Friday, April 11, 2014

AUNT EZEKIEL ATIMULIWA NYUMBANI KWA WEMA SEPETU


IMBWILI la aina yake limetokea nyumbani kwa ‘Beautiful Onyinye’ wa Bongo, Wema Sepetu, kati ya Martin Kadinda na nyota wa filamu za Bongo, Aunt Ezekiel, ‘Kubwa’ lina kisa klizima. Kwa mujibu wa chanzo chetu, gogoro zima lilishika nafasi asubuhi ya Aprili 6, 2014 nyumbani kwa Wema, Makumbusho jijini Dar es Salaam, kufuatia Kadinda ambaye ni meneja wa Wema kumvurumishia shutuma Aunt akidai ni mnafiki mkubwa, tena ndiye chanzo cha Kajala Masanja na Wema kutibuana huku akimtaka aondoke.


TWENDE POLEPOLE
Chanzo kilisema, siku hiyo Aunt alilala nyumbani kwa supastaa huyo, lakini asubuhi wakiwa bado wanagalagala kwenye sita kwa sita, Kadinda alifika na kuwakuta hawajaamka, ndipo alipolianzisha.
Kwanza aliwaamsha huku akimshutumu Aunt kwa nini amelala pale wakati ana kwake na ni mke wa mtu?
Mpashaji wetu alizidi kuweka wazi kwamba, baada ya Martin kumuuliza swali hilo, Aunt hakuwa na jibu la moja kwa moja (pengine alikodoa macho tu), ndipo jamaa huyo alipomwanzishia vita ya maneno makali huku akisisitiza aondoke.

KISIKILIZE CHANZO

“Siku hiyo Martin unayemjua wewe hakuwa mwenyewe. Alikuwa mkali sana. Ilifika mahali alimshangaa kwa nini yeye (Aunt) ni mke wa mtu halafu anakwenda kulala nyumbani kwa Wema na si kwake Mwananyamala?
“Alimwambia ujirani wake na Wema ndiyo umekuwa chanzo cha ugomvi wa madam huyo na staa mwenzake wa filamu, Kajala.


Aunt Ezekiel. “Yeye Martin anaamini kwamba, kuna maneno ambayo Aunt anayasema kwa Wema kuhusu Kajala ndiyo maana sasa hivi hawapikiki. Si unajua kwa sasa, Wema na Aunt ni kama pochi na kwapa?” chanzo kilimwaga mchele na kusisitiza jina lake kufichwa kapuni kama si kibindoni kabisa.

WEMA KATIKATI YA GOGORO
Mtonyo uliendelea kudai kwamba, wakati Martin akizidi ‘kumpelekea’ Aunt na kuifanya nyumba ikikose amani kwa kelele, Wema aliingilia kati na kumhoji meneja wake hivi: “Kama umechukizwa na kitendo cha Aunt kulala hapa, kwa nini unamuingiza Kajala kwenye ugomvi?”

AUNT: WE MARTIN UNA SABABU NYINGINE!
Muda wote huo, Aunt alibaki kimya, lakini madongo yalipozidi alijilipizia kwa kumwambia Martin kwamba, labda ana sababu nyingine lakini siyo kumwingiza katika ugomvi wa Wema na Kajala ambao haujui chanzo chake.

“Aunt alijizuia mwisho akamwambia we Martin una sababu nyingine, kwa nini unaniingiza mimi kwenye ugomvi wa Kajala na Wema?” chanzo kilisema kikimkariri Aunt.

IJUMAA ‘KUBWA’ LAWASAKA WOTE
Baada ya kupata nzitonzito hiyo, paparazi wetu alianza kwa kumtafuta Martin alipopatikana alikiri kutokea kwa ugomvi huo na kusema:
“Nilikuwa najaribu tu kumuelewesha Wema na Aunt kwa kuwa watu kwa hivi sasa wanawatazama kwa mtazamo tofauti kabisa na wanavyoamini wao. Mimi ndiyo nafahamu hivyo.
“Unajua watu wanamsema Aunt vibaya sana, hajui tu. Wanadai kwamba yeye ndiyo chanzo hasa cha ugomvi wa Kajala na Wema, sasa nilivyomkuta amelala pale ndiyo na mimi nikacharuka kwa kuwa kuna mambo ambayo tulikuwa hatujayafanya na Wema kwa sababu Aunt yuko pale,” alisema Martin bila kutaja mambo hayo ni yapi.

WEMA SASA

Kwa upande wake Wema alipopatikana hewani na kuulizwa kuhusu kisanga hicho, naye alikiri kutokea lakini akasema ‘mwisho wa siku’ waliweka mambo sawa.
“Ulikuwa ugomvi wa kawaida, si unajua sisi ni binadamu, Lakini baada ya yote waliweka mambo sawa na shughuli nyingine zikaendelea,” alisema Wema.
Paparazi: Ni kweli yeye ndiyo chanzo cha wewe na Kajala kugombana?
Wema: Noo! Hakuna kitu kama hicho. Kwanza hajui chochote kuhusu mimi na Kajala.

AUNT HOLA!

Juzi, Aunt alitafutwa kwa njia ya simu lakini hakupatikana. Paparazi alifika nyumbani kwake Mwananyamala ambapo wanyeji waliokutwa walisema amesafiri Dubai kwa mume wake.
Paparazi: Naweza kupata namba yake?
Mwenyeji: Aah! Wala hutuna, labda uje siku nyingine.

TUKIRUDI NYUMA
Kwa sasa, Wema na Aunt ni kama ‘mgambo wa jiji na machinga’ kila kukicha wapo sambamba lakini awali, Wema alikuwa na urafiki mkubwa na Kajala.
Wema ndiye aliyemtolea Kajala fedha kiasi cha shilingi milioni 13 kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar hivyo kumnusuru na kifungo katika keshi ya mwanadada huyo ya kutakatisha fedha chafu na kuuza nyumba iliyo kwenye dhamana kisheria.
Baada ya kuachiwa huru, Kajala na Wema walikuwa kama ‘bwana afya na bucha la nyama’ huku wengi wakimpongeza Wema kwa uamuzi wake huo mgumu.
Cha ajabu, siku za hivi karibuni, wawili hao wako kama Kaskazini na Kusini kwamba hawawezi kuwa sanjari, kisa kikidaiwa si kimoja. Wengine wanadai chanzo ni Kajala ‘kambeba’ jumla aliyekuwa bwana wa Wema, Clement ‘Kigogo wa Ikulu’.
Wapo pia waliodai kwamba, uadui wao umetokana na Kajala kuanza kuwa tajiri huku Wema akishuka kila kukicha. Lakini Aunt naye amekuwa akitajwatajwa kuchochea uhasama huo

JOKATE AHAMISHIA KIDOTI CHAKE KWENYE NDALA

Picha ya bidhaa mpya ya ndala ya Kidoti.

Mwanamitindo na mtangazaji wa TV nchini, Jokate Mwegelo amefunguka kwa kusema kuwa ameamua kufungua biashara ya ndala za brand yake ya ‘Kidoti’ kutokana na mapenzi yake ya uvaaji wa ndala kataki maisha yake ya kawaida .

“Mimi napenda kuvaa ndala, napenda kuvaa wakati nakwenda kushoot,siwezi kuvaa high hills wakati nashoot, wakati unapakwa make up unaonaee, unatengenezwa nywele, you cannot wear hills lazima uwe umevaa kitu comfortable,”.

“Kwahiyo nikaona kwamba ndala ni kitu kizuri,napenda kuvaa ndala,ni kitu easy,kuvaa rahisi halafu ni kitu ambacho watu wanakihitaji why not have ndala ambazo zina mvuto wa kipekee? Kama nilivyohaidi watu kwamba Jokate kupitia brand ya Kidoti itaanzisha bidhaa mbalimbali kukidhi mahitaji ya watu na jamii mzima.


Mwanamitindo na mtangazaji wa TV nchini, Jokate Mwegelo.

Nashukuru kuna support kwa Kidoti yenyewe kama brand. Kwahiyo tutaendelea kutoa vitu mbalimbali vya kufurahisha. Unajua kutoa surprise ni njia moja wapo ya kufurahisha, hawakutegemea kupata kitu kuzuri lakini wamekipata. Kwahiyo ni mambo ya Kidoti hayo ni bidhaa nzuri waipokee na tutaendelea kutoa bidhaa mbalimbali.” aliongeza.

Pia Kidoti amesema kuwa bidhaa ya ndala ya Kidoti itapatikana Tanzania nzima.
“Tutasambaza Dar es salaam nzima na mikoani,kwahiyo ni kitu ambacho kipo katika mipangilio ya kusambambaza sehemu mbalimbali ili upatikanaji uwe rahisi na tunafanya jitihada za kutangaza sehemu ambazo zitakuwa zinapatikana.”

TFF YAMTEUA MWAMUZI CHACHA KUCHEZESHA MICHUANO YA AYG


Release No. 061
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Aprili 11, 2014
CHACHA KUCHEZESHA MICHUANO YA AYG

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua mwamuzi msaidizi wa Tanzania anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ferdinand Chacha ameteuliwa kuchezesha michezo ya Vijana ya Afrika (AYG- African Youth Games).

Michezo hiyo ya kwanza ya Afrika itachezesha jijini Gaborone, Botswana kuanzia Mei 22-31 mwaka huu. Tanzania pia itashiriki katika mashindano hayo ya vijana wenye umri chini ya miaka 15.

SIMBA, ASHANTI UTD KUVAANA TAIFA
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho(Aprili 12 mwaka huu) katika raundi ya 25 ambapo Simba na Ashanti United zitapambana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.

Mechi nyingine zitakuwa kati ya Tanzania Prisons na Rhino Rangers (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, jijini Mbeya) wakati Coastal Union itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Keshokutwa (Aprili 13 mwaka huu) kutakuwa na mechi nyingine nne za kukamilisha raundi hiyo. Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya wenyeji Oljoro JKT na Yanga.

Mtibwa Sugar itacheza na Ruvu Shooting (Uwanja wa Manungu, Morogoro), Mgambo Shooting na Kagera Sugar zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku Mbeya City ikiumana na Azam kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

TIMU YA WATOTO WA MITAANI YATAMBULISHWA BUNGENI

Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania iliyotwaa ubingwa wa Dunia wa Watoto wa Mitaani nchini Brazil baada ya kuifunga Burundi mabao 3-1 kwenye fainali imetambulishwa leo (Aprili 11 mwaka huu) katika Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.

Baadaye timu hiyo leo itapata chakula cha mchana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda. Saa 10 jioni itatembeza kombe hilo katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Dodoma katika gari za wazi.
Jioni imeandaliwa hafla maalumu ya chakula pamoja na burudani hapo hapo mjini Dodoma ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.

MWENYEKITI WA CECAFA KUZUNGUMZA NA WAANDISHI

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodegar Tenga atakuwa na mkutano na waandishi wa habari Jumatatu (Aprili 14 mwaka huu).

Mkutano huo utafanyika kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizopo Ghorofa ya 3, Jengo la PPF Tower mtaa wa Ohio/Garden Avenue kuanzia saa 5 kamili asubuhi.

BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)

MBUNGE WA UBUNGO AOMBA HATI YA MUUNGANO

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, John Mnyika.

MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, John Mnyika, amesema atawasilisha hoja kuzuia shughuli za Bunge hilo kuendelea mpaka wajumbe watakapopatiwa hati halisi ya Muungano.

Mnyika, ambaye ni Mbunge wa Ubungo (Chadema) alitoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya wajenzi na kusema kuwa ameamua kuchukua hatua hiyo kwa vile hadi sasa serikali haijatoa hati halisi ya Muungano ingawa ni muhimu wajumbe waione.

Alikumbusha kuwa baada ya kupitishwa kwa Kanuni za Bunge alitaka kanuni ziruhusu wajumbe wa Bunge wapewe nyaraka wanazotaka katika utendaji wao wa kazi.

“Niliposema hivyo, Mbunge wa Simanjiro Ole Sendeka, alisimama na kupinga na akasema huyu Mnyika anataka kudai hati ya Muungano, naomba kanuni hiyo isiwepo” alisema.

Alisema Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar alisimama na kusema kuwa hati hiyo ipo katika Sheria ya Muungano, lakini hakuna hati halisi wakati taarifa zingine zikisema kuwa ipo Umoja wa Mataifa.

“Hata hivyo baada ya kanuni hiyo kupita, nilimwandikia barua Katibu wa Bunge kuomba hati halisi ya muungano, lakini hadi sasa hivi ninavyozungumza sijapewa hati hiyo.“
Alisema msingi wa Rasimu ya Katiba ni Hati ya Muungano na kwamba umefika wakati sasa wajadili rasimu huku wakiwa na hati halisi.

“Hawa CCM wanadai uwazi kwa kukataa kura ya siri sasa inabidi waonyeshe mfano kwa kuweka wazi Hati ya Muungano, wakikomaa tutawashtaki kwa wananchi,” alisema.

KABURI LA SHEIKH YAHYA HUSSEIN LAFUKULIWA





Kaburi la Sheikh Yahya Hussein ambaye alizikwa tarehe
21.5.2011.
Makaburi mawili ya Sheikh Yahya Hussein na Sheikh Kaseem Bin Jumaa yamevunjwa na mgambo wa jiji saa nane usiku eneo la Tambaza, makaburi ambayo yana muda mrefu katika eno hilo.

Hata hivyo haijajulikana chanzo cha kuvunjwa kwa makaburi hayo.

Wakiongea na waandishi wa habari baadhi ya wafanyabiashara wa maduka ya vyakula eneo hilo wamedai kuwa, walifika asubuhi na kukuta hali hiyo ya kuvunjwa kwa vibaraza vya maduka yao pamoja na kuvunjwa kwa makaburi hayo mawili ya watu masheikh mashuhuri hapa nchini.

Kaburi la Sheikh Kaseem Bin Juma ambaye alizikwa
mwaka 1994.

Naye mtoto wa marehemu Sheikh Yahya Hussein, Bi. Mariam Hussein alifika katika makaburi hayo na kujionea kwa macho yake jinsi kaburi la Baba yake lilivyobomolewa.

Mariam amesema anasikitishwa sana kwa kuvunjwa kwa kaburi la Baba yake bila ya sababu ya msingi.



Mtoto wa Marehem Sheikh Yahya Hussein, Mariam Yahya
Hussein akitafakari jambo kwenye eneo
alilozikwa Baba yake mzazi.

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...