Thursday, July 26, 2012

BAADA YA MV SKAGIT, HII NDIO TAARIFA RASMI YA AJALI NYINGINE YA JANA.




kama unakumbuka wakati MV SPICE ISLANDERS inazama muda mfupi baadae kuna jahazi la mizigo lilizama likitokea Tanga, sasa stori ya leo ni kwamba baada ya MV SKAGIT kuzama wiki iliyopita Jeshi la Polisi Zanzibar limethibitisha kuzama kwa Jahazi jumatano ya July 25 2012 siku saba baada ya ajali ya MV SKAGIT.

Msemaji wa Polisi Mohamed Mpinga amesema kwamba Jahazi lilikua linatokea Kusini Pemba kwenda Nungwi kaskazini Unguja ambapo mtoto wa miaka mitano Isaka Hamis alipoteza maisha.

Polisi mkoa wa Kusini Pemba wamesema chanzo cha ajali ni ujazaji wa mizigo uliopitiliza kwani Jahazi hilo lilibeba magunia kumi ya Muhogo, mikungu 10 ya ndizi pamoja na mizigo mingine ya kuni. Watu sita walinusurika kifo akiwemo mama mwenye mtoto wa miaka miwili, vyombo hivi vya uvuvi vimekua vikitumika kusafirisha abiria na mizigo kimakosa wakati pia havitakiwi kusafiri umbali mrefu.

HII NDIO KIGALI YA SASA, USIULIZE MIAKA IJAYO!




(hii picha ni kutoka kwa Alpha Rwirangira )

Rais Paul Kagame wa Rwanda amekua miongoni mwa marais wachache wa Ulimwengu wanaopewa sifa nyingi za kweli kuhusu msimamo wao, mipango yao na hata utekelezaji wa hiyo mipango waliyonayo.

Kwa taarifa nilizonazo Rais Kagame ameweza kuibadili Rwanda kwa kiwango kizuri sana ikiwa ni pamoja na nchi kuwa safi, kukua kiuchumi, kujengeka kimpangilio pamoja na ishu nyingine, sasa hivi sehemu kubwa ya mji wa Kigali umejengwa kwa mujibu wa ramani inayotakiwa, nyumba za kuishi zilizo kwenye mpango kama miji mingine ya nchi zilizoendelea, pamoja na barabara za ndani za Kigali kuwekwa mawe kitaalamu kuondoa vumbi kwenye mji.

Nyumba zilivyojengwa kimpangilio kwenye mji wa Kigali.

Huu ni mfano wa jinsi Kigali Rwanda ilivyopangwa, kujengwa katika miaka michache ijayo according to topboxdesign.
Habari/picha:Milard Ayo blog

MESSI AMFUATA OKWI AUSTRIA, SIMBA KULAMBA DOLA 300,000


Messi wa Msimbazi; Rama Singano


Na Princess Asia
KIUNGO chipukizi wa Simba SC, Ramadhani Singano ‘Messi’ anatarajiwa kuondoka nchini wakati wowote kwenda Austria kwa majaribio ya soka ya kulipwa, imeelezwa.
Chanzo cha habari cha uhakika kutoka ndani ya Simba SC, kimesema jana kwamba, Messi amepata ofa hiyo ya majaribio kupitia wakala mmoja wa wachezaji Tanzania, anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), anayefanya kazi na klabu hiyo.
“Kuna wakala mmoja ambaye anafanya kazi na sisi, ameleta ofa hiyo na kama kijana atafuzu, Simba itapata kama dola za Kimarekani 300,000 hivi,”kilisema chanzo kutoka Simba SC.
Messi huyo alipandishwa kutoka timu ya vijana ya Simba msimu uliopita na pamoja na kuingia mara chache akitokea benchi, lakini amewavutia wengi kwa soka yake na kwa sasa ni miongoni mwa wachezaji tegemeo wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes.
Tayari mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, anaendelea na majaribio katika klabu ya FC Red Bull Salzburg ya Austria yenye maskani yake Wals-Siezenheim, nchini humo na baada ya hapo ndipo majibu yatatoka.
Klabu hiyo inayotumia Uwanja wa Red Bull Arena, ikiwa zaidi inafahamika kama SV Austria Salzburg kabla haijanunuliwa na kampuni ya Red Bull mwaka 2005, imewahi kufika Fainali ya Kombe la UEFA mwaka 1994 na inacheza Ligi Kuu ya Austria, iitwayo Bundesliga kama Ligi Kuu ya Ujerumani.
Timu hiyo ni kama timu ambayo Okwi, anachezea kwa sasa, Simba SC, kwani nayo inavaa jezi za rangi ya nyeupe na nyekundu na imewahi kutwaa taji la Bundesliga ya Austria mara saba na pia ilicheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 1994–1995 kama Casino Salzburg, na kuwa timu pekee, ambayo haikufungwa na mabingwa wa wakati huo, Ajax Amsterdam.
Awali, Okwi aliikosesha Simba Sh. Bilioni 2 kwa kukataa kujiunga na klabu ya Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini na kuamua kwenda Austria, ambako inaelezwa klabu hiyo iko tayari kutoa Euro 600,000 akifuzu.
Awali Orlando Pirates ya Afrika Kusini ilimuomba Okwi akafanye majaribio huko kama angefuzu wangemsajili dau la dola 550,000 kabla ya kuibuka kwa taarifa za kutakiwa Italia na klabu ya Parma.
Hata hivyo, Simba SC ilisema imeshindwa kumshawishi Okwi kwenda kucheza Afrika Kusini kwa kuwa mwenyewe anataka kucheza Ulaya tu. Wakala aliyeiunganisha Simba na Pirates akawasilisha ofa nyingine kutoka Mamelodi, ambayo ni Euro 600,000 na kupanda hadi Sh. Bilioni 2, lakini bado mabingwa hao wa Tanzania, walishindwa kumshawishi Okwi kwenda Ligi Kuu ya Afika Kusini (PSL).



YANGA, AZAM KATIKA MTIHANI MZITO WA KUBAKIZA KOMBE NYUMBANI LEO



Spider Man
MABINGWA watetezi wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Yanga SC leo wanashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na timu ya Jeshi la Rwanda, APR katika Nusu Fainali ya pili ya michuano hiyo kuanzia saa 10:00 jioni, mchezo ambao utatanguliwa na Nusu Fainali ya kwanza kati ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Azam FC.
Yanga iliingia Nusu Fainali baada ya kuitoa Mafunzo ya Zanzibar kwa penalti 5-3, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90, wakati APR iliitoa URA ya Uganda kwa kuichapa mabao 2-1.
Nusu Fainali ya pili inayozikutanisha Azam FC iliyoitoa Simba kwa kuichapa 3-1 na AS Vita iliyoitoa Atletico ya Burundi kwa kuichapa 2-1, itaanza saa 8:00 mchana Uwanja huo huo wa Taifa.
Azam na Vita nayo itakuwa mechi tamu, kwa sababu timu zote zinacheza soka ya kuvutia na zina wachezaji wenye vipaji- zaidi kila timu ina mshambuliaji anayewania ufungaji bora wa michuano hii.
Azam kuna John Raphael Bocco ‘Adebayor’ mwenye mabao manne akifungana na Hamisi Kiiza wa Yanga katika nafasi ya tatu, wakati Vita inaye kinara wa mabao katika Kagame ya 2012, Etikiama Taddy mwenye mabao sita, akifuatiwa na Said Bahanuzi ‘Spider Man’ wa Yanga mwenye mabao sita.
Akizungumzia mchezo dhidi ya APR, kocha wa Yanga, Tom Saintefiet alisema kwamba utakuwa mgumu kwa sababu timu hizo zitakuwa zinakutana mara ya pili, baada ya mechi ya awali ya kwenye Kundi lao, C ambayo Yanga ilishinda 2-0.
“Utakuwa mchezo mgumu, APR ni timu nzuri, wanacheza kwa ufundi, nguvu, lakini tunataka kushinda na tutakwenda kupigana ili kushinda,”alisema Tom.


John Bocco 'Adebayor'

Hata hivyo, Mbelgiji huyo alisema katika mchezo wa leo atawakosa kipa wake namba moja Yaw Berko na kiungo Nizar Khalfan ambao wote ni majeruhi.
Mtakatifu Tom alisema kutokana na kucheza mechi mfululizo, wachezaji wengi wa Yanga wanalalamika maumivu, ila wako tayari kucheza na wana nia na dhamira ya kutetea Kombe.
Safu ya ushambuliaji ya APR inaweza kuongozwa na wakali wawili, Mrundi Suleiman Ndikumana na Olivier Karekezi ambao wote wana miili mikubwa ni hatari kweli sambamba na kiungo mshambuliaji, Mganda Danny Wagaluka, wakati Yanga bila shaka Said Bahanuzi na Hamisi Kiiza wataendelea kumpumzisha kwenye benchi Jerry Tegete na Haruna Niyonzima ataongoza safu ya kiungo.
Kihistoria mechi kati ya Yanga na APR huwa ni kali na za kusisimua tangu zianze kukutana mwaka 1996 katika Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati na mara nyingi watoto wa Jangwani ‘hutoshana nguvu’ na timu hiyo ya jeshi la Rwanda.
Azam ikiwa na morali ya hali ya juu, safu yake ya kiungo inatarajiwa kuongozwa na kiungo bora mzalendo kwa sasa Tanzania, Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr’ wakati kwenye ushambuliaji mfungaji bora wa Ligi Kuu, Adebayor wa Chamazi atapewa dhamana.
BIN ZUBEIRY inazitakia kila la heri timu za Tanzania katika hatua hii zishinde leo na kulihakikisha Kombe la Kagame kuendelea kuishi katika Bandari Salama. Mungu ibariki Tanzania, zibariki Azam na Yanga. Amin.


JE WAJUA?

1. Klabu ya Armee Patriotique Rwandaise, maarufu kama A.P.R., ilianzishwa mwaka 1993 na inamilikiwa na Jeshi la Rwanda na katika kipindi cha uhai wake, mafanikio yake makubwa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Rwanda mara 12 (1995, 1996, 1999, 2000, 2001, 2003, 2005, 2006, 2007, 2009, 2010 na 2011), Kombe la Kagame mara mbili (2004 na 2007) na kufika Nusu Fainali ya Kombe la Washindi mwaka 2003.



2. Young Africans SC maarufu kama Yanga iliyoanzishwa rasmi mwaka 1935, hadi sasa mafanikio yake makubwa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara mara 23, (1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2008, 2009 na 2011), Kombe la Kagame mara nne (1975, 1993, 1999 na 2011), kufika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mara tatu (1969, 1970 na 1998) na Kombe la Washindi 1996.

3. Wakati Yanga, kocha wake ni Mbelgiji Tom Saintfiet, APR inafundishwa na kocha Mholanzi, Ernie Brandts- na wakati Yanga Mwenyekiti wake ni mfanyabiashara milionea, Yussuf Manji, APR Mwenyekiti wake ni mdogo wa rais wa Rwanda, Paul Kagame aitwaye Alex Kagame.

4. Nembo ya Yanga ina alama ya Mwenge, ramani ya Afrika na mpira- ikimaanisha kushiriki harakati za Uhuru wa Tanganyika, ambayo baadaye iliungana na Zanzibar na kuwa Tanzania (Mwenge), timu halisi ya Afrika (ramani) na timu ya mpira (mpira), wakati nembo ya APR ina alama ya mnyama Simba na mpira- vikimaanisha, ni wafalme kama mnyama Simba porini (Simba) na timu ya mpira (mpira).

5. Wakati Yanga ambayo huvalia jezi za rangi ya kijani na njano, ilishiriki michuano hii kwa mara ya kwanza mwaka 1975 na kutwaa Kombe, APR ambao huvalia jezi za rangi nyeupe na nyeusi siku zote, mara nyingi zikiwa za mistari ya punda milia, ilishiriki kwa mara ya kwanza michuano hii mwaka 1996 na kushika nafasi ya pili, baada ya kufungwa 1-0 na Simba kwenye fainali.


6. Wakati wapinzani wa jadi wa Yanga, nchini Tanzania ni Simba SC kwa APR wapinzani wao wa jadi Rwanda ni Rayon Sport.


Makocha; Ernest Brandy Mholanzi wa APR kulia na Tom Saintfiet Mbelgiji wa Yanga



REKODI YA YANGA NA APR KAGAME;
1996 Dar es Salaam; Yanga 2-2 APR (Nusu Fainali, APR ilishinda kwa penalti 4-2)
2008 Dar es Salaam; Yanga 2-2 APR (Kundi C)
2012 Dar es Salaam; Yanga 2-0 APR (Kundi C, Julai 20)
2012 Dar es Salaam; Yanga V APR (Nusu Fainali, Julai 26)

Wednesday, July 25, 2012

MAADHIMISHO YA SIKU YA KUMBUKUMBU YA MASHUJAA VIWANJA VYA MNAZI MMOJA LEO



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, wakati alipowasili kwenye uwanja wa Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo Julai 25, 2012 kwa ajili ya kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Kikwete, akiwasili kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam leo, Julai 25, 2012 kuhudhuria sherehe za maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa, leo

Kutoka (kushoto) Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Rais wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd, Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Ameir Kificho, ........ na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Shamsi Vuai Nahodha, wakiwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja wakihudhuria sherehe za maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa, leo Julai 25, 2012.

Rais Dkt. Jakaya Kikwete, akiweka Ngao na Mkuki kwenye Mnara wa Mashujaa, wakati wa maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa, iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam



Rais Dkt. Jakaya Kikwete, akisalimiana na baadhi ya wazee waliopigana vita mbalimbali vya ukombozi wa nchi ya Tanzania, waliohudhuria katika maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa, iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na baadhi ya wazee waliopigana vita mbalimbali vya ukombozi wa nchi ya Tanzania, waliohudhuria katika maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa, iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisalimiana na baadhi ya wazee waliopigana vita mbalimbali vya ukombozi wa nchi ya Tanzania, waliohudhuria katika maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya Mashujaa, iliyofanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, leo Julai 25, 2012.

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...