuwa ni kiapo cha uaminifu kwa wabunge 11, ambao wamechaguliwa na wengine kuteuliwa na Rais baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Kwanza wa Bunge.

Wabunge hao ni pamoja na Goodluck Mlinga wa Jimbo la Ulanga, Shaaban Shekilindi wa Lushoto, Godbless Lema wa Arusha Mjini, Omar Kigoda Jimbo la Handeni, Deogratias Ngalawa wa Ludewa na Rashid Chauchau wa Masasi.

Katika Mkutano huu, jumla ya maswali ya msingi ya kawaida 125 yanategemewa kuulizwa na kujibiwa. Alisema utaratibu wa kumuuliza Waziri Mkuu maswali ya hapo kwa papo kila Alhamisi utaendelea.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...