Na Musa Mateja/Risasi Mchanganyiko
BOSS
Lady wa Kampuni ya Endless Fame, Wema Isaac Sepetu ‘Madam’ amesababisha
timbwili la aina yake hivi karibuni, akidaiwa kuwa kwenye harakati za
kutaka kukaa karibu na staa wa Bongo Fleva anayesumbua na wimbo wa
Chekecha Cheketua, Ali Saleh ‘Kiba’, Risasi Mchanganyiko limesheheni
mchapo kamili.
NI ARUSHA
Tukio hilo la aina yake lilitokea hivi karibuni kwenye
Ukumbi wa Triple A, jijini Arusha ambapo mrembo huyo wa Tanzania mwaka
2006 alienda kwenye sherehe ya mmoja wa rafiki zake huku yeye akipewa
‘taito’ ya mgeni rasmi.
TUJIUNGE NA CHANZO
Chanzo makini kilidokeza kuwa hivi karibuni,
Kiba alikuwa na shoo maalum mjini Arusha ambayo ilihudhuriwa na mamia ya
wakazi wa jiji hilo ambapo siku hiyohiyo, Wema naye alikuwa na
marafiki zake wakisherehekea na wenyeji wake, hivyo baada ya kuisha na
kusikia Kiba yupo mjini hapo, akaona ni fursa nzuri ya kwenda kumuona.
“Wema alialikwa na rafiki yake mmoja hivi huku Arusha sasa baada ya
sherehe yao kuisha na kuambiwa Kiba anaangusha shoo, akaona bora aibuke
Triple A akamuone,” kilisema chanzo hicho.
NI KUMKOMOA DIAMOND?
Katika aya nyingine, chanzo hicho kilimwaga
ubuyu kuwa, Wema aliamua kwenda kwenye shoo hiyo ya Kiba akiamini
atamrusha roho zilipendwa wake, Nasibu Abdul ‘Diamond’ ambaye anadaiwa
kuwa haziivi na Kiba.
“Nasikia Wema alitaka kwenda ukumbini ili
ikiwezekana apige mapicha ya kumwaga na Ali Kiba ili yakivuja yamuumize
Diamond,” kilisema chanzo hicho.
TEAM KIBA WAMZUIA
Chanzo hicho kilizidi kutiririka kuwa, baadhi
ya wapambe wa Kiba (Team Kiba) waliposhtukia mchezo huo, walimzuia Wema
getini ili asiweze kuonana naye.
“Wema alikuja majira ya saa 7:45 usiku akiwa na timu yake, kufika
pale walitaka kuingia, lakini kwa hali aliyokuwa nayo wakakataa
kumruhusu. “Walijua lazima angefanya kitu kwa Kiba, kitendo ambacho wao
hawakupenda, hivyo mabaunsa wakafanya kazi yao vizuri.
“Kitendo cha kumkatalia kuingia kilisababisha kizaazaa hasa kutoka
kwa wapambe wake. Ilitokea patashika nguo kuchanika kabla ya kukubali
yaishe na kuondoka zao,” kilisema chanzo hicho.
BOFYA HAPA KUMSIKIA WEMA
Baada ya kuvutiwa waya na kusomewa
mashtaka, Wema alitiririka; “Ni kweli nilikuwa Arusha kwa shughuli
zangu, nilifikia Mount Meru ambayo pia baadaye Kiba naye alifikia na
tulionana, usiku kulikuwa na pati ya marafiki zangu, tukawa huko
tulipomaliza tukaenda kwenye shoo ya Kiba.
“Kwa kweli sikumbuki chochote maana siku hiyo nilikuwa nimelewa sana,
kwa hiyo nashindwa kusema kama unachosema nilikifanya au la, ila kesho
yake niliambiwa kuwa tulikwenda kwenye shoo ya Kiba na hatukuingia.
“Hata wakati wa kurudi hotelini kwetu sikujua nilifikaje, zaidi ya kesho
yake asubuhi niliwasikia kina Martin wakisema kwamba tulienda Triple A
lakini kweli hatukuingia kutokana na fujo zilizokuwa zimejitokeza pale
hivyo tukaamua kurudi kulala.”
No comments:
Post a Comment