Thursday, April 16, 2015

HOFU YA BOMU YATIKISA CHUO KIKUU DAR

WAKATI hofu ya ugaidi wa Kundi la Al Shabaab la Somalia ikiwa bado imetanda kufuatia mauaji ya wanafunzi 146 wa Chuo Kikuu cha Garissa nchini Kenya, hisia za kuwepo kwa bomu imewakumba watu mbalimbali pamoja na wasomi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, baada ya kitu kilichodhaniwa kuwa bomu kukutwa katika kituo cha mabasi ya daladala kijulikanacho kama Kontena, kilichomo eneo la chuo hicho.
Kitu kilichodhaniwa kuwa ni bomu kikitolewa kwenye mfuko.
Tukio hilo lilitokea mchana wa Aprili 14, mwaka huu ambapo wanafunzi hao walionekana kuushangaa mfuko mweusi uliokuwa pembeni ya kituo hicho, ambao ndani yake kulionekana kiboksi cheusi, kilichowafanya kuamini kuwa ni bomu.
Waandishi wetu waliokuwa wakipita eneo hilo, waliwataarifu walinzi wa chuo hicho, ambapo mmoja wao alienda kushuhudia mfuko huo. Kabla ya kuufikia, aliwatawanya wanafunzi waliokuwa wametaharuki na kuusogelea, lakini hofu ya mlipuko ilimfanya asiuguse, badala yake akaenda kutoa taarifa kituo cha polisi chuoni hapo kwa ajili ya msaada zaidi.
Muonekano wa kitu hicho baada ya kutolewa mfukoni.
Katika kituo cha Polisi Chuo Kikuu, askari aliyejitambulisha kwa jina la Sajenti Buwa, aliambatana na mlinzi huyo hadi eneo la tukio na kwa ujasiri wa aina yake, polisi huyo aliufungua kwa tahadhari mfuko huo na kubaini kuwa halikuwa bomu, bali ni betri ya pikipiki iliyozungushiwa nyaya.“Hii ni betri ya pikipiki, hapa hamna kitu, hili siyo bomu lakini hili siyo la kupuuza, aliyeweka alidhamiria kitu...,” alisema Sajenti huyo.
Waziri wa Mambo ya Nje, Habari na Mawasiliano wa Umoja wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), Joseph Nyalomba, alikiri kupata taarifa za kuwepo kwa kitu kilichosadikiwa kuwa ni bomu.
“Tulisikia uvumi huo, lakini niliwasiliana na watu wa usalama wakasema kuwa ilikuwa ni betri ya pikipiki iliyotelekezwa na mtu asiyejulikana.
Chuo kikuu cha Dar es salaam.
Nawatoa hofu wanafunzi kuwa, ulinzi wa chuoni tumejitahidi kuuimarisha hivyo wasiwe na hofu, zaidi nawataka wawe walinzi wao kwa wao na kuripoti mara moja kwa watu wa usalama wakiona jambo tofauti,” alisema waziri huyo.
Imeandaliwa na Chande Abdallah, Issa Mnally, Shani Ramadhani, Mayasa Mariwata na Deogratius Mongela

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...