Tuesday, August 28, 2012

CHADEMA YATEMBEZA BAKULI KUCHANGIA WAFIWA, MAJERUHI VURUGU ZA POLISI MORO

 
KATIBU mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Dk. Wilbroad, Slaa jana
 alilazimika kuendesha shughuli ya kuomba msaada wa fedha kutoka kwa watu waliofurika kwenye mkutano wa chama hicho mjini Morogoro ili kuwachangia wafiwa na walioathirika na vurugu zilizoanzishwa na polisi dhidi ya wafuasi wa chama hicho.
Akifafanua, alisema zitatumika kuwasaidia majeruhi wawili waliopigwa risasi na polisi jana ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro.
Pia fedha hizo zitapekwa kwa familia ya marehemu Ally Zolla anayesemekana aliuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wa vurugu hizo.
Mmiongoni mwa watu waliozunguka na bakuli hilo ni pamoja na Mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika.
Fedha hizo hazikufahamika idadi yake hadi mwandishi wetu anaondoka kwenye viwanja hivyo majira ya saa moja usiku.

Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika akichangisha michango hiyo.
Michango iliyopatikana ikihesabiwa na makamanda.


MISS EAST AFRICA 2012 KURUSHWA “LIVE” NA M-NET

 
Miss Eritrea Rahwa Afewoki
 
Mashindano ya Miss East Africa mwaka huu yataonyeshwa LIVE kupitia Mnet ambapo yanatarajiwa kutizamwa na watu wanaokadiriwa kufikia million 200 kupitia televison na kwa njia ya internet Dunia nzima.

Aidha maandalizi ya mashindano hayo yanaendelea kwa kasi ambapo yamepangwa kufanyika tarehe 07 December, 2012 katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dare s salaam, Tanzania badala ya mwezi September kama ilivyokuwa imetangazwa awali ili kutoa muda zaidi kwa Nchi ambazo hazijapata wawakilishi wao kuweza kukamilisha zoezi hilo.

Mashindano ya Miss East Africa mwaka huu yanatarajiwa kuwa na mvuto wa aina yake ambapo yatashirikisha warembo kutoka katika Nchi 16 za ukanda wa afrika mashariki.

Nchi zilizothibitisha kushiriki mashindano hayo ni wenyeji Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi. Nchi zingine zilizoalikwa kushiriki ni pamoja na Ethiopia, Eritrea, Somalia, Djibouti, Southern Sudan, Malawi, pamoja na visiwa vya Seychelles, Madagascar, Reunion, Comoros, na Mauritius.

Mashindano ya Miss East Africa yanalenga kukuza ushirikiano na kutangaza utamaduni wa Afrika mashariki, pamoja na kutangaza utalii wa Tanzania kama Nchi wenyeji wa mashindano hayo makubwa katika ukanda huu wa Afrika

Tayari baadhi ya Nchi zinazoshiriki mashindano hayo zimeshatangaza wawakilishi wake ambazo ni Eritrea, Ethiopia, Uganda, Southern Sudan, Malawi na Seychelles. Nchi zilizosalia zinatarajiwa kutangaza wawakilishi wao kabla ya tarehe ya mwisho ambayo ni tarehe 28 mwezi September.

Mashindano ya Miss East Africa yanamilikiwa na kuandaliwa na kampuni ya Rena Events Ltd ya jijini Dar es salaam.

 
 Miss East Africa Seychelles Annabelle Marvel Pointe

Miss East Africa Uganda Aysha Nagudi.

NIGER, GHANA MABINGWA WAPYA AIRTEL RISING STARS AFRIKA 2012


Niger wakishangilia ubingwa wa Airtel Rising Stars Afrika 2012NAIROBI, Kenya



MASHINDANO ya Airtel Rising Stars Afrika 2012 yaliyoshirikisha mataifa 15 barani humu yamehitimisha juzi jijini hapa, ambapo mgeni rasmi wa fainali na nyota wa zamani wa ManchesterUnited, Peter Schmeichel, alikabidhi medali na zawadi kwa washindi upande wa wavulana na wasichana.


Niger walifanikiwa kutwaa ubingwa wa kwanza wa michuano ya kwa wavulana, katika fainali ya michuano hiyo, huku Ghana wakitawazwa mabingwa upande wa wasichana katika mashindano hayo – yaliyoanza na timu 18,000 na kujumuisha vijana walio chini ya miaka 17 wapatao 324,000 Afrika nzima.


Niger iliifunga Zambia kwa penati 5-4 kushinda ubingwa Airetl Rising Stars 2012 kwa wavulana, baada ya kumaliza dakika 90 bila ya kufungana licha ya kosa kosa nyingi kwa kila timu, ambapo pia dakika 30 za nyongeza pia hazikutoa mshindi na kulazimika kupigiana penati.


Mamane Karibou, Issa Souleymane, Abubacar Timbo, Idrissa Amadou na Issifou Garba wa Niger walifunga penati, kama ilivyokuwa kwa Wazambia Timothy Sakala, Thomas Juma Mutale, Dennis Chebuye na Albert Bwalya, huku Shadrack Chimanya akikosa mkwaju wake muhimu.

Katika fainali ya wasichana, Ghana walitoka nyuma na kuwafunga wenyeji Kenya waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kushinda na kuwachapa mabao 2-1.

Kenya walipata bao la uongozi lililowekwa nyavuni na Vivian Odhiambo dakika ya 27, kabla ya Emelia Lokko kuisawazishia Ghana 43 na pambano kuingia mapumziko kwa sare ya bao 1-1. Ghana ikarejea kipindi cha pili ikiwa tishio zaidi, ambapo Patience Narh aliifungia bao la ushindi 56 na kuwaduwaza Wakenya.

Wachezaji vijana 432 walishiriki fainali hizi jijini Nairobi kwa wiki nzima, wakiwezeshwa katika kila mahitaji na wadhamini, waratibu na waendeshaji wa michuano hiyo kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, huku vijana hao wakionyesha vipaji vya hali ya juu na kutoa taswira njema ya soka la Afrika.

Mabingwa Niger na Ghana walizawadiwa fedha taslimu dola za Kimarekani 10,000 kila moja, huku zikipata fursa kwa wachezaji wake wote kushiriki Kliniki Maalum itakayofanyika hapa Nairobi na Accra, Ghana, chini ya wakufunzi wa soka kutoka klabu za Arsenal na Manchester United za England.

SERENGETI BOYS KUKIPIGA NA KENYA UWANJA WA AZAM COMPLEX


Mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza kuwania tiketi ya kucheza Fainali za 10 za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 zitakazofanyika mwakani nchini Morocco kati ya Tanzania (Serengeti Boys) na Kenya itachezwa Septemba 9 mwaka huu Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam.

Tayari Serengeti Boys chini ya Kocha Jakob Michelsen na Msaidizi wake Jamhuri Kihwelo ikiwa na wachezaji 28 iko kambini jijini Dar es Salaam tangu jana (Agosti 27 mwaka huu) kujiandaa kwa mechi hiyo itakayoanza saa 10 kamili jioni.

Wachezaji waliko kambini ni makipa Abdallah Bakar (Mjini Magharibi), Hamad Juma (Azam) na Peter Manyika (JKT Ruvu). Mabeki ni Abdallah Salum (Mjini Magharibi), Basil Seif (Morogoro), Hassan Mganga (Morogoro), Ismail Gambo (Azam), Mgaya Abdul (Azam), Miraji Selemani (Polisi Morogoro), Miza Abdallah (Kinondoni), Mohamed Hussein (Azam), Pascal Matagi (Dodoma) na Paul James (Kinondoni).

Viungo ni Farid Musa (Kilimanjaro), Hussein Twaha (Coastal Union), James Mganda (Kipingu Academy), Mbwana Ilyasa (Simba), Mohamed Haroub (Zanzibar), Mohamed Kapeta (Kinondoni), Mudathiri Yahya (Azam), Mzamiru Said (Morogoro) na Selemani Bofu (JKT Ruvu).

Washambuliaji ni Abdallah Kisimba (Mwanza), Calvin Manyika (Rukwa), Dickson Ambunda (Mwanza), Joseph Lubasha (Azam), Kelvin Friday (Azam) na Salvatory Nkulula (Kipindu Academy).

Mechi ya marudiano itachezwa jijini Nairobi, Kenya kati ya Septemba 21, 22 na 23 mwaka huu. Timu itakayofanikiwa kusonga mbele itacheza raundi ya pili dhidi ya Misri. Mechi ya kwanza itachezwa nyumbani kati ya Oktoba 12, 13 na 14 mwaka huu wakati ya marudiano itakuwa kati ya Oktoba 26, 27 na 28 mwaka huu.
Misri ni kati ya timu 17 zilizoingia moja kwa moja raundi ya pili. Nyingine ni Afrika Kusini, Algeria, Burkina Faso, Cameroon, Congo Brazzaville, Cote d’Ivoire, Gabon, Gambia, Ghana, Guinea, Mali, Rwanda, Senegal, Sierra Leone, Tunisia na Zambia.

WAKATI HUOHUO:- KAMATI YA SHERIA KUPITIA USAJILI SEPT 2
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa inatarajia kukutana Jumapili (Septemba 2 mwaka huu) kupitia usajili wa wachezaji kwa msimu wa 2012/2013.

Usajili utakaopitiwa ni wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) na Lidi Daraja la Kwanza (FDL) ambapo Kamati itapitia pingamizi zilizowasilishwa na klabu mbalimbali dhidi ya wachezaji waliosajiliwa na klabu zingine.

TUSKER KUDHAMINI KOMBE LA CHALLENGE, YATOA MPUNGA LEO KAMPALA



Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye akizungumza na mwasisi wa CECAFA, Kezekia Ssegwanga Musisi kabla ya uzinduzi wa michuano ya mwaka huu ya Tusker katika hoteli ya Serena mjini Kampala leo.

KAMPUNI ya Bia Afrika Mashariki (EABL), kupitia bia yake ya Tusker Lager, leo imetangaza udhamini wa dola za Kimarekani 450,000 kwa ajili ya michuano ya mwaka huu ya Kombe la CECAFA –Tusker Challenge Cup itakayofanyika mjini Kampala, Uganda.
Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) pia imesema mashindano hayo yataanza Novemba 24 kwenye Uwanja wa Taifa wa Mandela, Namboole na kufikia tamati Desemba 8.
Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye alitua Kampala Jumatatu kwa maandalizi ya michuano hiyo na leo wamezindua rasmi kwenye hoteli ya Serena Hotel mjini Kampala na Meneja Masoko wa EABL, Lemmy Mutahi amesema lengo la michuano hiyo ni kuzisaidia maandalizi timu za Afrika Mashariki na Kati katika kuwania tiekti ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014 nchini Brazil.
Musonye alisema udhamini huo ni ongezeko la aslimia 5, kutoka michuano ya mwaka jana mjini Dar es Salaam, ambayo Uganda waliibuka mabingwa.
Musonye alisema udhamini huo utahusu usafiri, malazi na huduma nyingine, wakati jumla ya dola za Kimarekani 60.000 zitakuwa kwa ajili ya zawadi, bingwa akipewa dola 30.000, tmshindi wa pili dola 20.000 na dola 10.000 mshindi wa tatu. Musonye alisema mechi zote zitaonyeshwa na Televisheni ya Super Sport.
 

Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye akipokea Kombe la mwaka huu la Tusker kutoka kwa Mutahi katika hoteli ya Serena mjini Kampala leo. Kulia ni rais wa FUFA, Livingstone Kyambadde.

Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Afrika Mashariki (EABL), Lemmy Mutahi (katikati) akikabidhi mfano wa hundi kwa Katibu wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye. Kulia kabisa ni rais wa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Livingstone Kyambadde mjini Kampala leo.

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...