Friday, April 17, 2015

KATIBA INAYOPENDEKEZWA NI KIVULI CHA ‘KATIBA YA NYERERE’

Tundu Lisu.
UKITAKA kuwaudhi Watanzania wengi – wasomi na wajinga, wafupi na warefu, walevi na wasiotumia vileo  – unachotakiwa kufanya ni kutaja makosa aliyoyafanya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Julius Kambarage Nyerere akiwa madarakani.
Tundu Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki, katika mijadala ya kuweka mambo sawa kitaifa, aliposema: “Nyerere hakuwa  Mungu” akimaanisha yaliyofanywa na kusemwa na Nyerere hayakuwa msahafu, alisakamwa na watu kibao kwa kusema ukweli wa wazi hata kwa mtoto mdogo!
Wanaoisoma safu hii wakiwa wamenuna wafahamu kwamba Nyerere alikuwa kiongozi wa nchi hii hivyo historia aliyoiacha itasemwa na Watanzania kwa miaka nenda-rudi.
Nyerere atazungumziwa sana kwa vile alituachia urithi wa mambo mengi yakiwemo ambayo leo yanaendelea kutukosesha furaha ya kweli kisiasa na kiuchumi na ambayo warithi wake wanayatumia kupitia jina lake.

Katiba ya sasa ya mwaka 1977 iliyotungwa wakati wa utawala wake, ambayo wengi wanaiita ‘Katiba ya Nyerere’, ndiyo chimbuko la matatizo mengi ya kisiasa yanayoendelea kuleta giza na kuwakosesha Watanzania wengi tabasamu la kitaifa.
Katiba hiyo iliandikwa na watu wachache na kupitishwa na watu wachache kwa kivuli cha bunge, wakati huo likiwa na wabunge wa Chama Cha Mapinduzi  (CCM) tu!    Heshima na woga wa Watanzania kwa kiongozi wao huyo viliwafanya  ‘wakubali yaishe’ na katiba hiyo ikaanza kutumika hadi leo!
Kabla ya katiba hiyo ya 1977, kulikuwa na katiba zenye sura hiyohiyo ya kukidhi utawala wa serikali yake ya chama kimoja – baada ya kuvipiga marufuku vyama vingine vya siasa mwaka 1965! Nyerere kama binadamu na wanasiasa wengine alikuwa hakosi maajabu!
Alikuwa anakiri kwamba katiba aliyokuwa anaitumia ilikuwa ya kidikiteta, na kwamba ilikuwa inatoa mwanya kwa mtu yeyote kuitumia na kuendesha nchi kidikteta.  Ajabu ni kwamba aliendelea kuitumia katiba hiyohiyo mpaka anaondoka madarakani mwaka 1985!  Kwa wasiokumbuka, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliitawala Tanzania kwa miaka ipatayo 25!
Kwa Nyerere kukiri kutumia katiba ya kidikteta, watu waliokuwa wanampenda na kumwogopa, walitegemea katiba hiyo ingekoma baada ya yeye kuachia madaraka na hivyo kutoa mwanya wa kuandikwa katiba mpya isiyokuwa ya kuogopana wala kutishana.
Lakini haikuwa hivyo! Aliondoka na kuiacha ikaendelea kutumiwa na ‘waliopokea  kijiti’ kutoka kwake ambapo maudhui yake yameingizwa katika Katiba Inayopendekezwa.Kama enzi ya Nyerere, Katiba Inayopendekezwa inampa rais madaraka ya kifalme ya kuteua viongozi wote muhimu wa kitaifa kuanzia wilayani na mikoani, mawaziri, makatibu wakuu wa wizara, wakuu wa majeshi ya ulinzi na polisi, usalama wa taifa, wakuu wa mashirika na taasisi za umma na kadhalika.
Miongoni mwa taasisi nyingi anazoteua viongozi wake ni pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi!  Hilo ndilo chimbuko kubwa la mikanganyiko yote ya maisha ya kisiasa katika dhamira ya kujenga demokrasia ya kweli ya umma.
Christopher Mtikila.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kuwa chini ya ‘ajira’ ya rais ambapo wajumbe wake wanajua rais ndiye mwenye uwezo wa kuwafukuza kazi.Kwa kifupi, katika mfumo huu, watumishi wote wa taasisi za umma, wanaoteuliwa na rais  wataendelea kuwajibika kwa rais ambaye kimsingi ndiye mwajiri wao -- si wananchi!
Kumlimbikizia madaraka rais ni kuendelea kuyaweka maisha ya wananchi chini ya ghilba na utashi wa wanasiasa badala ya kuwapa wananchi uwezo wa kuchagua wakuu wa wilaya na mikoa sehemu zao.
Mfano wa ghilba za wanasiasa kuhusu ‘Katiba ya Nyerere’ ni kuhusu mgombea binafsi.
Katiba hiyo ya 1977 ilikuwa na kifungu kilichoruhusu wagombea binafsi wa nafasi zote za kisiasa, bila kulazimika kuwa katika chama chochote. Kifungu hicho kilikuwepo  ‘kimyakimya’ bila kutumiwa, na bila wananchi kuambiwa kwamba kipo.
Baada ya mfumo wa vyama vingi kuanza, kiongozi wa Democratic Party, DP, Christopher Mtikila, alieleza nia ya kutumika kwa kifungu hicho, jambo lililopingwa bila sababu za msingi na wanasiasa waliokuwa madarakani hadi likafika mahakamani.
Kwa vile lilikuwemo katika katiba, mahakama bila kusita ilikubaliana naye.  Lakini katika maajabu ambayo yamekuwa yakifanywa na wanasiasa wa nchi hii,  bunge la CCM lilifanya mabadiliko ya dharura, mabadiliko ya 11 ya Katiba katika Ibara ya 34 na kukifuta kifungu hicho kilichoruhusu wagombea binafsi!
Tendo hilo lilifanyika Nyerere akiwepo, na hakusema lolote, licha ya kuwa alikuwa amesisitiza kifungu hicho kitumike katika siasa za vyama vingi alipohutubia mkutano wa Siku ya Wafanyakazi mjini Mbeya!
Katiba Inayopendekezwa imeridhia wagombea binafsi lakini kwa masharti magumu ajabu! Kwa nini? Hizo ndizo ghilba za wanasiasa.
Miaka 35 tayari imepita tangu ‘Katiba ya Nyerere’ ilipoanza kutumika katika juhudi za kuimarisha utawala wa chama kimoja ambapo nguvu na hatamu zote za kuongoza maisha ya watu zilikuwa mikononi mwa mtu mmoja.
Kuendelezwa kwa ‘maudhui’ ya Katiba ya 1977 – leo mwaka 2015 – kwa ghilba za kupitia Katiba Inayopendekezwa, ni kufungua mlango ambao wanaosimamia ghilba hizo watakuja kuleta majanga kwao na kwa wananchi wenzao na kuishia kujuta!
Kuwarudisha Watanzania katika siasa za miaka 35 iliyopita ni kuwaonea na ni dhambi.
Umefika wakati kwa viongozi kuwaogopa wananchi ambao ndiyo waajiri wao na si wananchi kuwaogopa viongozi! Hapo ndipo tutakapojenga jamii ya kutolipiziana  visasi katika kupeana ‘vijiti’ vya kisiasa. Wahenga walisema: Majuto ni Mjukuu!

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...