Saturday, January 23, 2016

KUMBE NIYONZIMA NDIYE MSAJILI WA KAMUSOKO!


Kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima.

SIRI imefichuka, kwamba kiungo wa Yanga, Haruna Niyonzima, ndiye aliyefanikisha usajili wa nyota Thabani Kamusoko kujiunga na timu hiyo kutoka FC Platinum ya Zimbabwe.
Wote wawili wakawa sehemu ya kikosi cha kwanza cha Yanga mwanzoni mwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara na kuipa timu yao matokeo mazuri ikiwemo ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Simba.

Haruna Niyonzima, akiongea na Thabani Kamusoko (kushoto mwenye jezi namba 13)
Upepo ulibadilika Desemba, mwaka jana baada ya Niyonzima kuchelewa kurejea kutoka kwao Rwanda alipokwenda kuitumikia timu ya taifa iliyoshiriki Kombe la Chalenji, Ethiopia.
Kamusoko, raia wa Zimbabwe, akaonekana kimbilio jipya kwa mashabiki wa Yanga huku ikionekana kuwa anaweza kubeba majukumu yote ya Niyonzima ambaye alisimamishwa na kusitishiwa mkataba wake na uongozi kwa kosa hilo la kuchelewa kurudi.
Hata hivyo, Niyonzima alimalizana na uongozi kwa utetezi kuwa kuchelewa kwake kulitokana na majeraha aliyopata wakati akiitumikia Rwanda.

ALIVYOMSAJILI KAMUSOKO
Bosi mmoja mwenye nguvu kubwa katika mambo ya usajili ya Yanga ambaye hakutaka kutajwa jina, aliliambia Championi Jumamosi: “Niyonzima ndiye aliyefanikisha usajili wa Kamusoko, yeye ndiye aliyeleta wazo la kwanza kuhusu mpango huo.
Wachezaji wa timu ya Yanga wakiendelea na mazoezi.

“Alitueleza wazi kwamba anamjua vizuri Kamusoko kwani amekutana naye mara kadhaa katika mechi kuanzia wakiwa timu za taifa za vijana hadi sasa katika timu za wakubwa.
“Sasa wakati ule tulipocheza na Platinum ndipo alipotueleza kuhusu umuhimu wa Kamusoko, nasi tukamfuatilia na kujiridhisha halafu tukamsajili na kweli sasa anaisaidia timu.”

NIYONZIMA, KAMUSOKO WAFANYA KIKAO
Akiripoti mara ya kwanza katika mazoezi baada ya kusamehewa na uongozi, jana Ijumaa asubuhi kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, Niyonzima alitumia muda mwingi kuzungumza na Kamusoko.
Niyonzima na Kamusoko walitumia zaidi ya dakika sita katika mazungumzo hayo na kuwa marefu kwa kiungo huyo kuliko alivyozungumza na wachezaji wengine wote.
“Kurejea kwa Niyonzima kumeniongezea nguvu mimi na timu nzima, huyu ni mtu mzuri, unapocheza naye kikosini mambo huwa mazuri, namjua muda mrefu kabla ya kukutana naye Yanga na ni mtu mzuri,” alisema Kamusoko.
Kwa upande wake Niyonzima, alisema: “Namjua vizuri Kamusoko, nimecheza naye kuanzia timu za vijana na zile za wakubwa tukiwa wapinzani na sasa tupo pamoja Yanga, nathamini uwezo wake.”
Kamusoko ameonyesha uwezo mkubwa akiwa na Yanga wakati huu kwa umahiri wake wa kutoa pasi za mwisho na ufungaji na kuiwezesha timu yake kuwa kileleni mwa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 39 katika mechi 15.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...