Monday, March 3, 2014

MAKUNDI BUNGE LA KATIBA NI MPASUKO


NIMSHUKURU Mungu kwa kuniwezesha kuwa nanyi leo na kuniwezesha kuandika haya nitakayoandika hapa, hakika Mungu ahimidiwe.


Hivi sasa kuna mkusanyiko wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba bungeni Dodoma, awali kukutana kwao kulitia faraja na matumaini na wananchi wakawa na matarajio na matamanio makubwa kuona katiba mpya inakuja baada ya mijadala makini ya wajumbe.

Wengi tunatarajia kuona Tanzania ya kesho ikiwa na haki, usawa, amani, furaha na maendeleo ya kweli badala ya kusikia ajenda za kizandiki ambazo baadhi ya wajumbe wametumwa na makundi yao.

Naamini makundi hayo yatazimwa na nguvu ya umoja, fikra pevu na uzalendo wa Kitanzania bila kujali itikadi za kisiasa. Tunapojadili katiba, chama kikae pembeni kwa manufaa ya Watanzania wote bila kujali itikadi.

Mungu autangulie mjadala wa Bunge la Katiba uzae matunda mema kwa nchi yetu ili unufaishe watu wote, sasa na vizazi vijavyo. Kinachotakiwa ni kuwa rasimu ya Tume ya Joseph Warioba ndiyo iwe msingi wa majadiliano kwa sababu wajumbe walizunguka nchi nzima na kupata maoni ya raia.

Hakuna siri kwamba, ukifuatilia mijadala ndani ya Bunge Maalum la Katiba utagundua kuwa kuna makundi mbalimbali yameibuka na hasa kwa wanasiasa licha ya kuonywa na Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete mara kwa mara kuhusu hilo.

Katiba ya sasa ilikuwepo enzi za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambako Watanzania walisomeshwa bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu. Katiba hiyohiyo ipo hadi leo ambako kuna ubaguzi mkubwa kwenye elimu. Hayo ndiyo ya kuangalia.

Hivi sasa wanyonge wametengwa, wanasoma elimu duni ilhali matajiri na watoto wa wenye uwezo wakiwemo wanasiasa wanapewa elimu inayowaandaa kuajiriwa, kukopesheka kwenye benki na kurithi vyeo vya baba zao.

Katiba ya sasa ambayo inaonekana imepitwa na wakati haina kipengele hata kimoja kinachoruhusu viongozi kuwa wezi, mafisadi, watumiaji wabaya wa fedha za umma, lakini watu wanafanya hayo.
Matendo hayo yamekithiri kwenye ofisi za umma, tumeshuhudia mikataba mibovu mingi isiyonufaisha nchi. Katiba mpya imulike hayo na kutoa dawa.

Ukweli ni kwamba hakuna nchi duniani ambayo imeendelea kutokana na kuwa na katiba nzuri bali yameletwa na raia wanaojitambua, wanaochagua viongozi sahihi wenye maarifa, wabunifu na wanaojituma.

Makundi ndani ya Bunge Maalum la Katiba pia yameanza kuleta mpasuko ki-nchi kwani suala la uwiano wa wajumbe katika bunge hilo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar (Hawasemi Tanzania Visiwani), lilizua malumbano huko Dodoma yaliyotokana na mjumbe, Said Ally Mbarouk, kueleza kuwa Zanzibar kwa muda mrefu imekuwa ikionewa na kudhulumiwa.

“Sisi Wazanzibari kwa muda mrefu tumekuwa tukilalamika kuwa Watanganyika wamekuwa wanatuonea, wanatudhulumu katika Muungano huu. Mara nyingine mjadala wa malalamiko haya hufanyika katika Baraza la Wawakilishi ambalo wewe mheshimiwa Mwenyekiti (Pandu Ameir Kificho) ni Spika,” alisema Mbarouk.

Kauli hiyo ilimfanya Job Ndugai ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kusimama na kujibu, alisema kuna umuhimu wa wajumbe kuwa na umakini katika lugha wanazozitumia kwenye vikao vikubwa kama hicho.

“Lugha ni muhimu sana. Utu wa mtu uko katika lugha...kitu muhimu ni kujenga hoja ili wenzako wakuunge mkono,” alisema na kuongeza: “Lakini anaposimama mtu akasema kwa miaka 50 ya Muungano huu kumekuwa na dhuluma na uonevu na mambo kama hayo ehh, haya bwana.”
Ukweli ni kwamba sasa wenzatu wa Zanzibar wamepata nafasi kwa kushirikiana na Watanganyika kuimarisha Muungano wetu.

Tahadhari kwa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba ni kwamba wasipokuwa makini mkutano wao unaweza kuzaa Katiba itakayoendeleza kero ama kusambaratisha kabisa Muungano kama ambavyo imetokea kwenye nchi nyingine duniani zilizokuwa zimeungana.

Nionavyo mimi ni kwamba Bunge hilo ndiyo mahali ambapo watu wanaweza kutoa madukuduku yao katika nyanja mbalimbali lakini kwa kutumia lugha za kistaarabu na kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa niaba ya Watanzania wote.

Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

No comments:

Post a Comment

POSTED TITLE

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...