Thursday, January 29, 2015

WABUNGE WATAKA WAZIRI MKUU NA CHIKAWE WAACHIE NGAZI


Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

BAADHI ya wabunge waliochangia hoja ya dharura bungeni leo wamewataka Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, wawajibishwe.

Hayo yametolewa wakati wa kujadili Hoja ya Dharura kuhusu kupigwa kwa baadhi ya viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) akiwemo mwenyekiti wake, Prof. Ibrahim Lipumba na baadhi ya wanachama wake juzi huko Mtoni-Mtongani jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda. 
SPIKA MAKINDA: Spika wa Bunge, Anne Makinda, alianza kwa kusema kuwa wabunge wachangie hoja hiyo kwa dakika tatu.WAZIRI CHIKAWE: Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, alianza kwa kusoma ripoti ya serikali kuhusu kilichotokea wakati wa mkusanyiko wa wanachama wa CUF. Alisema jeshi la polisi lilipokea taarifa kuhusu nia ya chama hicho kufanya maandamano na mkutano wa kuwakumbuka wanachama wa CUF waliouawa Januari 27, 2001 huko Zanzibar.

Aliongeza kwamba kutokana na masuala ya kiusalama jeshi la polisi liliona si vyema kuruhusu maandamano hayo lakini wafuasi wa chama hicho waliamua kukiuka amri hiyo na kukusanyika huko Mbagala Januari 27, mwaka huu ambapo walidhibitiwa na polisi.
Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahim Lipumba.

MWANASHERIA MKUU: Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. George Masaju, aliomba hoja ya dharura kuhusu polisi kuwapiga viongozi na wanachama wa CUF juzi isijadiliwe bungeni maana suala lipo mahakamani.

TUNDU LISSU: Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, alianza kwa kukataa wabunge kuchangia mada kwa dakika tatu, akisema Waziri Chikawe alikuwa amepewa dakika 30, na Mwanasheria Mkuu akipewa dakika 15.
Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Asema sheria inamruhusu mbunge kuchangia dakika zisizozidi dakika 15 hivyo Lissu alisema angetumia dakika 15 ila Spika aliingilia kati na kusema wangetumia dakika 10 na Lissu akakubali.Lissu alisema mrithi wa Werema (Mwanasheria Mkuu wa sasa, Mh. Masaju) si mshauri wa bunge akiongeza kwamba bunge likitaka ushauri litamfuata Katibu wa Bunge.

Aliongeza kuwa ‘waziri wa mapolisi’ (Chikawe) ameongea uongo na kudhihirisha kuwa kauli ya 'Wapigwe Tu' (iliyowahi kutolewa na Waziri Mkuu Pinda bungeni) si ya bahati mbaya.Alisema viongozi wa upinzani wanapigwa kwa kuwa kuna mafasisti serikalini na katika jeshi la polisi akiongeza kwamba kazi ya polisi si kukataza maandamano bali ni kuyaratibu.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe.

Alilijulisha bunge kuwa hivi sasa wapinzani wana kesi nyingi walizofunguliwa na polisi kwa njama wanazozijua na amelitaka bunge kuchukua hatua na kuwawajibisha Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kwa tukio hilo la juzi.

MHE. HABIB MNYAA: Mbunge wa CUF Mkanyageni, Habib Mnyaa, alisema ombi la kufanya maandamano lilipelekwa tangu Januari 22 na si 27 kama alivyosema Mh. Chikawe, mwaka huu na maandalizi yakafanyika ila jambo la kushangaza ni kwamba taarifa kutoka jeshi la polisi kusitisha maandamano hayo ilitolewa siku yenyewe ya maandamano asubuhi ya Januari 27, 2015.

Alihoji kwa nini nguvu zinazotumiwa na jeshi hilo kuwapiga wanachama wa CUF zisitumike kupambana na majambazi wanaovamia vituo kama kule Ikwiriri na Tanga?Katika kuhitimisha, alitaka jeshi la polisi livunjwe na Waziri Mkuu ajiuzulu.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.

MBOWE: Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, alisema amesikitishwa na taarifa iliyotolewa na Waziri Chikawe bungeni kwani alivyoongea na baadhi ya maofisa wa polisi makao makuu walimwambia agizo la kupigwa wafuasi wa CUF lilitoka ngazi za juu.

Akisisitiza alisema yeye na wenzake wamewahi kushambuliwa mara nyingi na jeshi hilo lakini pamoja na kuripoti kwenye vyombo husika mpaka sasa hakuna ufutialiaji wowote uliofanyika.
Asema baadhi ya wabunge wanacheka bungeni maana hawajawahi kujeruhiwa na polisi na wanaouawa na kupigwa na polisi si ndugu zao.
Mbunge James Mbatia.
Mbunge James Mbatia alisema uamuzi uliofanywa na serikali kuikimbizia mahakamani kesi dhidi ya Prof. Lipumba si sahii kwani zilikuwa ni njama za kutaka suala hilo lisijadiliwe bungeni.Hata hivyo, alimshukuru Spika wa Bunge kuruhusu mjadala ufanyike bungeni ambapo alisema ukweli utaliweka taifa letu huru, kwani mtu yeyote anayemwaga damu ya mwenzake ni gaidi na hawezi kuvumiliwa. Mbatia aliongeza kuwa vitendo hivyo vilivyofanywa na polisi vinajenga uhasama ndani ya taifa letu na akawataka waliohusika katika tukio la juzi wachukuliwe hatua kali za kisheria na za kijeshi kwa kukiuka maadili ya polisi

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...