Wednesday, March 6, 2013

DK MWINYI AMTEMBELEA ABSALOM KIBANDA MUHIMBILI




Waziri wa Afya, Dk Hussein Mwinyi leo asubuhi amemtembelea kumjulia hali Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda aliyelazwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.


Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa New Habari ambao pia wanachapisha magazeti ya michezo ya Dimba na Bingwa, usiku wa kuamkia leo alishambuliwa na watu wasiojulikana.


Ingawa watu hao wanaaminika kuwa ni majambazi, lakini imeelezwa hawakupora kitu chochote ndani ya gari lake, mfano simu na kompyuta mpakato (laptop).




Kibanda aliumizwa na watu hao ambao walimvamia wakati akiingia nyumbani kwake Mbezi jijini Dar es Salaam. Wakavunja kioo cha gari na kumtoa nje kabla ya kuanza kusmhambulia ikiwa ni pamoja na kumkata mapanga kichwani na kulijeruhi vibaya jicho lake, pia imeelezwa wamemyofoa kucha.


Kibanda ameumizwa vibaya jichoni, tayari madaktari wameonyesha hofu ya jicho hilo kurudi katika hali yake ya kawaida na uwezo wa kuona tena. Hata hivyo wamekuwa wakiendelea na juhudi.

Kabla ya kurejea New Habari, Kibanda alikuwa Mhariri Mtendaji wa Free Media wanaochapisha gazeti la Tanzania Daima na Sayari, kabla ya hapo alikuwa Mwananchi Communications.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...