Na Wilbert Molandi
Dar es SalaamWINGA wa Yanga,
Simon Msuva anaendelea vizuri na majaribio katika kikosi cha Bidvest
Wits ya Afrika Kusini, uongozi wa timu yake umesema kama akifuzu upo
tayari kumuuza kwa dau la dola 700,000 (zaidi ya Sh Bilioni 1.3).
Yanga imeamua kukata mzizi wa fitina baada ya Msuva kutoroshwa
katikati ya wiki hii kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio katika klabu
hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Afrika Kusini (PSL).
Msuva ambaye mkataba wake unafikia tamati msimu ujao, leo anamaliza
majaribio na kurejea nchini usiku na kama akifuzu atakuwa ameitajirisha
klabu yake ambayo tayari imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambapo leo
inakamilisha ratiba kwa kucheza na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda
Sijaona, Mtwara.
Winga huyo aliyesajiliwa na Yanga misimu miwili iliyopita akitokea
Moro United, sasa anasubiri tuzo yake ya ufungaji bora kwani hadi sasa
amefunga mabao 17 akifuatiwa na Amissi Tambwe aliyefunga 17. Hata hivyo,
Tambwe anaweza kuongeza mengine leo katika mchezo dhidi ya Ndanda.
Kama Msuva akifanikiwa katika majaribio yake anaweza kumtoa kikosini
Christopher Katongo raia wa Zambia au Fikru Tefera wa Ethiopia ambao
wanaichezea timu hiyo inayomilikiwa na Idara ya Michezo ya Chuo Kikuu
cha Bidvets maarufu kama Wits.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. Jonas Tiboroha, alilihakikishia Championi
Jumamosi kuwa, kila mchezaji wa kikosi hicho ana thamani yake lakini
wenye viwango vya wastani ni dola 500,000 (Sh milioni 965) na wenye
uwezo wa juu ni dola 700,000.
Hiyo ina maana, Msuva ambaye yupo katika kundi la wachezaji wenye viwango vya juu kikosini kwa sasa ana thamani ya dola 700,000.
“Hatumzuii mchezaji kwenda kuichezea timu nyingine, lakini lazima
klabu inayomuhitaji ifuate utaratibu ili tupate haki zetu, mchezaji
mwenye kiwango cha wastani tunamuuza kwa dola 500,000 na yule mwenye
kiwango cha juu ni dola 700,000,” alisema Tiboroha.
“Pia tuna kigezo kingine ambacho tutakitazama kwamba ni lazima timu
inayomnunua mchezaji wetu iwe inashiriki michuano ya kimataifa, maana
fedha si kila kwetu.”
Endapo Msuva atafanikiwa kujiunga na Bidvest,
atakuwa mchezaji wa pili wa kutegemewa na Yanga aliyeshiriki kikamilifu
kuipa ubingwa msimu huu kuondoka kwani wa kwanza ni Mrisho Ngassa
anayetimkia Free State Stars ya Afrika Kusini pia.
No comments:
Post a Comment