Singida Mashariki ni moja kati ya majimbo ya uchaguzi yaliyopo Wilaya
ya Singida Vijijini mkoani Singida, likiongozwa na Mheshimiwa Tundu
Antipas Lissu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Awali, jimbo hilo lilikuwa likijulikana kama Singida Kusini kabla ya
kugawanywa mwaka 2010 na kupata majimbo mawili, Singida Mashariki na
Singida Magharibi.
Kama ilivyo kawaida, gazeti hili lilifanya ziara kwenye jimbo hilo na
kuzungumza na wananchi walioeleza kero zinazowasumbua na jinsi mbunge
wao alivyotimiza ahadi alizowaahidi alipogombea mwaka 2010.
MATATIZO YA WANANCHI
Katika ziara yake jimboni humo, Uwazi
lilibaini matatizo yanayowakabili wananchi wa Singida Mashariki yakiwemo
kunyanyaswa wakilazimishwa kulipa michango ya ujenzi wa maabara kwenye
shule, ukosefu wa mawasiliano ya simu kwenye baadhi ya maeneo, uchakavu
wa vyumba vya madarasa, uhaba wa walimu, ukosefu wa vifaa vya
kufundishia kwa shule nyingi za jimbo hilo pamoja na vijiji vingi
kutokuwa na nishati ya umeme.
SEKTA YA MAWASILIANO
Wananchi waliozungumza na Uwazi, walisema
suala la mawasiliano limekuwa tatizo sugu kwani sehemu nyingi hakuna
minara ya makampuni ya simu za mikononi, hali inayosababisha wananchi
kukosa mawasiliano au sehemu nyingine kulazimika kupanda milimani au
kwenye miti kutafuta mawasiliano mazuri.
“Yaani ukitaka kupiga simu lazima uangalie sehemu yenye miinuko au
upande kwenye mti ndipo uweze kuwasiliana vizuri, afadhali kipindi hiki
tangu Lissu aingie madarakani tunaona tofauti kwani kampuni za simu
zimeanza kujenga minara kuliko ilivyokuwa mwanzo, hali ilikuwa mbaya,
tunaomba aendelee kutupigania tupate mawasiliano mpaka vijijini,”
alisema Suzana Lyantulu, mkazi wa Kijiji cha Makyungi.
SEKTA YA ELIMU
Uwazi lilibaini kwamba, katika jimbo hilo kuna
matatizo mengi katika sekta ya elimu lakini kubwa, ni suala la wananchi
kulazimishwa kuchangia elimu na wakati mwingine kujikuta wakipokonywa
mifugo yao au kulipishwa faini kubwa, jambo ambalo Mheshimiwa Lissu
amekuwa mstari wa mbele kulizuia.
“Tunamshukuru Mheshimiwa Lissu, tulikuwa tunanyanyasika sana kipindi
cha nyuma, tunalazimishwa kuchangia elimu kwa nguvu wakati fedha
tunazotoa zinaishia kwenye mifuko ya wajanja wachache.
“Mbunge wetu akaingilia kati na kutukataza kuchangia pesa zozote
mpaka tuambiwe kwanza tulizochanga awali zimefanya kazi gani. Kwa kweli
Lissu ni mpiganaji na ametimiza ahadi yake ya kukomesha michango kama
alivyoahidi wakati akiomba kura,” alisema Nicodemus Kachenje mkazi wa
jimbo hilo.
SEKTA YA AFYA
Wakigusia kero za afya, wakazi wa jimbo hilo walisema viongozi wengi wa
serikali wanaendekeza ufisadi kiasi cha kusababisha majengo ya zahanati
kama Kimbwi, ujenzi wake kusimama baada ya fedha zilizochangwa na
wananchi kutafunwa na wajanja.
“Tunashukuru mbunge wetu ameingilia kati na kusema tusichange tena
fedha zozote mpaka zile tulizochanga tuambiwe kwa uwazi zimefanya kazi
gani, viongozi wengi ni mafisadi huku kwetu,” alisema Cleopa Zakaria.
Kero zingine ni ubovu wa miundombinu zikiwemo barabara nyingi za
jimboni humo ambazo hazina ubora unaohitajika na ukosefu wa umeme katika
baadhi ya vijiji.
MAELEZO YA MBUNGE
Baada ya kusikiliza maelezo ya wananchi, Uwazi
lilimtafuta mbunge wa jimbo hilo, Mhe. Lissu ambaye alisema anazitambua
vyema changamoto za wananchi wake na kueleza jinsi alivyojitahidi
kuzitatua.“Nilipoingia madarakani, mambo mengi yalikuwa hovyo sana
jimboni kwangu, ufisadi, rushwa na unyanyasaji wa wananchi kwa sababu ya
michango ulikuwa mkubwa lakini nimejitahidi kadiri ya uwezo wangu
kuwasaidia.
“Suala la wananchi kulazimishwa kuchangia fedha kwa ajili ya shughuli
za maendeleo halikubaliki kwa sababu hilo ni jukumu la serikali na kila
mwaka bajeti kubwa zinatengwa kwa ajili ya kazi hiyo.
“Wanaokataa kuchanga fedha ni wanaoniunga mkono kwani wakati nawaomba
kura niliahidi kuwafutia michango yote wanayochangishwa na serikali
ambayo inaliwa na watendaji wa serikali za mitaa, hatuwezi kuchanga
fedha wakati serikali ina uwezo wa kujenga maabara na zahanati kama
ilivyoahidi,” alisema Lissu na kuongeza kuwa anawaomba wananchi wake
waendelee kumuunga mkono ili akamilishe mambo yote aliyowaahidi ikiwa ni
pamoja na kuwakomboa kutoka kwenye lindi la umaskini.
No comments:
Post a Comment