Sunday, January 24, 2016

MANJI:TIBOROHA ALIFICHA BARUA ZA NIYONZIMA!

Mwenyekitiki wa Klabu ya Yanga Yussuf Manji akionge mbele ya wanachama wa klabu hiyo na Waandishi wa habari hawapo pichani.
JANA mwenyekiti wa Klabu ya Yanga SC, Yussuf  Manji alikutana na waandishi wa habari katika makao makuu ya klabu ya Yanga kwa ajili ya kutoa ufafanuzi juu ya sakata la kujiuzulu kwa Katibu Mkuu wa klabu hiyo pamoja na kutoa taarifa ya maandishi ya sababu za kung’oka kwa Dr. Jonas Tiboroha.

Yapo mengi lakini hizi ndiyo baadhi ya sababu ambazo zimetolewa na uongozi wa Yanga kwa maandishi zikianinisha sababu za Dr. Tiboroha kuondoka kwenye klabu ya Yanga.

Ktibu ametajwa kama ndiye ambaye alisababisha au alitoa sababu za uongo kuhusu suala la Haruna Niyonzima. Taarifa alizokuwa akizipata zilikuwa hazifiki kwenye kamati ya utendaji, kamati ya nidhamu ambayo ilikaa haikupata ushirikiano mwisho wa siku kamati ikaamua kuchukua uamuzi ambao baadaye wakaja kuuona kwamba haukuwa sahihi kwasababu katibu alikuwa amekalia baadhi ya taarifa muhimu.

Sababu nyingine iliyotolewa ni kwamba, katibu hakuweza kufikia malengo ambayo aliwekewa. Wakati anaikuta Yanga ilikuwa inatumia bajeti ya Tsh. 500 kwa mwaka lakini sasahivi Yanga inatumia karibu bilioni 2 kwa mwaka. Katibu kashindwa kuongeza mapato ya klabu ya Yanga kwahiyo ameshindwa kuitumia nafasi yake vizuri.

BDF ya Botswana ilianzima US$ 5,000/- ambazo hadi sasa hazijarejeshwa: EXCOM iligundua taarifa kuhusiana na deni hili, imekuwa ikifichwa na hakuna maelezo mrejesho kuhusiana na hilo kutoka kwa Tiboroha ambaye amekuwa na ukaribu na wahusika kutoka Botswana.

Manji akasisitiza kuwa Tiboroha alikuwa ni mwajiriwa, kwahiyo mwajiri wake anao uwezo wa kusitisha kibarua chake wakati mwingine hata watu wasijue kwanini.

Sababu nyingine iliyotajwa ni kwamba Katibu alikuwa najiendeleza binafsi kuliko taasisi. Alionekana kutaka kujiendeleza binafsi kusikika peke yake na kujulikana mwenyewe kama Mungu mtu jambo ambalo lilichochea kelele ndani ya klabu kama vile yeye ni malaika.

Hakufuata ushauri aliopewa na wataalamu wa TRA, hali iliyosababisha akaunti za Yanga kufungwa, hivyo mimi kulazimika kuanza kutoa fedha zangu za mfukoni katika uendeshaji wa Klabu kwa kipindi chote na wakati huo wachezaji walikuwa wakidai mishahara na tuko katikati ya msimu.

Katibu kushirikiana na TFF katika masuala mengi ambayo Yanga kama klabu ilikuwa inapinga, Katibu alikuwa anaonekana kui-support TFF. Alisahau kama yeye ni mwajiliwa wa klabu ya Yanga. Lile la kushindwa kumpigania msemaji Msemaji wa Klabu, Jerry Murro asifungiwe na TFF, huku akimchimba huku akijua alikuwa akipitia taarifa zote kabla ya Jerry kuzitoa. Alikuwa na roho mbaya kwa kuwa Jerry alipata umaarufu zaidi kwa wanachama kutokana na kuipigania klabu.

Kuna madai kwamba klabu ya Yanga ilipata mwaliko kutoka FIFA kwenda semina Ghana lakini Katibu akajipitisha mwenyewe kwamba ataenda kuhudhuria yeye bila kamati ya kukaa na kuamua nani ataiwakilisha.

Ngoma alipewa taarifa na Tiboroha kwamba anatakiwa kwenda kufanya majaribio na klabu moja nchini Uturuki. Tiboroha alifanya hivyo akijua Ngoma alikuwa anakwenda kushiriki michuano ya MAPINDUZI Cup, mbaya zaidi hakuwa amewasiliana na EXCOM kuhusiana na hilo kabla kumfahamisha mchezaji na kumpa taarifa hiyo.

Baadaye kocha Kocha Mkuu, alilalamika kwamba kufanya vile ilikuwa ni kuondoa morali ya mchezaji katika michuano hiyo ya MAPINDUZI CUP na baada ya hapo, angekuwa akiwaza kuhusiana na Uturuki tu. Mwisho, kocha alisema, Ngoma alicheza chini ya kiwango katika michuano hiyo, akiamini Yanga inamzuia kusonga mbele kimaisha.

Taarifa hiyo pia inaonesha kwamba, Katibu alimwajiri daktari ambaye alihudumu mechi dhidi ya Mgambo lakini baadaye ikagundulika kwamba daktari huyo alikuwa ni mwanachama anayemiliki kadi ya Simba.

Ukiangalia hayo juu, ni kati ya machache ambayo nimeona ninaweza kuyaanika kwenye vyombo vya habari, lakini yako mengi ambayo ni nyeti na haitakuwa sahihi kuyaanika kwenye vyombo vya habari kwa maslahi ya klabu. Yanga ilianza kung’amua mambo yanayomhusu Tiboroha muda sasa, alipoona mengi yamegundulika. Januari 14, 2016 aliandika barua kuomba radhi kwangu, akikiri kufanya makosa na kusema alikuwa akiyajutia.

Sisi, hatukukubaliana na kutoa msamaha kutokana na hofu ya unafiki wake, na nilitoa ushauri; kwamba vizuri akachukua hatua ya kujiuzulu mara moja na huenda ingekuwa vizuri aeleze ana matatizo ya kifamilia pia kiafya, lengo lilikuwa ni kumpa nafasi ya kuachana na Yanga kwa amani pia kuilinda familia maisha yake huko mbeleni. Lakini nilimtaka ahakikishe zile fedha tunazowadai BDF kutoka Botswana, mara moja zinawasilishwa Klabuni na baada ya hapo, rasmi atakuwa amejiondoa.

Tiboroha alikubaliana na hilo na kuandika barua ya kujiuzulu alioiwasilisha Januari 22, 2016.

Pamoja na kumshauri ili ajiuzulu kwa heshima, lakini alionekana kuanza kutengeneza “Presha ya wanachama” kama vile mtu aliyeonewa. Kuna mkutano wa ujanjaujanja uliitishwa makao makuu ya Klabu, Tiboroha akiwa mshiriki mkuu nyuma ya pazia, hii ilikuwa ni Januari 23, 2016. Lengo ni kutengeneza hali ya hofu kwa Wanachama, jambo ambalo si sahihi.

Kwa yote hayo hapo juu: Kamati ya Utendaji (EXCOM) inapenda kutoa taarifa kuwa imevunja mkataba wa Tiboroha kama Katibu Mkuu wa Yanga.

Inaonekana kulikuwa na fukuto la muda mrefu kati ya Katibu na uongozi wa juu wa klabu hiyo na kulikuwa na sababu nyingi za kumng’oa katika kiti hicho lakini sakata la Haruna Niyonzima limekuwa kama chambo au chanzo cha Katibu huyo kutimka kunako mtaa wa Jangwani.

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...