Kwa sasa tunapozungumzia mastaa wa muziki wanaofanya vizuri hapa
Bongo, jina la Nasibu Abdul ‘Diamond’ lazima litachukua nafasi ya kwanza
kisha wengine watafuata. Ni kijana anayejituma sana na jitihada zake
hizo zimemfanya awe maarufu barani Afrika.
Nyuma ya mafanikio ya Diamond wapo watu wengi. Mwenyewe amekuwa
akimshukuru sana mama yake, Sanura Kassim ‘Sandra’ kwa malezi aliyompa
hadi kufikia hapo alipo leo. Ukimuacha mama yake, wapo watu wengine
wengi lakini leo nataka kukupa angalau kwa uchache uhusiano uliopo kati
ya Diamond na DJ wake, Romy Jones.
Katika safari ya kimuziki, Diamond na Romy wametoka mbali sana. Kwa
wasiojua, wawili hawa ni ndugu kabisa, ni mtu na kaka yake kwa upande wa
mama zao. Yaani mama wa Diamond na mama wa Romy ni mtu na dada yake.
Mwandishi wa makala haya, alipata nafasi ya kuzungumza na Diamond juu maisha yake na Romy enzi za utoto wao, soma hapa chini…
Maisha ya utotoni
Diamond: “Awali Romy alikuwa akiishi Kinondoni
kwa baba yake lakini kila wikiendi alikuwa anakuja Tandale, tunakula
‘good time’ kisha anaondoka. Ikafika kipindi baba yake akafariki na hapo
ndipo mama wa Romy alipolazimika kurudi kwao, Tandale akamkuta dada
yake (mama Diamond) akiwa na mimi. Hapo ndipo tukakua na kucheza pamoja.
“Hakuna sehemu ambayo ungemkuta Romy bila mimi kuwepo. Yalikuwa ni
maisha f’lani ambayo natamani yajirudie. “Ukweli Romy alikuwa ni mkubwa
kwangu lakini tuliishi kama mapacha licha ya kwamba Romy alikuwa mtundu
kuliko mimi.
Ishu ya shule ikawaje?
Kwa namna tulivyokuwa ilikuwa ngumu kupelekwa shule tofauti, tulisoma shule moja kuanzia shule ya msingi hadi sekondari.
Ubishoo ilikuwa
tangu utotoni
“Unajua sisi wazazi wetu
walikuwa wa kisasa, walikuwa wanajua kutuvalisha vizuri na ndiyo maana
picha nyingi za utotoni cheni, raba, jinzi na tisheti za kijanja kama
kawa. Kwa hiyo huu usafi hatukuuanzia juzi wala jana, sisi tangu ‘long
time’ kitambo.”
Walichopendelea zaidi
“Enzi hizo tukiwa wadogo hatukujua kama
tutakuja kufanya muziki, tulifanya mambo mengi ya kitoto tu. Tulikuwa
tunacheza sana mpira kama ilivyo kwa watoto wengine.”
Muziki ilikuwaje?
“Wakati tuko wadogo, nakumbuka kuanzia tukiwa
shule ya msingi, mama yangu alikuwa akitupeleka sana kwenye maeneo ya
burudani. Ikitokea kuna mashindano ya kuimba ‘talent show’ alikuwa
akitushika mkono na kutupeleka, huko ndiko tulikoanzia mambo ya muziki.”
Mwanzo wa ustaa
Romy alipokuwa akifanyiwa ‘intaviu’ katika Kipindi cha Sporah hivi
karibuni alisema: “ Wakati nilipoanza kufanya kazi ya utangazaji pale
Clouds, Diamond hakuwa lolote, alikuwa akiniona kwenye TV, yeye bado
anapambana na maisha ya uswahilini huku akifanya muziki.
“Wakati mimi naanza kupata zile elfu 10 na zaidi, yeye alikuwa hana hata mia. Nikawa namtoa kimtindo.
“Ikafika kipindi ndiyo nikamtambulisha Diamond kwa watangazaji wenzangu
akiwemo Adam Mchomvu, nikawaambia nina mdogo wangu anaitwa Diamond
anaimba, tunamsaidiaje.
“Tukarekodi nyimbo kibao zikaishia hewani. Kuna moja ya kurap
tukafanya na Gez Mabovu na Gwea (wote marehemu) kisha nikaipeleka
Clouds. Mchomvu alipoisikia akaipenda ikaanza kupigwa, Diamond akawa
anafurahi sana. Safari ya kimuziki ikaanzia hapo na mpaka sasa mimi ni
Official DJ na Tour Manager wa Diamond.
No comments:
Post a Comment