Friday, January 1, 2016

Ray C, kama ni kweli unamuaibisha JK kwa makusudi


Rehema Chalamila Ray C.

MIONGONI mwa wasanii ambao wanabeba nembo ya Muziki wa Kizazi Kipya upande wa wanawake, huwezi kuacha kulitaja kwa kujiamini kabisa jina la Rehema Chalamila, ambaye mashabiki wanamtambua zaidi kama Ray C.

Alifanya kazi kubwa, siyo tu kuonesha kuwa wanawake wanaweza, bali pia kuthibitisha kiasi kikubwa cha ubora wake katika tungo, uimbaji na zaidi, uwezo wa kutumia mwili wake kuvutia mashabiki kwa kuonesha manjonjo jukwaani.

Jambo hili lilisababisha kupata wafuasi wengi ndani na nje ya nchi kiasi cha wakati f’lani kuwa miongoni mwa wasanii wachache wa kike waliokuwa wakialikwa katika matamasha kwa bei mbaya, enzi ambazo yeye, Lady Jaydee, Stara Thomas na Unique Sisters walikamata Bongo Fleva.

Huenda, uwezo wake huo, uliomfanya kukutana na watu wengi katika maeneo mbalimbali, ndiyo uliomfanya akaanza kubadili aina ya maisha yake, kutoka yale aliyozoea hadi mapya, ambayo kwa bahati mbaya, yanaelekea kumaliza enzi zake zitakazobaki historia.

Upo ushahidi wa wazi kuwa binti huyu, akiwa kileleni kabisa mwa mafanikio yake, alijiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya, ujinga ambao unafanywa na wasanii wengi wa Muziki wa Kizazi Kipya, wenyewe wakidhani kwa kufanya hivyo, wanaonekana kuwa wajanja na watoto wa mjini, wakati ukweli ni kinyume chake.

Baada ya picha zilizonaswa akiwa yuko bwii kutolewa gazetini, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alijitolea kumsaidia, kwani alikumbuka mchango wake mkubwa katika Bongo Fleva.

Baada ya kupata matibabu na kufikia unafuu wa kuridhisha, akiwa na mama yake mzazi, Ray C alikwenda Ikulu mjini Dar es Salaam kumshukuru Kikwete kwa msaada wake mkubwa na kuahidi kwa umma kuwa asingerejea tena kwenye kubwia unga.

Hata baada ya kuwa bado anaendelea kupata matibabu ya kumsaidia kuachana na matumizi hayo ya unga, yapo madai ya chinichini kuwa msanii huyo aliyewahi kubatizwa jina la Kiuno Bila Mfupa, anaendelea kula ‘ngada’.

Wanaodai hivyo ni watu wake wa karibu, ndugu zake na hata watu ambao wamemsaidia sana kumrejesha katika ‘dunia’ inayotakiwa.

Tunawajua watu wengi waliotumia unga na kuathirika vibaya, lakini baada ya kusaidiwa kujitambua, waliamua kwa dhati kufuata masharti ya dozi na hatimaye wamepona kabisa na wanaendelea na kazi za ujenzi wa taifa kama kawaida.

Anaweza kukataa kwa nguvu kubwa kuwa ameacha kula ‘sembe’, lakini utumiaji wa madawa uliokithiri haujifichi, hata kwa mwonekano tu wa kawaida humtambulisha, ndiyo maana mateja wote wa unga muonekano wa sura zao unafanana!

Nimshauri tu kwa nia njema kuwa ulaji unga haujawahi kusaidia maisha ya mtumiaji yeyote, awe staa au raia wa kawaida. Kwa taarifa yake, wajanja wote wanaukimbia unga na kuwaachia mafala, ndiyo maana kila siku wanabakia kuwa ombaomba, wadokozi na baadhi yao kufanya uhalifu unaokatiza maisha yao.

Ingawa kila mtu ana haki ya kuachwa kuishi maisha yake binafsi, lakini baadhi ya staili, licha ya kuwa ni uvunjaji wa sheria, pia hazikubaliki. Ni mjinga pekee ndiye anaweza kujivunia staili ya maisha inayomaliza uwezo wake wa kufikiri, kutenda na hata kuendelea.

Na sisi wengine, hatupaswi kukaa kimya tunapoona mtu mwenye uwezo wa kujiendeleza yeye binafsi na jamii inayomzunguka, akijimaliza makusudi. Huenda alianza kuvuta akiwa hajui athari zake kwa vile alikuwa bado ‘mshamba’, lakini vipi leo aendelee hata baada ya kushtuliwa kuwa unga ni soo?

Ray C, kama yanayosemwa ni kweli, jitazame upya kwani kujiingiza kwenye unga tena ni kumuabisha Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...