HII ni habari ya kutisha! Takriban miaka mitatu imekatika tangu kifo
cha aliyekuwa staa wa Bongo Movies, Steven Kanumba huku watu wawili
wakifariki dunia kwa nyakati tofauti lakini nyuma ya pazia ya vifo vyao,
mzimu wa Kanumba unatajwa kuhusika kutokana na watu hao kutaka kuishi
mahali pa marehemu huyo, endelea kusoma Risasi Jumamosi.
SOMA TUKIO HILI LA KUSHANGAZA
Itakumbukwa kwamba, baada ya kifo
cha Kanumba, mama yake mzazi, Flora Mtegoa ndiye aliyeshika jukumu la
kusimamia mali za marehemu mtoto wake (alikuwa na haki).
Miongoni mwa mali hizo ukiachilia mbali, magari, vifaa vya kurekodia
filamu, viwanja na filamu zilizokuwa hazijalipwa, mama Kanumba
aliimiliki ofisi ya Kanumba iliyokuwa ikijulikana kwa jina la Kanumba
The Great Film iliyokuwa Sinza.Hata hivyo, hivi mapema Februari, mwaka
huu, mama Kanumba alitoa vitu kwenye ofisi hiyo kwa madai ya kushindwa
kulipa pango, hivyo ofisi ikawa wazi.
KILICHOTOKEA SASA
Habari ambazo gazeti hili ilizipata zilidai
kwamba, mpangaji mwingine aliikodisha ofisi hiyo kwa mkataba wa mwaka
mmoja lakini hivi karibuni mtu huyo amefariki dunia.Msikilize shuhuda:
“Kuna jamaa alipanga kwenye ofisi iliyokuwa ya Kanumba mara tu baada ya
mama Kanumba kuondoka vitu kwa kushindwa kulipia mkataba mpya.
“Huyo jamaa alikuwa anahusika na masuala ya ujenzi. Jamaa alilipia
kodi ya mwaka mmoja, akawalipa watu wamfanyie usafi yeye akaenda ‘saiti’
kwenye mambo yake ya ujenzi. Inadaiwa akiwa kule, kuna ‘kijiko’
kilichokuwa kinachimba kiwanja, bahati mbaya kikarudi nyuma na kumgonga,
akaanguka na kufariki dunia.”
JE, NI MZIMU WA KANUMBA?
Kifo cha mtu huyo ambaye jina lake
halikuweza kupatikana mara moja, kinaunganishwa na tukio lilitokea mwaka
juzi baada ya kifo cha Kanumba kilichotokea Aprili 7, mwaka 2012.Mara
baada ya Kanumba kufariki dunia ghafla, mwanamke mmoja alikwenda kupanga
nyumba ile aliyokuwa akiishi marehemu iliyopo Sinza, Dar, naye
alifariki dunia ghafla.
MAJIRANI WALIZUNGUMZA
Wakati wa tukio hilo, wanahabari wetu
walifika nyumbani kwa mwigizaji huyo ambapo walizungumza na majirani
wakaelezea juu ya uwepo wa tukio hilo.Walisema japo hawaamini juu ya
imani za masuala ya mzimu wa marehemu lakini kitendo cha mwanamke huyo
kufariki dunia muda mfupi baada ya Kanumba kufa kiliwafanya washtuke na
kuamini kwamba huenda ni mzimu wa Kanumba ndiyo ulichukua roho ya
mpangaji huyo.
WENGINE WALIAMINI HIVI
Hata hivyo, baadhi ya watu wengine pia
walisema yao wakidai kwamba, wanaamini kifo cha mwanamke huyo ni cha
kawaida kama ilivyo kwa vifo vingine.“Kama siku za Kanumba zilivyokuwa
zimewadia na huyo mpangaji pia siku zake zilikuwa zimefika ndiyo maana
amefariki dunia,” alisema mmoja wa majirani.
ALIVYOSEMA MZEE ALIYEKULA CHUMVI NYINGI
Mzee mmoja
aliyejitambulisha kwa jina la Mohamed Sumali (76), mkazi wa
Mabibo-Relini, Dar akizungumza na gazeti hili kuhusu mazingira ya vifo
hivyo, alisema:“Ipo mizimu ya hivyo. Mtu akifa, wa kwanza kuhamia kwenye
nyumba aliyokuwa akiishi marehemu naye anakufa. Lakini si kwamba nyumba
ndiyo ina mizimu. Kama hivyo vifo vimetokea kweli basi na mzimu wa
Kanumba umeshaondoka.”
MAMA KANUMBA AZUNGUMZA
Baada ya kuzipata habari hizo, mwanahabari
wetu alimvutia waya mama Kanumba kutaka kujua kama anajua lolote juu ya
marehemu mtoto wake kuacha mzimu ambao unahusishwa na vifo hivyo ambapo
alikiri kusikia taarifa za kifo cha jamaa aliyepanga kwenye ofisi za
Kanumba lakini akasema hata yeye hajui sababu za kifo chake.
“Hata mimi nimesikia, lakini sielewi chochote kuhusiana na mtu huyo
kufariki dunia. Imenishtua kwa kweli maana si unakumbuka hata kule
alikopanga (Kanumba) mwanzoni nako aliyepanga ile nyumba naye alifariki?
Sijui hata ni kwa nini?” alihoji mama Kanumba kwa sauti iliyoashiria
kushangaa sana.
No comments:
Post a Comment