Monday, November 4, 2013

VURUGU ZA BUNGENI SASA KUPATIWA DAWA MBADALA


Spika wa Bunge, Anne Makinda.

UTAMADUNI mbovu ulioanza kujitokeza kwa baadhi ya wabunge kuonesha kukosa nidhamu, umeandaliwa kanuni mpya ambazo pamoja na mambo mengine, zitadhibiti matukio hayo na kuadhibu wahusika.
Taarifa zilizofikia gazeti hili zimeeleza kuwa Rasimu ya Mwongozo wa Kanuni za Maadili ya Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyotoka mwishoni mwa wiki, imebainisha namna Bunge litakavyodhibiti matukio hayo.

Udhibiti Kwa mujibu wa mtoa habari wetu kutoka miongoni mwa wabunge, rasimu hiyo imewabana wabunge kutofanya vurugu kwa kuzomea au vinginevyo kunakoweza kusababisha shughuli za Bunge kusitishwa.

Ili kudhibiti kutokea vurugu bungeni, mtoa habari wetu ameeleza kuwa Spika amepewa madaraka ya kuahirisha shughuli za Bunge bila hoja yoyote kutolewa ili kupisha muda wa kudhibiti vurugu hizo.
Ingawa rasimu hiyo haikutamka adhabu kwa wabunge watakaokutwa na hatia, mtoa habari wetu amesema Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, imepewa nguvu ya kujadili watuhumiwa na kutoa ushauri kwa Spika kuhusu hatua zaidi.
Kuwepo kwa rasimu hiyo kumetokana na mapendekezo ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ambayo mwaka jana ilipendekeza wabunge watungiwe kanuni zinahohusu maadili.

Katika mapendekezo ya kamati hiyo, waliomba uwepo wa kanuni zitakazoweka viwango kwa mienendo ya wabunge pale watakapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kibunge wawapo nje na ndani ya eneo la Bunge.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Mlalo, Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi (CCM), alisema katika taarifa ya mapendekezo hayo kuwa uzoefu unaonesha baadhi ya mabunge katika Jumuiya ya Madola, tayari wana kanuni za maadili na mwenendo wa wabunge.

Alisema pia kuna utafiti umefanyika ulioonesha kwa kiasi fulani kuwepo kwa kanuni hizo, kunaongeza imani ya wananchi kwa mabunge yao.

Hivi sasa maadili ya wabunge yanasimamiwa na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, ambayo imeelezwa kwamba kwa madhumuni ya usimamizi bora wa maadili ya wabunge, sheria hiyo haikidhi mahitaji kama ikiachwa itumike peke yake.
Kamati hiyo ilieleza kuwa kuwepo kwa mwongozo wa kanuni za maadili kwa wabunge, kutawafanya wabunge hao kuonesha viwango vya juu vya maadili, katika kutekeleza majukumu yao kwa umma hususani wanapokuwa wakiisimamia Serikali.
Hata hivyo, mtoa habari wetu alisema kanuni hizo hazitahusisha maisha binafsi ya mbunge, familia yake au pale anapotoa maoni yake ya kisiasa kwa kuzingatia kuwa yeye ni mwanachama wa chama cha siasa.

Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, kanuni hizo pia hazitawahusu wabunge ambao ni mawaziri wanapotekeleza majukumu yao.
Chanzo kingine cha habari kimebainisha kuwa huenda rasimu hiyo ikajadiliwa wiki hii, kama Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kupanga shughuli za Bunge, ikiamua hivyo.

“Rasimu imetoka ni kweli na inaweza kujadiliwa bungeni iwapo Kamati ya Uongozi itaona inafaa kwenye bunge hili, wabunge wanachopaswa kufanya ni kutoa maoni na mapendekezo yao au kuongeza jambo, lakini hawawezi kukataa kuipitisha. “Mwongozo huo ni mzuri … wabunge wanaofuata maadili watafurahi uwepo wa kanuni hizo za wabunge, lakini kwa wale wasiofuata maadili wanaweza kuona ni kero kwako, lakini rasimu ni nzuri,” alieleza mtoa habari huyo.

CHANZO NI HABARI LEO

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...