Friday, January 30, 2015

ZITTO KABWE AWASILISHA TAARIFA MAALUM YA KAMATI KUHUSU HALI YA KIFEDHA NA UTENDAJI TTCL


Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe.

Mheshimiwa Spika,tarehe 21 Januari 2015, Kamati ilifanya kikao cha mashauriano kilichohudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Msajili wa Hazina, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Menejiment ya Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL). Lengo la kikao hicho likiwa ni kutafuta namna bora ya kuikwamua TTCL kutoka katika hali mbaya ya kifedha na kiutendaji ili iweze kuhimili ushindani uliopo katika sekta ya mawasiliano nchini.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kuelezea hali ya TTCL naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu kuwa TTCL ilianzishwa kwa Sheria ya Kampuni ya Simu Tanzania Na. 20 ya mwaka 1993 na kusajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni Na. 212, tarehe 31 Desemba 1993 baada ya kuvunjwa kwa lililokuwa Shirika la Posta na Simu Tanzania mwaka 1993. Hadi hivi sasa Hisa za TTCL zinamilikiwa na Serikali na Bharti Airtel Tanzania B.V kwa uwiano wa asilimia 65 na asilimia 35 sawia na hivi sasa kuna mazungumzo kati ya Serikali na Bharti Airtel juu ya Serikali kununua hisa asilimia 35 za Bharti Airtel ili imiliki asilimia 100 za TTCL.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa hesabu zilizokaguliwa, TTCL ilipata hasara ya Sh. 20.883 bilioni kwa mwaka 2012 na hasara ya Sh. 16.258 bilioni kwa mwaka 2013.

Mheshimiwa Spika, kutokana na TTCL kupata hasara kwa muda mrefu, takribani kwa miaka 10, Kampuni sasa imekuwa na jumuisho kubwa la hasara ambayo kwa mwaka 2013 imefikia jumla la Sh. 334.48 bilioni. Ukubwa wa hasara hii umeiondolea TTCL mvuto wa kukopeshwa na Taasisi za Fedha hata zile zenye nia ya kuikopesha.

Mheshimiwa Spika, ukosefu wa fedha za kutosha kutekeleza miradi ya Kampuni umekuwa kikwazo kwa TTCL kukabiliana na ushindani wa kibiashara. Kwa kipindi kirefu ufanisi wa TTCL kiuwekezaji na kifedha umeendelea kudorora. Aidha, tangu TTCL ibinafsishwe mwaka 2001, hakuna uwekezaji mkubwa uliofanyika na mpango wa kutafuta mkopo kutoka mabenki ya ndani na nje ya nchi unakwamishwa na masharti ya kupata udhamini wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, kukosekana kwa fedha za kutosha kuendesha Kampuni kumesababisha TTCL kushindwa kuboresha au kukarabati miundombinu inayoendelea kuchakaa. Hivi sasa karibu asilimia 50 ya miundombinu ya TTCL ni michakavu (obsolete) na inahitaji kubadilishwa na mitambo ya kisasa.

Mheshimiwa Spika, wingi wa hasara ikijumuishwa na uhaba wa uwekezaji umepelekea TTCL kuwa na mtaji hasi wa wanahisa (Negative shareholders Equity) ambapo mpaka kufikia mwaka 2013 TTCL imekuwa na mtaji hasi wa jumla ya Sh.87.896 bilioni. Hii ikitafsiriwa kitaalamu inamaanisha kuwa TTCL ni Kampuni muflisi.

Mheshimiwa Spika, mnamo mwaka 2005 Serikali iliipa TTCL mkopo wa jumla ya Dola za Marekani milioni 28 kwa ajili ya kulipa wafanyakazi waliostaafishwa, deni hilo halijalipwa mpaka sasa na limefikiwa jumla ya Sh. 76.6 bilioni pamoja na riba. Aidha, ukiacha deni hili TTCL inadaiwa na TCRA jumla ya Sh. 25 bilioni hivyo kufanya jumla ya deni kuwa Sh. 101.6 bilioni. Mheshimiwa Spika, Kamati inaona kuna umuhimu wa Serikali kufanya maamuzi ya haraka ya kuikwamua TTCL ili iweze kuendelea kutoa huduma kwenye Sekta ya Mawasiliano ikizingatiwa kuwa Kampuni hiyo ndiyo inayoendesha Mkongo wa Taifa, ina wafanyakazi ( 1549) wanaotegemea ajira katika Kampuni hiyo na inatoa huduma ya internet kwa makampuni mengine ya simu nchini

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...