Friday, March 20, 2015

MTOTO WA MIAKA 3 BONGO ANAYEFUNDISHA SEKONDARI

MTOTO Nice Valentino mwenye umri wa miaka mitatu na miezi tisa, ambaye ana vitu vingi vya kushangaza, ikiwemo kufundisha wanafunzi wa shule za sekondari, ameibuka ndani ya mjengo wa Global Publishers Ltd, Bamaga-Mwenge akiwa na baba yake mzazi na kuanika maajabu saba ya kushangaza, Risasi Jumamosi linakujuza.
Mtoto Nice Valentino akikokotoa maswali aliyopewa na waandishi.
AJABU LA KWANZA
Kwa mujibu wa baba mzazi wa mtoto huyo, Valentino Swenya, aliyezaliwa katika wilaya ya Kiteto mkoani Manyara, Nice alianza kuandika maneno na namba za Kiingereza akiwa na umri wa miezi sita, jambo ambalo liliwashangaza sana.

AJABU LA PILI
Kadiri alivyokuwa akikua, ndivyo uwezo wake wa kuzungumza kiingereza ulivyozidi, lakini katika hali ya kushangaza, Nice hafahamu kabisa kuzungumza Kiswahili, lugha ya wazazi wake na anapolazimika kuongea, basi huongea kwa shida kama inavyowatokea wageni wanaojifunza lugha hiyo ya taifa.

AJABU LA TATU
Jambo lingine linalowashangaza watu ni juu ya uwezo wake wa kufanya hesabu ngumu, licha ya ukweli kwamba katika maisha yake, hajawahi kusoma hata shule za chekechea.“Kuna wakati niliwahi kumpeleka shule moja ya sekondari ya kata, akawafundisha wanafunzi kufanya hesabu ambazo wao zinawashinda, hebu fikiria hao watoto ni wa kidato cha tatu.

...Akiendelea kufanya swali alilopewa.
Na wakati mwingine wanafunzi wakipita nyumbani kwangu, ninawapa swali lililo sawa na kuwaambia wafanya pamoja, Nice anawahi kumaliza akiwa amepatia, lakini hao wanafunzi wa vidato vya juu wanachelewa huku wakiwa wamekosa,” anasema baba wa mtoto huyo ambaye ni mwalimu kitaaluma.

AJABU LA NNE
Kana kwamba haitoshi, mtoto Nice ana ujasiri wa hali ya juu mbele ya macho ya watu, kwani haogopi tofauti na walivyo watoto wengi wa umri wake. Akiwa katika chumba cha habari cha gazeti hili, mtoto huyo alikuwa akijibu maswali mbalimbali aliyoulizwa kwa ufasaha na bila kuogopa na hata wakati kundi kubwa la waandishi waliokuwa wakishangaa uwezo wake walipompigia makofi, hakuonyesha kuwajali.

Kitendo cha kuzungukwa na watu wazima zaidi ya 60 waliokuwa chumba cha habari na yeye kutoonyesha uoga, kinaashiria kuwa kijana huyo anao uwezo wa kuhutubia hata mkutano wa hadhara bila hofu.
AJABU LA TANO
Kitu kingine kilichowaacha watu hoi, ni maelezo ya baba yake kuwa kijana huyo uelewa wake ni wa hali ya juu, kwani mara kadhaa anapojaribu kumuelekeza kitu, yeye hufanya mara mbili au tatu zaidi.

Nice Valentino akiwa na babaa'ke.
“Kuna siku nilimfundisha kuandika namba hadi nikafikia laki moja kwa tarakimu. Cha kushangaza, yeye aliweza kuniandikia tarakimu za milioni moja na kuitamka bila wasiwasi,” alisema.
AJABU LA SITA
Jambo lingine linalomtofautisha kijana huyo na hali ya kawaida, ni kitendo chake cha kuwa na uwezo wa kusoma maandishi yaliyoandikwa kwa lugha ya kiingereza tu, lakini hawezi kabisa kusoma maandishi ya Kiswahili au lugha nyingine yoyote.

“Anajua kusoma kwa ufasaha kabisa maneno yote ya kiingereza, jambo hili linatushangaza sana na hata anapozungumza, anajua vema kuhusu wakati uliopo, uliopita na hata ujao (tenses), lakini kama ukimwandikia kiswahili, anasoma kama Wahindi wanavyosomaga,” anasema baba yake.

...Akipozi.
AJABU LA SABA
Waandishi wetu walimuuliza kama anamfahamu msanii Diamond Platnumz, alisema hamjui, lakini alipoulizwa kama anajua kuimba wimbo wowote, aliimba wimbo wa dini (Gospel) kwa lugha ya kiingereza uitwao Glory to the Lord ulioimbwa na mwanamuziki aliyezaliwa mwaka 1950, Mmarekani Donald James ‘Don Moen’ unaomaanisha Utukufu kwa Bwana.

Ili kumsikia na kumuona mtoto huyo laivu akikokotoa mahesabu sambamba na mahojiano yote akiwa chumba cha habari, tembelea tovuti ya www.globatvtz.com

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...