Monday, March 24, 2014

JB, TIMU YA EATV NIRVANA WAUVAMIA MJI WA LUSHOTO

Alfajiri ya Machi 6, timu ya Nirvana, Grow, pamoja na JB walielekea soko kuu la Lushoto ambapo walikutana na wakulima ili kusikia hadithi zao za mafanikio pamoja na changamoto. Nirvana na Kampeni ya GROW wanahamasisha lifestyle njema! Lakini tunavyokula vyakula bora, vyenye virutubisho tunajua vinatoka wapi!

Akizungumza kutoka katika sehemu yake ya biashara, Zinira Ally (kushoto aliyekaa) alishuhudia jinsi ambavyo anasomesha watoto na kulisha familia yake kwa pesa inayotokana na biashara yake ya uuzaji wa mbogamboga na matunda.

"Nzenze"... Salaam na wapenzi wa filamu zikiendelea.

JB, Lotus na Deo wakitizama mazao mbalimbali katika soko kuu la Lushoto.

Veronica Joseph ambaye ni muuzaji wa mboga mboga sokoni Lushoto anasema angependa kuona mabadiliko katika miundombinu ya soko ili kulinda ubora wa mazao, “soko halina ubora, watu wananunua vyakula hivi hivi kwa bei ghali kwenye supermarket kwa sababu ya ubora, sie tunauza tu bora tunauza, tunaogopa vyakula kuoza, tungekuwa na mafriji ya kuhifadhia mboga mboga na sisi tungeweza kuuza bei sawa na supermarket.”Akiendelea kutaja changamoto, Veronica ambaye ni mama wa watoto wawili, alionyesha kusikitishwa kwake na maisha duni wanayoishi wakulima, “mkulima analima chakula ambacho wengine wanakula hadi kutupa lakini yeye hawezi hata kula mlo kamili kwa sababu kipato anachopata ni kidogo” Veronica anaamini kama, “masoko yangeboreshwa, tungeuza bidhaa kwa bei nzuri ili na sisi tusomeshe watoto wetu na kujikimu kimaisha.”

Uvuvi unalipa..??

Ugeni umefika katika meza ya Asha Paulo (Kushoto) na Shakira Rashid (kulia), hawa ni wauzaji wa samaki katika soko kuu la Lushoto. Asha na Shakira wanaelezea jinsi ambavyo mikopo kwa wakulima na wafugaji isivyokuwa rafiki. Asha anasema, “mikopo ina masharti makali sana, sidhani kama inamlenga mtu wa hali ya chini kwani makato ni makubwa sana.”

Watangazaji wa kipindi cha Nirvana, Lotus na Deo walishangaa kuona apple zinazolimwa Tanzania. Kisado kimoja ambacho kwa wastani kina ma-apple ishirini (20) kinauzwa kwa Tshs. 2000 wakati kwa wastani apple moja jijini Dar es salaam linauzwa hadi Tshs. 1000. Baada ya kuonja, Deo anashangaa kuona ladha haipishani sana na ile ya matunda hayo yanayoagizwa kutoka nje. Ukweli ni kwamba miundo mbinu, technolojia, sera na mifumo iliyopo imewaangusha wakulima hapa Tanzania! Fikiria kwamba ni rahisi na kuna faida zaidi kusafirisha apple kutoka nje ya nchi kuliko hapa hapa Lushoto Tanzania!

Paulina Isaya (mwenye nguo nyeusi), muuzaji wa matunda apple katika soko kuu la Lushoto anasema, “kama wakulima wangepewa mafunzo sahihi, mbegu bora na kuhakikishiwa masoko, hakika matunda hayo yangekuwa na kiwango kama hayo yanayoagizwa kutoka nje”.

Taswira ya soko kuu la Lushoto kwa nje.

JB akiangalia kabichi zilizowekwa pembezoni mwa barabara. (Haikujulikana mara moja kama zilikuwa zinasubiri kusafirishwa ama la)

Katika kuelekea siku ya wanawake duniani,iliyoadhimishwa Duniani kote mnamo Machi 5, kampeni ya Grow ikiongozana na mmoja wa mabalozi wake muigizaji Jacob Stephen ‘JB’ iliungana na kipindi cha EATV Nirvana na kuutembelea mji wa Lushoto,Jijini Tanga.

Kampeni ya GROW, inayoendeshwa na Oxfam, inahamasisha mabadiliko kwenye mifumo iliyopo ili iwafanufaishe wakulima na wafugaji/wavuvi wadogo wadogo hususani wanawake wawe na maisha endelevu! Inawasherekea kwa mchango wao mkubwa wa kulisha nchi huku wakipambana na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa masoko, pembejeo na miundo mbinu. Katika harakati hizi, mnamo mwaka 2011, shindano la "Mama Shujaa wa Chakula " lilizinduliwa rasmi hapa nchini. Lengo la tuzo hii ni kutambua mchango wa wanawake hasa waishio vijijini.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...