Thursday, February 28, 2013

JOHN MNYIKA.....NCHI IMEINGIA TENA KWENYE MGAWO WA UMEME, SERIKALI IELEZE WANANCHI UKWELI NA HATUA KUHUSU UDHAIFU KWENYE UTEKELEZAJI WA MPANGO WA DHARURA



Nchi imeingia tena katika mgawo wa umeme kinyume na ahadi iliyotolewa na Waziri wa Nishati na Madini Prof Sospeter Muhongo bungeni tarehe 28 Julai 2012.


Hali hiyo ni matokeo ya Serikali kutozingatia tahadhari niliyoitoa bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani na kwa nyakati mbalimbali kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini juu ya hali tete iliyotarajiwa kuwepo na hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme.


Ikiwa ni sehemu ya wajibu wa kibunge wa kuisimamia Serikali nawataka viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuacha kuficha hali ya mambo na kuwaeleza ukweli wananchi kuhusu mgawo wa umeme uliojitokeza na hatua za haraka zinazochukuliwa kurekebisha hali hiyo.


Iwapo Wizara na TANESCO hawatatoa matangazo ya ukweli kwa wananchi, kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini nitaeleza vyanzo vya mgawo wa umeme uliojitokeza ili hatua ziweze kuchukuliwa wakati huu ambapo wajumbe wa kamati ya nishati na madini wenye wajibu wa kuisimamia Serikali kwa niaba ya Bunge katika sekta hizo nyeti hawajateuliwa.




Aidha, pamoja na kutoa maelezo kuhusu mgawo wa umeme, Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO watumie nafasi hiyo pia kueleza hatua zilizochukuliwa kuhusu ukaguzi wa awamu ya pili kuhusu tuhuma za ufisadi katika ununuzi wa vifaa na uzalishaji wa umeme wa dharura ikiwemo kuhusu mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme.


Ikumbukwe kwamba mwanzoni mwezi Agosti 2012 Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT) iliunda timu ya wakaguzi kufanya ukaguzi maalum wa hesabu za Shirika la Umeme (TANESCO) kufuatia tuhuma za ubadhirifu wa fedha za umma zilitajwa bungeni na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini katika maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani tarehe 27 Julai 2012 na Waziri wa Nishati na Madini wakati wa majumuisho ya hoja ya Serikali tarehe 28 Julai 2012.


Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO waeleze pia hatua iliyofikiwa kuhusu uchunguzi mwingine uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kuanzia mwezi Agosti 2012 wa mchakato wa ununuzi wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme wa dharura kutokana na tuhuma mbalimbali zilizotolewa bungeni kuhusu ununuzi huo suala ambalo Kambi Rasmi ya Upinzani ilitaka pia tarehe 27 Julai 2012 liundiwe kamati teule ya Bunge ili uchunguzi wa kina uweze kufanyika.


Wenu katika uwakilishi wa wananchi,


John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati na Madini

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...