Thursday, April 16, 2015

RAFIKI WA LULU ANASWA NA UNGA!

Jamaa ambaye inasemekana ni rafiki wa karibu wa staa mkubwa wa sinema za Kibongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ aitwaye Morris Sekwao ‘Junior’ inadaiwa amepata msala ‘hevi’ baada ya kutiwa mbaroni nchini Nigeria akituhumiwa kunaswa na madawa ya kulevya ‘unga’.Habari kutoka kwa mtu wa karibu wa familia ya Junior zilidai kuwa, jamaa huyo alipatwa na mkasa huo hivi karibuni nchini humo ambapo alikuwa akitokea Bongo na mzigo huo.
Morris Sekwao ‘Junior’ akiwa na sanduku la madawa ya kulevya aina ya Ephedrine alilokutwa nalo.
AKAMATWA UWANJA WA NDEGE NA KILO 25
Chanzo hicho kilidai kwamba Junior alikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Murtala Muhammed (MMIA) uliopo Ikeja, Lagos nchini Nigeria, akiwa na madawa hayo aina ya Ephedrine yenye uzito wa kilo 25.Ilidaiwa kwamba Junior ambaye ni rafiki wa mastaa mbalimbali Bongo, alidakwa na polisi wa uhamiaji uwanjani hapo baada ya kutilia shaka begi kubwa alilokuwa amelibeba.
NI BEGI ZIMA
Ilidaiwa kwamba, baada ya ukaguzi alikutwa na begi zima la unga wenye ujazo huo wa kilo 25 ambao thamani yake haikuwekwa wazi mara moja.
KAMA MASOGANGE
Chanzo hicho kilizidi kumwaga ‘ubuyu’ kwamba aina ya madawa aliyokamatwa nayo ni kama yale aliyokamatwa nayo video queen wa Bongo, Agness Gerald ‘Masogange’ nchini Afrika Kusini ‘Sauzi’ mwaka 2013.
Morris Sekwao akiwa na Lulu.
BOSI YULEYULE
Madai mazito yalishushwa kwamba ‘doni’ aliyembebesha mzigo (aliyemfanya punda) Junior ndiye yuleyule aliyedaiwa kumbebesha Masogange.Ilisemekana kuwa baada ya kukamatwa, uchunguzi wa kipolisi unaendelea nchini humo ambapo kwa sheria za Nigeria, jamaa huyo akikutwa na hatia anaweza kwenda jela miaka kadhaa.
NDUGU WAHAHA
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba kukamatwa kwa Junior kumewashtua baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki zake kwa kuwa hawakuwa wanajua kama ndugu yao huyo anafanya kazi hiyo.
KAMANDA NZOWA AFIKISHIWA TAARIFA
Kamanda wa Kikosi cha Kupambana Dawa za Kulevya Bongo, Godfrey Nzowa alipoulizwa juu ya taarifa za kukamatwa kwa kijana huyo alisema hajazipata lakini aliahidi kufuatilia ili kupata undani wake.
Kamanda wa Kikosi cha Kupambana Dawa za Kulevya Bongo, Godfrey Nzowa.
KUHUSU JUNIOR
Habari zilizo kwenye makabrasha ya gazeti hili zinaeleza kuwa Junior ni mtoto wa mjini ambaye mara nyingi hupenda kuambatana na wasanii mbalimbali Bongo ambapo mara nyingine husafiri nao nje ya nchi bila kujulikana anapiga dili gani.
NDIYE ALIYEMKIMBIZA LULU USIKU WA KIFO CHA KANUMBA?
Ilidaiwa kwamba usiku wa kuamkia Aprili 7, 2012 ambapo ndiyo siku kilitokea kifo cha aliyekuwa mwigizaji mkubwa Bongo, marehemu Steven Kanumba, Junior ndiye aliyedaiwa kumkimbiza Lulu kutoka nyumbani kwa Kanumba na kwenda naye kwenye Ufukwe wa Coco kabla ya kukamatwa alfajiri yake maeneo ya Bamaga-Mwenge jijini Dar.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...