Friday, June 20, 2014

MUME WA FLORA MBASHA YUPO NJE KWA DHAMANAShetani mbaya! Wakati jana mumewe Emmanuel Mbasha (32) akipandishwa kizimbani kwa mara ya pili kwa soo la ubakaji wa shemejiye, mwimba Injili kinara Bongo, Flora Mbasha (31) amepitia katika hatua tatu za aibu, Ijumaa lina ripoti kamili.
Mwimba Injili kinara Bongo, Flora Mbasha akiwa na mumewe Emmanuel Mbasha.

Mbasha ambaye naye ni mwimba Injili na mfanyabiashara alitarajiwa kupandishwa kizimbani jana kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Wilaya ya Ilala, Dar akitokea mahabusu Keko akikabiliwa na mashtaka mawili ya ubakaji wa shemejiye mwenye umri wa miaka 17.

Habari kutoka kwa mtu wa karibu wa Flora ambaye alihama nyumbani na kwenda kuishi hotelini maeneo ya Sinza, Dar, kitendo hicho kilimuingiza staa huyo kwenye hatua ya tatu ya aibu na kujikuta akiwa katika masikitiko makubwa.

AIBU YA KWANZA
Kwa mujibu wa mtu huyo wa karibu aliyeomba hifadhi ya jina, aibu ya kwanza inayomuuma Flora ni ile ya ndoa yake kuingia kwenye gogoro kisha kudaiwa kutengana na mumewe kinyume na kile anachokihubiri kupitia nyimbo zake zinazopendwa na wengi ndani na nje ya Bongo.

Binti wa miaka 17 anayedaiwa kubakwa na mume wa mwimbaji wa nyimbo za injili Bongo Flora Mbasha, Emmanuel Mbasha.

“Unajua lile neno la ‘mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake, bali mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe’ (Mithali 14:1) linamfanya awe na aibu mbele za watu.
“Unaambiwa kanisani (anasali Kanisa la Ufufuo na Uzima la Mchungaji Josephat Gwajima kwenye Viwanja vya Tanganyika Packers, Dar) anaona aibu hasa kwa waumini wenzake.

“Flora amedumu na Ima (Mbasha) kwenye ndoa kwa miaka 12 hivyo kutokea kwa kilichotokea ni aibu kwani tayari walikuwa wamekomaa tofauti na walipoona wakiwa na umri mdogo.
“Hebu fikiria, mtoto amekuwa mkubwa, anaposikia mama ana matatizo na baba si ni aibu jamani? Cha msingi tuwaombee wamalize matatizo yao, inaweza kusaidia kuifuta aibu hiyo kwani imeandikwa ‘Ndoa na iheshimiwe na watu wote...’ ( Waebrania 13 : 4 -),” alisema mnyetishaji wetu akisisitiza kuwa akitajwa gazetini ataonekana mvujishaji wa mambo ya siri ya wanandoa hao.

AIBU YA PILI
Chanzo hicho kiliendelea kutiririka kuwa aibu ya pili inayomkabili Flora ni skendo ya yeye kudaiwa kuhamishia makazi kwa mchungaji wake, Gwajima.

Katika aibu hiyo, mumewe alinukuliwa na gazeti mama la hili, Uwazi akimlalamikia mchungaji huyo amwachie mkewe kwani yeye ndiye alisababisha sakarakasi zote hizo za ndoa yake.
Ilidaiwa kuwa kwa mke wa mtu achilia mbali mhubiri kwa njia ya nyimbo, kitendo cha kukumbwa na skendo nayo ni aibu pia.
Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Josephat Gwajima.

“Kwa mtumishi kutajwa kwenye jambo kama hilo lisilo na mrengo wa kupendeza masikioni mwa watu, ni aibu kuu,” kilidai chanzo hicho.

AIBU KUU YA TATU
Ilisemekana kuwa achilia mbali ndoa, mambo ya mchepuko lakini aibu kuu ya tatu kwa Flora, ni kashfa ya ubakaji wa shemejiye inayomkabili mumewe Mbasha.
“Unajua usifikirie kwamba mume akipata aibu mke anaweza kuikwepa. Hawezi kwa sababu ‘wanazungumza lugha moja’ (yaani ni mwili mmoja). Ona sasa mume anapandishwa kizimbani kwa ubakaji.
Mwimbaji wa nyimbo za injili Bongo Flora Mbasha

“Pia usifikiri watu watasema kashfa ni ya Ima peke yake. Kwanza hata kutamka watu wanasema mume wa Flora. Ikumbukwe aibu ya mume ni ya mke pia. Ni vigumu mno kwa Flora kusema aibu ni ya mumewe pekee,” alitiririka mto habari huyo.

FAMILIA ZATOFAUTIANA
Wakati hayo yakiendelea, habari zinadai kuwa familia za pande zote zinatofautiana huku kila moja ikilaumu nyingine.

Ilidaiwa kuwa upande wa Mbasha unamlalamikia mama wa Flora kuwa anamuunga mkono mwanaye badala ya kusaidia kutuliza hali ya hewa.

Ilielezwa kuwa upande wa Flora wao wanamlaumu Mbasha kwa madai kuwa chanzo cha yote ni mgawanyo wa mali hasa baada ya kuona kuwa hakuna tena ndoa.
FLORA ANASEMAJE?
Akizungumza na Ijumaa juzi kwa njia ya simu, Flora alitoa la moyoni: “Kweli naumia sana tena sana. Kwa sasa kesi ipo mahakamani, siwezi kuizungumzia lakini ndiyo hivyo. Siyo siri nateseka sana.”
Mbasha anadaiwa kumbaka ndugu wa Flora ambaye ni yatima kati ya Mei 23 na 25, mwaka huu ambapo kesi yake inaendelea kuunguruma baada ya kukaa mahabusu ya Keko kwa siku kadhaa ambapo sheria ndiyo itakayoanika siri zote juu ya sakata hilo.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...