Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA)
limemfungulia Msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kwa
jina la Nay wa Mitego kuendelea na shughuli za Sanaa baada ya kuwa ametekeleza
adhabu (maagizo) zote alizopewa kama masharti ya kumfungulia.
Aidha, BASATA kama mlezi wa wasanii
linamfungulia kufuatia yeye mwenyewe (Nay wa Mitego) kujutia na kukiri kwamba
amejifunza na yuko tayari kubadilika na kwamba hatarudia makosa aliyoyafanya.
Hata hivyo, pamoja na kumfungulia
kuendelea na shughuli za Sanaa Baraza linamweka kwenye uangalizi maalum msanii
huyo kama sehemu ya kuhakikisha anaendesha shughuli za Sanaa kwa kuzingatia
sheria, kanuni na taratibu sambamba na kuzingatia maadili katika kazi zake.
Itakumbukwa kwamba mnamo tarehe
27/07/2016 Baraza lilimfungia Msanii Nay wa Mitego kwa kipindi kisichojulikana
na kumtaka kutekeleza maagizo yafuatayo:
1. Kuhakikisha
amesajiliwa na kuwa na kibali cha kuendesha
shughuli za Sanaa
2. Kulipa
faini ya shilingi milioni moja (1,000,000/-)
3. Kuomba
radhi watanzania kupitia mkutano na waandishi wa habari na kwenye akaunti zake
za mitandao ya kijamii
4. Kuufanyia
marekebisho wimbo wa ‘Pale Kati’ ili
ubebe maudhui yenye maadili.
Msanii Nay wa Mitego ametekeleza
adhabu zote tajwa hapo juu. Leo hii tunamkabidhi rasmi cheti chake cha usajili
na kibali cha BASATA.
Hata hivyo, pamoja na kuleta
marekebisho mara mbili ya wimbo wa ‘Pale Kati’ Baraza bado halijaridhishwa na
marekebisho hayo hivyo linaendelea kuufungia wimbo huu hadi hapo
litakapojiridhisha umekidhi vigezo vya kimaadili.
Katika kikao na Msanii Nay wa Mitego
cha kufanya tathimini ya utekelezaji wa adhabu yake kilichofanyika tarehe
12/08/2016 Ofisi za BASATA ameagizwa kuendelea kuufanyia marekebisho wimbo wake
huo kama bado anaona anauhitaji.
Baraza linatoa maelekezo kwa vyombo
vya habari na watanzania kwa ujumla kuacha kuucheza wimbo huo hadi hapo
itakapoelekezwa vinginevyo. Hatua na adhabu za kisheria zitachukuliwa kwa
chombo chochote cha habari kitakachokiuka agizo hili.
Aidha, katika kikao hicho cha
tathimini ilibainika kwamba Msanii Nay wa Mitego kwa taarifa potofu alizopewa
alipanda Jukwaani kwenye tamasha la Mwendo Kasi la tarehe 30/07/2016 akiwa
katika adhabu.
Kwa kosa hili ameandika barua ya
kuomba radhi na Baraza linafikiria hatua za kuchukua kwa waandaaji wa tamasha
hili.
Baraza linatoa wito kwa wasanii
kuendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji shughuli za Sanaa
sambamba na kuhakikisha wanazingatia maadili katika kila kazi wanazobuni ili
kuepuka matatizo yasiyo ya lazima ambayo yanaathiri kazi zao kwa kiasi kikubwa
sana.
SANAA NI KAZI TUIKUZE, TUILINDE NA
KUITHAMINI
Godfrey L. Mngereza
KATIBU MTENDAJI, BASATA