Thursday, June 7, 2012

YONDAN AKAMILISHA ASAINI RASMI YANGA
Yondan akikamilisha usajili wake Yanga, mbele ya Seif Magari kulia, Kushoto ni mtu wa Simba, ambaye alimpeleka mchezaji huyo kumaliza usajili naye akapewa posho yake.
KELVIN Patrick Yondan, beki wa kati wa Simba alikana kusaini mkataba wowote na Simba na alisema yeye alisaini Yanga tu mkataba wa miaka miwili.
Akizungumza Yondan alimesema Simba walimpakazia kusaini mkataba mpya na anataka wapenzi wote wa soka Tanzania watambue kwamba kuanzia sasa yeye ni mchezaji halali wa Yanga.
"Kesho tutaongea vizuri, nimechoka,"alisema Yondan baada ya kukamilisha usajili wake, mbele ya mgombea Ujumbe wa kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb na swahiba wake Seif Ahmad 'Magari' usiku huu.
"Alikuwa amesaini kila kitu, kuna sehemu alikuwa hajamaliza kujaza, ndio amemalizia na ametuhakikishia hana mkataba na Simba, hivyo huyu ni mchezaji ambaye mimi na Seif tunamsajili kwa ajili ya klabu yetu kipenzi, Yanga,"alisema Bin Kleb.
  Yondan aliikana Yanga awali kwa sababu walimsainisha fomu bila kumpa fedha, lakini kwa sasa amepewa Milioni 30 zake taslimu na amemaliza kila kitu.
PICHA/HABARI : BINZUIBERY  BLOG

Wednesday, June 6, 2012



MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amesema moto uliowashwa na chama hicho katika Operesheni Sangara utaendelea nchi nzima, lengo likiwa ni kuiondoa CCM madarakani na iwapo itasalimika mwaka 2015, atajiuzulu siasa.

Mbowe alitoa kauli hiyo juzi alipohutubia mamia ya wakazi wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wakati chama hicho kilipofanya mkutano mkubwa kwenye uwanja wa mpira wilayani humo.
Alisema CCM kimepoteza mwelekeo wa kuongoza taifa na ndiyo sababu maisha ya Watanzania yamezidi kuwa mgumu kadri miaka inavyozidi kusonga mbele.

“Wajibu wa Serikali kokote duniani ni moja tu, kuwezesha watu wake kutoka katika hali ngumu za maisha na kuwapeleka kwenye heri, leo CCM wameligawa Taifa katika vipande, wanauza rasilimali za nchi na kuwadidimiza watu wa kipato cha chini wengi wao wakiwa ni wakulima,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Ndugu zangu ngojeni niwaulize swali, wakati wa utawala wa Mwinyi na Mkapa (marais wastaafu, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa), ni kipindi gani maisha yalikuwa mazuri?” Wananchi wakajibu (kipindi cha Mwinyi). Miaka 10 ya uongozi wa Mkapa na miaka saba ya Kikwete, ni kipindi gani maisha yamekuwa magumu zaidi?" Wakajibu (Kikwete); Je, 2015 wanakuja tena kutuomba kura huyo atakayekuja si ndiyo itakuwa mbaya zaidi, Chadema hatuwezi kukubali na moto huu tuliowasha utaendelea nchi nzima hadi Uchaguzi Mkuu wa 2015 na kama CCM itasalimika nitajiuzulu siasa.”

Mbowe alikishambulia CCM akidai kimepoteza mwelekeo uliowekwa na waasisi wake, chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere wa kuzingatia usawa, udugu huku kikijikita katika msingi wa kutetea wakulima wanyonge na wafanyakazi lakini sasa kimewagawa wananchi katika matabaka ya walio nacho na wasio nacho.

“CCM ya Mwalimu Nyerere ilijali wakulima na wafanyakazi wa kipato cha chini, ilijenga mshikamano baina ya Watanzania wote bila kujali ukabila. Tanzania ina makabila zaidi ya 120, lakini tunaishi kama mtu na ndugu yake, leo taifa limegawanyika vipande huku maadili ya uongozi yakiporomoka,” alisema Mbowe.

Katika mkutano huo uliokutanisha viongozi wote wa kitaifa wa chama hicho, Mbowe alisema kwa sasa CCM kimevuruga hata mitalaa ya elimu huku akituhumu watunga sera kuwa wanafanya hivyo makusudi kwa kuwa watoto wao hawasomi katika shule hizo.

“Mwalimu alijenga CCM iliyozingatia usawa, watoto wote walisoma shule moja, mimi nilisoma na watoto wa Mwalimu Nyerere, mawaziri na wakulima katika shule hiyo, leo watoto wa mkulima wanasoma shule za kata ambazo hazina walimu, vitabu, maabara wala library (maktaba), wakati watoto wa vigogo wakisoma nchi nje na wale wa wakuu wa wilaya wakisoma shule za (academy),” alisema Mbowe.
Aliwataka wakazi wa mikoa ya kusini, Lindi na Mtwara kuunganisha nguvu kwa lengo la kukiondoa CCM madarakani katika chaguzi zote ukiwamo mkuu wa 2015.

“Ndugu zangu wa Masasi, mimi Mbowe ninatimiza miaka 21 nikiongoza siasa za upinzani zenye lengo la kuleta ukombozi wa kweli kwa Taifa hili, nimefunguliwa kesi za uchochezi tisa hadi leo, lakini sitaacha harakati hata wakinifunga, bado nitaendelea na harakati za ukombozi hadi Watanzania watakapofikia kwenye uhuru wa kweli,” alisema Mbowe.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alieleza kusikitishwa kwake na umaskini unaoukabili Mkoa wa Mtwara licha ya kuwapo rasilimali nyingi zinazouzunguka ikiwamo gesi na korosho.

Alisema kumekuwa na ufisadi mkubwa unaofanywa katika ununuzi wa korosho na licha ya wananchi kukatwa Sh30 katika kila kilo wanayouza, bado mikoa hiyo ya kusini inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji, huduma muhimu za kijamii kama zahanati na shule.

“Taifa linaweza kuendelea ikiwa rasilimali za nchi ambazo zinatoka kwa wananchi zitawarudia na kutumika katika kuendeleza miradi ya maendeleo. Leo mnakatwa Sh30 katika kila kilo moja ya korosho mnayouza, tumetafuta ni kiasi gani cha korosho kimepatikana kwa mwaka hapa nchini lakini taarifa hizo hatuzipati.”

RAIS KIKWETE ACHANGISHA BILIONI 3.2 KATIKA HARAMBEE YA KUCHANGIA MKAPA HIV/AIDS FOUNDATION



Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akimpongeza Bw. Deo Mwanyika, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Barrick Tanzania baada ya kuibuka mchangiaji mkubwa kwa kutoa dola za Kimarekani laki 5 kwa ajili ya kuchangia taasisi ya Mkapa Hiv/Aids Foundation Jumanne Juni 5, 2012 usiku katika hoteli ya Kilimanjaro jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi na kulia ni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mzee Benjamin William Mkapa aliyeandaa hafla hiyo iliyoweza kukusanya shilingi bilioni 3.2 na kuvuka malengo ya harambee hiyo kwa asilimia sita.



Rais Jakaya Kikwete, akimkabidhi picha ya kuchora Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya UNDI Consulting Group Limited, Bw Philip Makoka aliyoinunua kwa shilingi milioni 20 wakati wa Harambee ya kuchangia fedha programu ya Mkapa Fellows inayoendeshwa naTaasisi ya Mkapa HIV/AIDS iliyofanyika Dar es Salaam kwenye hoteli ya Kilimanjaro Hyatt Regency jijini Dar es Salaam. Kulia ni mchoraji wa picha hiyo, Bwana Muzu.



Rais Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akisindikizwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi (kushoto) na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mzee Benjamin William Mkapa baada ya kuwa mgeni rasmi katika harambee ya kuchangia Taasisi ya Mkapa HIV/AIDS foundation na kusaidia kukusanya shilingi bilioni 3.2 na kuvuka malengo ya harambee hiyo kwa asilimia sita.

(PICHA NA IKULU)
TANZANIA YAPANDA KATIKA VIWANGO VYA SOKA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Juni 6, 2012
Tanzania imepanda kwa nafasi sita kwenye orodha ya viwango ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) iliyotolewa leo (Juni 6 mwaka huu) na shirikisho hilo.
Kwa viwango vya Mei mwaka huu, Tanzania ambayo timu yake ya Taifa (Taifa Stars) inadhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilikuwa namba 145 hivi sasa imefika nafasi ya 139 ikiwa na pointi 214.
Mei 26 mwaka huu Taifa Stars ilicheza mechi ya kirafiki na Malawi na kutoka suluhu. Malawi yenye pointi 324 imeporomoka kwa nafasi tano kutoka ya 102 hadi 107.
Ivory Coast ambayo katika mechi yake ya mwisho Juni 2 mwaka huu iliifunga Taifa Stars mabao 2-0 imeporomoka kwa nafasi moja kutoka ya 15 hadi 16 ikiwa na pointi 943. Hata hivyo ndiyo inayoongoza kwa upande wan chi za Afrika katika viwango hivyo.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)



WABUNGE WA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI WALA KIAPO

Mh. Samuel Sitta ambayeni mwakilishi wa Tanzania.

Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wameapishwa rasmi kushika madaraka hayo huku Tanzania ikiwa na Wawakilishi tisa katika Bunge hilo.

Wabunge hao waliapa baada ya kupatikana Spika wa mpya wa Bunge hilo ambapo safari hii ikiwa ni Uganda kushika Uongozi huo wa Juu wa Bunge na Mwana Uchumi, Margareth Zziwa kuchukua nafasi hiyo.

Wabunge wote wa Tanzania katika Bunge la Jumuiya ya Mashariki waliokula kiapo ni pamoja na Mwenyekiti wa Wabunge wa Tanzania kwenye Bunge EALA, Alhaj Adam Omar Kimbisa na Katibu wake, Mh Shy-Rose Saddrudin Bhanji.

Wengine ni Mhe. Anjela Charless Kizigha, Mh. Maryam Ussi Yahya, Mh.Nderkindo Perpetua Kessy, Dkt Twaha Issa Taslima, Mhe. Abdullah Ali Hassan Mwinyi, Mhe Bernard Musomi Murunyana, Mhe. Charles Makongoro Nyerere na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta anaeingia kwa wadhifa wake wa Uwaziri.

Wabunge hao wameapishwa pamoja jana na wabunge wenzao wa Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi.

Mh.Abdullah Alli Hassan Mwinyi.

Mbunge Shy-Rose Banji akila kiapo chake.

Shy Rose-Banji akitia saini nyaraka za kiapo.

Mh.Charles Makongoro Nyerere.

Mh. Alhaji. Adam Kimbisa.

Dkt Twaha Issa Taslima.

Mh.Nderkindo Perpetua Kessy.

Mhe Bernard Musomi Murunyana.

Mhe. Anjela Charless Kizigha.

---

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...