Wednesday, May 21, 2014

MASWALI 5 KIFO CHA MENEJA EWURA

JAMBO limezua jambo! Maswali matano ya msingi yameibuka kufuatia kifo cha aliyekuwa Meneja Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza kilichotokea hotelini katika mazingira ya kutatanisha muda mfupi baada ya kuwasili jijini Dar akitoka Dodoma ambako alihojiwa na Kamati ya Bunge ya Bajeti, Amani limeyanasa.


Meneja Biashara ya Petroli wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Julius Gashaza enzi za uhai wake.

Habari za kiintelijensia zilidai kwamba marehemu Gashaza ndiye aliyekuwa na majukumu ya kupanga bei za mafuta kila mwezi, alikuwa mjini Dodoma kwa siku mbili, Ijumaa na Jumamosi iliyopita kuhusu kuweka wazi kiwango cha mafuta kinachoingizwa nchini, mgawo wa fedha unaotolewa na Ewura kwenda kuhudumia umeme katika vijiji (Rea) na fedha za mfuko wa barabara.

Jumapili iliyopita, meneja huyo alikutwa amekufa kwenye Hoteli ya Mwanga Lodge iliyopo Yombo-Vituka, wilayani Temeke jijini Dar na kusadikiwa kuwa alijinyonga kwa tai kwenye nondo za dirisha la chooni katika chumba Na. 113.Mwandishi wetu alifuatilia kwa karibu tukio hilo la kusikitisha na kubaini mambo kadha wa kadha.


Hii ni Hoteli aliyodaiwa kulala Meneja huyo wa Ewura.

NYUMBANI KWA MAREHEMU

Jumatatu iliyopita mwandishi wetu alianza kwa kufika nyumbani kwa marahemu lakini hakuna aliyekuwa tayari kutoa ushirikiano mwa mwanahabari wetu.
Baada ya hapo, mwandishi wetu alikwenda kwenye hoteli hiyo ambako ndiko alikopata maswali hayo matano yenye kuumiza kichwa.

Mhudumu mmoja wa hoteli hiyo ambaye aliomba hifadhi ya jina, alisimulia mazingira yote ya kifo cha meneja huyo, alisema:

“Usiku wa kuamkia siku ya tukio, marehemu alikuja hapa hotelini akiwa ameongozana na watu wanne. Wanawake wawili na wanaume wawili akiwemo yeye marehemu.
“Nilisikia wale wanawake mmoja alikuwa mke wa marehemu, mwingine mke wa rafiki wa marehemu. Wakachukua chumba, wakaingia ndani wote.


Chumba alichodaiwa kulala Meneja wa Ewura.

“Baada ya muda, walitoka watatu. Mke wa marehemu, rafiki yake na mke wa rafiki yake.
“Kwa hiyo inamaanisha ndani ya chumba alibaki marehemu, maana si waliingia wanne na wametoka watatu!

“Tulilala! Asubuhi alikuja yule rafiki wa marehemu akasema anaomba kusaidiwa kumwona marehemu maana amekwenda kugonga lakini hajaamka na mlango umefungwa.

“Tulikwenda wote, kufika kweli mlango ulifungwa. Ikabidi tuchukue funguo nyingine kufungua.
“Hakuwemo chumbani na kwenye kitanda palionesha alama ya mtu kukaa tu si kulala kwani palitengeneza duara alipokaa.

“Kwenda chooni ndipo tukamkuta amekufa kwa kujinyonga kwa tai.”
Alisema kwamba ndipo taratibu za kuwaita polisi zilifuata.


Hiki ni choo alichokutwa meneja huyo.

MANENOMANENO YA WATU
Kufuatia hali hiyo, kumeibuka maneno mengi. Wengine wanadai marehemu alinyongwa na wabaya wake, wapo wanaosema alijinyonga kufuatia uchungu wa kutishiwa maisha na wabaya wake kuhusu kazi.

Wengine wakaenda mbele zaidi kwa kudai kuwa wanyongaji hao walimfuatilia kwa muda mrefu siku ya tukio.

MASWALI MATANO
Swali la kwanza: Kama kweli marehemu alinyongwa ni kwa nini mlango ulikutwa umefungwa kwa ndani? Je, mnyongaji alitokaje baada ya kutekeleza mauaji hayo?


Meneja Gashanza (mwenye kofia) akiwa kazini enzi za uhai wake.

Swali la pili: Kama kweli marehemu alinyongwa, kwa nini kitandani kulikutwa na alama ya mtu kukaa tu na kusiwepo kwa dalili za mapambano au purukushani?

Swali na tatu: Kama kweli alijinyonga mwenyewe ni kwa nini iwe kipindi hiki ambacho inadaiwa alipokea vitisho kutoka kwa wabaya wake kwamba atauawa?
Swali la nne: Uamuzi wa kuchukua chumba kwenye hoteli hiyo ulitoka kwa nani? Marehemu mwenyewe au? Kama alishauriwa, aliyemshauri ana cha kujibu?

Swali la tano: Kama kulikuwa na matatizo ya kikazi kama ilivyodaiwa, basi Mkurugenzi Mstaafu wa Ewura, Haruna Masebu atakuwa anayajua hivyo angeweza kusaidia kuyasema.

Swali lingine ambalo lingeweza kuongeza idadi ni juu ya uwezekano wa kuingizwa kwa funguo nje wakati ya ndani ilizungushwa lakini imebainika kwamba baada ya funguo kufungwa na mlango kuwa ‘lokdi’, funguo hiyo huwa ‘luzi’ tena hivyo mwenye funguo nje anaweza kuisukuma na kuingiza nyingine.

ALIWAHI KUSIAIDIA GLOBAL KUPATA KIBALI CHA KAMPUNI YA KUINGIZA MAFUTA
Marehemu atakumbukwa na uongozi wa Kampuni ya Global Publishers kwani aliwahi kuisaidia kupata kibali cha kuingiza mafuta nchini bila mizengwe wala kutaka shukrani.

Kwa mujibu wa Meneja wa Masoko wa Global Publishers na Kampuni ya Shigongo Oil, Benjamin Mwanambuu, marehemu alikuwa akifanya kazi yake kwa kufuata utaratibu na sheria.

“Kwa kweli nilimfahamu marehumu Gashaza wakati wa kutafuta kibali cha kungizia mafuta katika Kampuni ya Shigongo Oil. Alikuwa mtu mwema sana, asiyetaka njia za uchochoro. Kila hatua ilikuwa ya haki na uwazi,” aliema Mwanambuu.

Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Temeke, Engelbert Kiondo alikiri kutokea kwa tukio hilio akisema ameshaingiza ‘vijana’ wake kuchunguza ukweli wa tukio hilo la kujinyonga au kunyongwa.

Mwili wa marehemu Gashaza uliagwa juzi nyumbani kwake, Yombo-Vituka, Dar na kusafirishwa Ngara, Kagera kwa mazishi. Mungu ailaze pema peponi roho ya marehemu. Amina.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...