Msanii nguli wa muziki wa kizazi kipya na nyota wa Wimbo wa Nitampata
wapi aliyewahi kuwa mchumba wa Wema Sepetu, Nasibu Abdul ‘Diamond’
amenusurika kukatwa mguu katika Hospitali ya TMJ, Mikocheni jijini Dar
es Salaam kufuatia ugonjwa wa Foot Corn (maarufu kwa jina la kisahani)
kumtesa kwa kipindi kirefu.
Kwa mujibu wa chanzo chetu makini, Diamond ambaye kwa sasa anaminya
kimalavidavi na mwanamama Zarina Hassan ‘Zari’, alianza kusumbuliwa na
ugonjwa huo takribani siku 730 zilizopita (miaka miwili), huku mwenyewe
akipuuzia matibabu yake na kuelekeza nguvu kwenye shoo za ndani na nje
ya nchi.
“Mara kwa mara alikuwa akilalamikia maumivu makali ya mguu
lakini kwa kuwa yalikuwa yakija na kupotea, alikuwa akipuuzia kwenda
hospitali mpaka juzi (Ijumaa) alipoamua kwenda TMJ,” kilisema chanzo
chetu kwa masharti ya kutotajwa jina.
WALICHOKIBAINI MADAKTARI
“Madaktari walipompima, walishangazwa na jinsi alivyokuwa amechelewa
kwenda kupata matibabu, nasikia ugonjwa aliokuwa nao ni hatari sana.
Kama angeendelea kuchelewa, huenda wangelazimika kumkata mguu kabisa,
Diamond aliogopa sana,” kilisema chanzo hicho.
Ikazidi kuelezwa kuwa
baada ya vipimo kukamilika na kubainika kuwa alikuwa na Foot Corn,
madaktari walimueleza kuwa ni lazima wamfanyie upasuaji wa haraka wa
kutoa nyama zilizokuwa zimeota kwenye mguu wake ambazo zilitengeneza
kitu kama kisahani.
NDANI YA CHUMBA CHA UPASUAJI
Baada ya taratibu
zote kukamilika, Diamond aliingizwa ndani ya chumba cha upasuaji ambapo
jopo la madaktari kadhaa, wakiwemo wenye asili ya Bara la Asia
walimfanyia upasuaji.
SHOO NYINGI ZILISABABISHA ACHELEWE MATIBABU
Kwa mujibu wa chanzo kingine ambacho ni ndugu wa msanii huyo, sababu
iliyosababisha Diamond akachelewa kwenda hospitali kutibiwa tatizo hilo,
ni kubanwa na shoo nyingi ambapo alikuwa akihofia kwamba akienda
hospitali anaweza kulazwa au matibabu yakachukua muda mrefu hivyo
kuvuruga mikataba ya shoo ambayo tayarti alikuwa ameshasaini.
MSIKILIZE DIAMOND
Baada ya kukamilika kwa upasuaji huo, mwanahabari wetu aliyekuwa
akifuatilia tukio zima kuanzia mwanzo hadi mwisho, alizungumza na Mbongo
Fleva huyo ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Nawashukuru sana
madaktari wa TMJ kwa kuweza kufanikisha upasuaji huu, Mungu awabariki
sana. Ugonjwa ulianza kama miaka miwili hivi iliyopita lakini
nilishindwa kufanya upasuaji kwani shoo zilikuwa zinabana, safari hii
nikaona bora tu nifanye maana niliambiwa nikiacha tatizo linaweza kuwa
kubwa zaidi,” alisema Diamond.
MSIKIE DAKTARI BINGWA WA UPASUAJI
Ijumaa Wikienda halikuishia hapo, lilimtafuta Dk. Edward Wayi, Daktari
Bingwa wa Upasuaji wa Hospitali ya CCBRT ambaye pia huzunguka katika
nchi mbalimbali za Afrika kutibu watu ambapo aliufafanua ugonjwa huo
kitaalamu.
“Ugonjwa wa Foot Corn unapokuanza, dalili za awali ni maumivu makali ya mguu ulioathirika.
“Ugonjwa usipotibiwa, husababisha malengelenge ambayo hupasuka na
kusababisha kidonda. Kidonda hicho kisipotibiwa, husababisha kuharibika
kwa ngozi ya ndani ya mguu inayotenganisha mifupa ya mguu na ngozi ya
ndani. Hali hii kitaalamu huitwa Bursitis.
“Mgonjwa akishafikia hatua hii, huwa kwenye hatari ya kupata tatizo
lingine kubwa zaidi liitwalo Septic Arthritis ambapo bakteria huingia
ndani ya mwili kwa kupitia kidonda, kusambaa kwenye mfumo wa damu na
kwenda kujikusanya kwenye viungio vya mifupa (joints).
“Mgonjwa
akifikia hatua hii, viungio vya mifupa huvimba na kupata maumivu makali
mithili ya mtu anayechomwa na sindano au msumari. Hata hivyo, kwa kuwa
maumivu huwa yanakuja na kukata, wengi hupuuzia na matokeo yake, ugonjwa
huingia kwenye hatua ya hatari zaidi iitwayo Osteomyelitis.
“Katika hatua hii, bakteria huwa tayari wamepanda na kuingia ndani ya mfupa kisha kuanza kuushambulia kwa kasi.
Mgonjwa akishafikia hatua hii, huwa hakuna tiba nyingine zaidi ya mguu
kukatwa. Nawashauri Watanzania kutopuuzia ugonjwa huu kwani tayari watu
wengi wameshakatwa miguu kwa sababu ya kuchelewa kupata matibabu,”
alihitimisha daktari huyo.
No comments:
Post a Comment