Tuesday, January 19, 2016

MUUZA UNGA MAARUFU AKAMATWA DAR!


Mfanyabiashara maarufu jijini Dar ‘kigogo’, Daudi Yakubu Kanyau anayehusishwa na biashara ya unga.

Stori: Makongoro Oging’ na Issa Mnally, UWAZI
DAR ES SALAAM: Mfanyabiashara maarufu jijini Dar ‘kigogo’, Daudi Yakubu Kanyau (pichani) anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kikosi cha Kupambana na Kudhibiti Madawa ya Kulevya, Makao Makuu Ufundi, Kilwa Road, Dar akihusishwa kwa namna moja au nyingine na biashara ya madawa hayo maarufu kwa jina la ‘unga’.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, mfanyabiashara huyo alikuwa akitafutwa na dola kwa kufuatilia nyendo zake siku nyingi baada ya kuwemo kwenye orodha ya watu wanaosadikiwa kuijua kiundani biashara hiyo.

Nyumba aliyomjengea mtumishi wake.

TAARIFA NDANI YA JESHI LA POLISI
Taarifa zilizopatikana ndani ya jeshi la polisi zinadai kuwa Kanyau alikamatwa nyumbani kwake, Salasala jijini Dar wiki moja iliyopita kwa ushirikiano wa kikosi cha madawa ya kulevya na kikosi cha kupambana na utakatishaji fedha haramu (money laundering) ambao wao huchunguza utajiri wa mtu na uhalali wa kipato.

MALI ZAKE ZASHIKILIWA
Habari zaidi kutoka ndani ya jeshi hilo zinadai kuwa polisi wanashikilia mali za Daudi kwa ajili ya uchunguzi wa namna alivyozipata pia kuchunguza misaada mbalimbali aliyokuwa akiitoa kwa jamii, kama vile kujenga nyumba za familia, ibada na mingine.

KWA NINI?
Hatua hiyo imekuja baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kutangaza vita dhidi ya wauzaji na watumiaji wa unga na kuagizwa kukamatwa mara moja, wakiwemo wale wanaoshukiwa.


Moja ya gari lake linaloshikiliwa.

DCI ANENA
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Tanzania, Diwani Athumani hivi karibuni aliliambia gazeti hili kuwa msako mkali umeanzishwa na watu wengi wamekamatwa, wakiwemo vigogo lakini hakuwa tayari kutaja majina yao hadharani kwa madai kwamba upelelezi bado unaendelea.

ALIWAHI KUKAMATWA UWANJA WA NDEGE
Jumamosi iliyopita, Uwazi lilizungumza na kamishna mstaafu, SACP Godfrey Nzowa ambaye alikuwa bosi wa kitengo cha kudhibiti madawa ya kulevya ambapo alisema miaka mitatu iliyopita, yeye aliwahi kumkamata Kanyau kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar.

HUYU HAPA NZOWA MWENYEWE
“Mimi niliwahi kumkamata Kanyau miaka kama mitatu iliyopita pale uwanja wa ndege akitokea nje ya nchi na tulifuatana naye hadi kwake, Magomeni Mapipa (wakati huo). Tulifanya upekuzi nyumbani kwake lakini hatukupata kitu. Wananchi wamekuwa wakitupa taarifa kuwa amekuwa akifanya biashara hiyo ndiyo maana tulimkamata na kumpekua,” alisema Nzowa.

DCP Boaz.

Kamanda Nzowa alisema anaamini kuwa katika serikali hii ya Rais Magufuli ‘JPM’ vigogo wengi wanaojihusisha na biashara hiyo watakimbilia nje ya nchi maana kumekuwa na ushirikiano mkubwa wa vyombo vya dola.

UWAZI LATINGA KILWA ROAD
Jumamosi iliyopita, Uwazi lilifika makao makuu ya kitengo hicho na kumkuta Kanyau akishikiliwa huku akiendelea kuhojiwa. Mama yake mzazi, dada zake na ndugu wengine walikuwepo.

Mama mzazi wa Kanyau alisikika akisema anashindwa kulala kwa sababu ya kukamatwa kwa mtoto wake huyo. Alidai kwamba hawezi kula bila kumuona mwanaye ndiyo maana amekuwa akifika hapo kwa lengo la kula naye, pia kuona kama kuna uwezekano wa kumuwekea dhamana.

MKUU WA KITENGO NA UWAZI
Uwazi lilizungumza na Kamishna Msaidizi wa Polisi, Robert Boaz ambaye amechukua nafasi ya Nzowa. Boaz alikiri kukamatwa kwa Kanyau na kusema bado anaendelea kuhojiwa na upelelezi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.

“Nisingependa kuzungumzia suala la Kanyau kwa kipindi hiki maana upelelezi bado unaendelea na kuna uwezekano wa kutoa taarifa zaidi kwa vyombo vya habari, lakini sisi kama jeshi la polisi tunaomba ushirikiano wa karibu na wananchi kuwafichua watu wote wanaojihusisha na biashara hii haramu.

“Mlango wangu upo wazi saa zote hivyo nawaomba raia wema wajitokeze kutupa taarifa zitakazosaidia katika mapambano dhidi ya wanaojihusisha na madawa ya kulevya. Tunaahidi hakuna siri itakayotoka kwa watakaotupa ushirikiano,” alisema Kamanda Boaz.

BAADHI YA VIGOGO POLISI WATAJWA
Habari zilizolifikia gazeti hili wakati linakwenda mitamboni zinadai kuwa baadhi ya vigogo wa jeshi la polisi wamekuwa wakitajwa kujihusisha na biashara ya kuuza unga huku wengi wao wakikamatwa, wengine wakiamua kuacha kazi wenyewe.

“Hao wanaokamatwa kwa kuhusishwa na biashara ya unga, ujue wapo na baadhi ya viongozi wa polisi. Kuna waliokamatwa, lakini wengine sasa kwa kuona hali mbaya wameamua kuacha kazi wenyewe,” kilisema chanzo chetu kimoja kutoka jeshi hilo.
Habari hii inaendelea kufuatiliwa.
25

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...