Monday, February 25, 2013

TIMBULO KAKAMATWA BURUNDI NA MADAWA YA KULEVYA?





Kuna tetesi kuwa msanii wa Bongo flava maarufu kwa jina la Timbulo, ambaye amepata umaarufu mkubwa kutokana na umahiri wa kuimba katika nyimbo zake kadhaa kama Domo Langu, Waleo Wakesho, Samson na Delilah, amekamatwa mjini Bujumbura kwa tuhuma za kukutwa na madawa ya kulevya. Timbulo alikuwa huko katika kufanya mipango ya kufanya maonyesho kadhaa nchini Burundi mwezi April mwaka huu

BREAKING NEWS ..SERIKALI YABATILISHA UCHAGUZI WA TFF


Serikali kwa kupitia waziri wa habari ,vijana ,michezo na utamaduni Dk.Fennela Mukangara imeingilia kati na kubadilisha mchakato wote wa uchaguzi wa TFF kwa madai ya kuwa katiba iliyotumika si halali na kutaka uchaguzi huo ufanyike upya kwa kupitia katiba mwaka 2006 na kwamba kwa kutumia ibara ya 10 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumuondoa msajili wa vyama na vilabu michezo.

SERIKALI YA AWAMU YA NNE YAONGOZA KWA KUKOPA



TAASISI isiyo ya kiserikali ina yojishughulisha na masuala ya Madeni ya Taifa na Maendeleo (TCDD), imesema Serikali ya Tanzania ndiyo inaongoza kwa kukopa zaidi, ikieleza kuwa kati ya mwaka 2008 hadi mwaka 2011, imekopa kiasi cha Sh15trilioni na kufanya deni la taifa kufikia Sh21trilioni.

Rais Kikwete aliingia madarakani mwaka 2005, baada ya rais aliye mtangulia, Benjamin Mkapa kumaliza kipindi chake cha uongozi wa miaka 10 kilichoanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2005.

TCDD imebainisha kuwa Serikali inakopa fedha hizo kutoka Benki Kuu (BoT), Benki za Biashara, Kampuni za Bima na Mashirika ya Hifadhi za Jamii. Pia inakopa katika taasisi za kimataifa ikiwamo, Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo Afrika (ADB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Katika maelezo yake, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo Hebron Mwakagenda, alisema kuwa kite ndo cha Serikali kukopa fedha kwa ajili ya matumizi yasiyo muhimu pamoja na kuwalipa watumishi wake mishahara, ndiyo sababu ya kukua kwa deni hilo la taifa.

“Serikali ya awamu ya nne imekopa kwa kiwango kikubwa, kwani tangu iingie madarakani imeshakopa Sh15trilioni, sasa sijui mpaka inamaliza muda wake itakuwa imekopa kiasi gani?” alisema Mwakagenda akihoji na kuongeza;

“Hata kama kukopa ni kuzuri basi tukope na fedha tuzifanyie mambo ya maana hasa katika maendeleo, tukope tu pale inapokuwa lazima kufanya hivyo.”

TCDD imeeleza kwamba hali hiyo ni hatari, hasa ikizingatiwa kuwa miaka kadhaa iliyopita, Tanzania kupitia Mpango wa Nchi Maskini zenye Madeni Makubwa (HIPC), ilifutiwa kiasi kikubwa cha madeni, lakini sasa imeanza kukopa tena na deni kukua kwa kasi.

Taasisi hiyo pia imesema kitendo hicho kimechangia kuporomoka kwa uchumi wa taifa kunakosababishwa na riba kubwa za mikopo hiyo, ambapo kulingana na idadi ya Watanzania ukigawanya deni hilo kwa wote, inaonyesha kuwa kila Mtanzania anadaiwa wastani wa Sh450,000.

Mwakagenda, ambaye taasisi yake inafanya kazi ya kuishauri Serikali katika suala zima la deni la taifa na maendeleo, alisema hadi kufikia Oktoba mwaka jana, deni la nje lilikuwa Sh15.9 trilioni.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliyoitoa bungeni mjini Dodoma mwaka jana, taifa linapoteza Sh3 trilioni katika ukwepaji wa kodi na ubadhirifu, huku akishauri kuwa mambo mawili yakifanyiwa kazi deni hilo litapungua au kumalizika kabisa.

“Deni linakuwa kwa kiasi kikubwa na tunakopa katika mabenki ya biashara, ambayo riba yake ni kubwa, fedha nyingi zinazokopwa hutumika kulipa mishahara,” alisema Mwakagenda.

Alifafanua kwamba mwaka 2007 hadi 2008 deni la taifa lilikuwa Sh6.4 trilioni na kwamba, kuanzia mwaka 2007 hadi 2011 deni hilo limeongezeka hadi Sh21 trilioni.

*MECHI YA YANGA, AZAM YAINGIZA SH.MIL 240/-




Mechi namba 120 ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa jana (Februari 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa Yanga kuibuka ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam imeingiza sh. 239,686,000.



Watazamaji 39,315 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 58,794,927.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 36,562,271.19.



Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 33,315 na kuingiza sh. 165,655,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 485 na kuingiza sh. 9,700,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 29,895,725.82, tiketi sh. 3,183,890, gharama za mechi sh. 17,937,435.49, Kamati ya Ligi sh. 17,937,435.49, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 8,968,717.75 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 6,975,669.36.

Saturday, February 23, 2013

CHADEMA: Kawambwa amebakiza siku kumi



Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika

KAULI ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa kwamba hawezi kujiuzulu, imeamsha hasira ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambacho kimesisitiza kwamba maandamano ya kumng’oa yako pale pale na sasa amebakiza siku kumi.


Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika wakati alipotakiwa kueleza msimamo wa chama chao, hasa baada ya kauli ya Waziri Kawambwa jana kwamba hawezi kujiuzulu.


Akizungumza na gazeti hili jana, Mnyika ambaye ni Mbunge wa Ubungo, alisema kauli aliyoitoa Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe kwamba anampa siku 14 Waziri Kawambwa ajiuzulu, vinginevyo atang’olewa kwa maandamano bado ipo pale pale.


Alisema majibu ya Waziri Kawambwa yameonesha dharau kwa Watanzania, hasa walalahoi ambao ndio watoto wao wengi wamepata ziro katika mitihani yao ya kidato cha nne.


“CHADEMA tunaendelea kusisitiza kwamba Waziri Kawambwa ang’oke, awajibike, ameshindwa kazi na hili tunamaanisha,” alisisitiza Mnyika.


Alisema CHADEMA inaangalia namna ya kuitisha maandamano hayo kwa kuwashirikisha vijana waliofeli kwani wanaamini wamehujumiwa.


Mnyika aliwataka Watanzania na wengine wenye uchungu na udhaifu wa elimu ya Tanzania, hasa wazazi wajitokeze kwani fedha walizowekeza kwa watoto wao kwa ajili ya elimu, zimeteketea.


Wakati akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Furahisha, Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, ikiwa ni ufunguzi wa Baraza la Viongozi wa CHADEMA, Kanda ya Ziwa Magharibi, Mbowe alitoa siku 14 kwa Dk. Kawambwa na Naibu wake, Philipo Mulugo, kuhakikisha wamejiuzulu nyadhifa zao.



Mbowe ambaye aliongoza maandamano makubwa ya magari na pikipiki kuelekea uwanjani hapo, alisema Kawambwa, naibu wake, Mulugo, pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, wameshindwa kuiongoza sekta hiyo muhimu, ndiyo maana kwa sasa wanafunzi wanaishia kuandika matusi na kupata sifuri katika mitihani.


Alisema waziri huyo lazima ajiuzulu nafasi hiyo, kwani taifa ameliingiza pabaya na kuanza kuzalisha maelfu ya watoto wa maskini kumaliza elimu zao za msingi na sekondari wakiwa hawajui kusoma na kuandika.


Alisema hili ni janga la kitaifa, hivyo lazima Kawambwa aondoke ndani ya wiki mbili, vinginevyo CHADEMA itaitisha maandamano makubwa nchi nzima kushinikiza kiongozi huyo ang’oke madarakani.


“Kwa vile Kawambwa ameshindwa kuisimamia vema sekta hii ya elimu, na kwa vile watoto wetu wengi wanafeli na kuishia kuandika matusi kwenye mitihani yao, CHADEMA tunampa wiki mbili awe amejiuzulu.


“Kila mwaka wanafunzi 1,200,000 hadi 1,300,000 nchi nzima wanafanya mitihani yao. Lakini wanaoshinda ni kati ya 35,000 hadi 400,000 pekee, hivyo watoto wengine wanashindwa kuendelea na masomo yao. Kwa hiyo tunataka huyu waziri na naibu wake wajiuzulu ndani ya wiki mbili,” alisema Mbowe.


Alisema kwa sasa Tanzania inazalisha vijana wapatao 800,000 kwa mwaka ambao wanakosa fursa ya kuendelea na masomo yao, na alimtaka Rais Jakaya Kikwete kuacha kucheka na kubembeleza viongozi wabovu wanaodidimiza maendeleo ya nchi na raia wake, na kwamba Tanzania inakabiliwa na majanga makubwa mawili ya elimu duni na udini.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe, alimtaka Waziri Kawambwa na Naibu wake, Mulugo, kuwajibika na kupisha katika wizara hiyo.


Pia alimtaka Rais Kikwete aichukue wizara hiyo na kuwa chini ya ofisi yake.


Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Zitto alisema kuwa ni muhimu viongozi wanaosimamia wizara hiyo wakawajibika.


Alisema uwajibikaji huo unapaswa kufanyika kuanzia kwa katibu mkuu wa wizara hiyo pamoja na kamishna.


Zitto alisema kuwa rais anapaswa aelezwe kuwa iwapo matokeo yatabaki hivi mwakani, na yeye atatakiwa kuondoka katika nafasi hiyo.


Chanzo: Tanzania Daima

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...