Friday, March 20, 2015

BABA HAJI: KANUMBA AMEONDOKA NA SANAA YA BONGO

NYOTA wa filamu za Kibongo, Haji Adamu Rajabu ‘Baba Haji’ amefunguka kuwa, soko la filamu  Bongo kwa sasa linashuka siku hadi siku  na sababu kubwa ni  wasanii kutopenda kwenda shule kujiendeleza kielimu na kujua ni jinsi gani filamu inatakiwa kutengenezwa.
Nyota wa filamu za Kibongo, Haji Adamu Rajabu ‘Baba Haji’.
Akizungumza na Risasi Jumamosi,  Baba Haji alisema anakubaliana na kila mtu anayesema soko limeshuka kwa sababu wasanii wanapenda kukopi,  pia hawapendi kuandika miswada ya filamu na kupendelea kuingiza mambo ya kizungu, ingawa wengi wanamtaja msanii Steven  Kanumba kuwa ameondoka na soko hilo.
Baba haji anafunguka kama hivi…

Risasi Jumamosi: Vipi, mbona kimya kingi? Soko la filamu limekwenda na Kanumba au unalionaje?

Baba Haji: Tunaweza kusema hivyo, kwa sababu yeye alikuwa anajitoa kwa hali na mali, anatoa pesa zake kwa ajili ya filamu, ni tofauti na wasanii wengine ingawa pia alikuwa akitumia sana ‘media’ kueleza kila anachokifanya.

Risasi Jumamosi: Unadhani ni kwa nini wasanii wengi wanapenda kufanya kazi na Wanaigeria?
Baba Haji: Kwa sababu wao wanalipwa tu ila nchi nyingine wana sheria kali, kufanya kwao filamu ni mpaka uwe na digrii ya sanaa.

Risasi Jumamosi:  Wewe umejipanga vipi kwa hilo?
Baba Haji: Mimi nimejipanga vizuri kwa sababu nilikwenda Shule Bagamoyo (Pwani) kwa muda wa miaka mitatu na nilifanikiwa kupata diploma ya sanaa, wakati nakwenda shule nakumbuka Kanumba aliniambia napoteza muda kwani soko ndiyo lilikuwa limechanganya ila namshukuru Mungu hata niliporudi sijapotea sana kwa mashabiki.

Risasi Jumamosi: Una kipimo gani kinachoonesha hujapotea?
Baba Haji: Filamu nilizocheza ni nyingi na juzi nimegundua bado nipo baada ya filamu yangu ya Jamila na Pete ya Ajabu kutoka na kupokelewa na mashabiki vizuri mpaka wamelibadili jina langu kwa sasa wananiita Baba Jamila.

Risasi Jumamosi: Matarajio yako ya baadaye ni yapi?
Baba Haji: Mungu akipenda mwezi wa tisa narudi shule  kwa ajili ya kuchukua digrii ya sanaa ambayo nina uhakika itanipeleka mbali zaidi na nimefanikiwa kufungua kampuni yangu inayoitwa Hapa Production ambayo imeandaa filamu yangu ya kwanza ya Mama si Mama itatoka hivi karibuni Mungu akipenda.

Risasi Jumamosi: Unadhani ni kwa nini mnashindwa kupasua anga za kimataifa zaidi ukiacha ishu ya Kanumba kujitolea pesa zake mfukoni?Baba Haji: Nawashauri wasanii wajinoe zaidi kwenye lugha ya kigeni kwani na yenyewe inachangia wao kushindwa kufanya vizuri kwenye soko la kimataifa.
Marehemu Steven  Kanumba enzi za uhai wake.
Risasi Jumamosi: Unaweza kunipatia historia yako fupi ya sanaa tangu ulipoanzia mpaka sasa?
Baba Haji: Nilianza kuigiza 1998, nilianzia kundi lililoitwa Mtanzania ambalo lilikuwa chini ya Chama cha  Mapinduzi (CCM), mwaka 2000 nikaenda Nyota Academia kundi lililokuwa likiongozwa na mwalimu marehemu George Otieno ‘Tyson’, mkurugenzi akiwa ni Singo Mtambalike ‘Richie’.

Sikuishia hapo, mwaka 2002 tulianzisha Kundi la Kamanda Family nikiwa na Richie Mtambalike ambapo tulicheza michezo mbalimbali kisha tukaamua kuanza kucheza filamu ambapo tulicheza filamu ya Masaa 24 tukaona filamu ndiyo mpango mzima.
Mwaka 2003 nilicheza filamu ya Miss Bongo niliyoshirikiana na Aunt Ezekiel, iliyofuata ilikuwa ni Jeraha ya Ndoa, nilicheza na Monalisa.Mwaka 2004 nilikwenda Bukoba (Kagera) ambapo nilichukuliwa na Abantu Vision kwa ajili ya kufanya sinema iliyohusiana na mambo ya HIV ilivyoingia Tanzania. Filamu hiyo ilifanikiwa kuchukua Tuzo ya Ziff kama Filamu Bora ya mwaka 2005.
Mwaka 2010 nilijiunga na Chuo cha Sanaa Bagamoyo ambapo nilisoma mpaka kumaliza mwaka 2013.
Mwaka 2014 nilifanikiwa kucheza filamu nyingi kama vile Barbara, Kitoga, Don’t Cry, Mary Mary, Charles Mvuvi, Mwandishi wa Habari, Jamila na Pete ya Ajabu na Wa Mwisho Wewe.

Mwaka huu ndiyo wa mavuno kwangu kwani nimejiandaa vema kutoa filamu zangu mwenyewe ambazo zitakuwa na changamoto kubwa kwani nimesoma kwa ajili ya kuja kuvifanyia kazi na kuibadili kabisa tasnia ya filamu.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...